
Vurugu kubwa zimeibuka jana Jumanne, Februari 17, 2026 usiku katika mchezo wa mchujo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baina ya Benfica na Real Madrid kwenye Uwanja wa De Luz baada ya mshambuliaji wa Madrid, Vinicius Jr, kudaiwa kufanyiwa ubaguzi wa rangi huku mwenzake Trent Alexander-Arnold akitaja tukio hilo kuwa “fedheha kwa soka.
Mchezo ulisimamishwa kwa dakika 10 baada ya mwamuzi Francois Letexier kuonyesha ishara ya kuvuka mikono, kuashiria kuripotiwa kwa tukio la ubaguzi wa rangi.
Katika mkasa huo, kocha wa Benfica, Jose Mourinho, pamoja na mmoja wa maofisa wa benchi la ufundi la klabu hiyo, walioneshwa kadi nyekundu.
Vinicius, ambaye baadaye aliwaita wabaguzi wa rangi “waoga” kupitia taarifa yake, alikuwa amefunga bao la kwanza na hatimaye la ushindi kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Letexier kwa kusherehekea bao hilo kwa kucheza kwa namna iliyotafsiriwa kuwachokoza mashabiki wa Benfica.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 25, alikasirishwa na kauli aliyodai kuambiwa na winga wa Benfica raia wa Argentina,
Vinicius anadai aliitwa “tumbili”, lakini kiungo wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mchezaji wa Benfica alidai kutumia matusi ya chuki dhidi ya ushoga, si ya kibaguzi.
Tukio hilo limeibua mitazamo tofauti ambapo kuna upande unaoamini Vinicius alibaguliwa huku mwingine ukionekana kutokukubaliana na hilo.
Beki wa Real Madrid, Alexander-Arnold alisema matukio hayo yalikuwa “ya kuchukiza” akionekana kuchukizwa na kile ambacho Vinicius alifanyiwa.
Hata hivyo Meneja wa Benfica, Jose Mourinho ameonekana kutoamini kama Vinicius alibaguliwa.
“Benfica si klabu ya kibaguzi. Hilo ndilo jambo la mwisho kabisa,” amesema Mourinho.