Marekani.Msanii wa Hip Hop kutokea Marekani,  50 Cent, alianza kuwa baba kabla hajapata mafanikio makubwa katika muziki lakini uhusiano kati yake na mwanaye mkubwa, Marquise (29), umekuwa na misukosuko mingi.

Kwa muda mrefu wawili hao wamekuwa hawapatani na hata kuvunjiana heshima, huku migogoro yao mingi kuhusu malezi na fedha ikijadiliwa kwa uwazi mkubwa kupitia mitandao ya kijamii.

Mkali huyo wa kibao cha In Da Club (2003), alijaliwa mtoto huyo mnamo Oktoba 1996 katika uhusiano na aliyekuwa mpenzi wake, Shaniqua Tompkins ambaye waliachana kwa drama nyingi. 

MMNYU 01
MMNYU 01

Wazazi hao walikuwa pamoja miaka ya 1990, uhusiano ambao kwa muda mrefu ulibeba tabia ya kuvunjika na kurudiana, kisha kuja kuachana kabisa ila waliendelea kuvutana mahakamani kuhusu malezi. 

Kwa ujumla, 50 Cent ni baba wa watoto wawili, mwingine ni Sire Jackson (2012) aliyezaa na Daphne Joy kabla ya kuachana. Na kwa leo, tutaangazia mgogoro kati yake na mtoto wake mkubwa, Marquise.

Baada ya kuachana, 50 Cent na mzazi mwenzie, Shaniqua waliingia kwenye mvutano mkali na wa muda mrefu wa kisheria kuhusu malezi ya Marquise, mgogoro ambao haukupata muafaka rasmi hadi Oktoba 2008.

MMNYU 07

Wakati wa mzozo huo, 50 Cent alikiambia kituo cha MTV kuwa uhusiano wake na mwanaye umebadilika kwa kiasi kikubwa na hiyo ni kwa sababu yeye na mama mtoto hawakuwa tena marafiki.

“Kwa sasa ili kumpata mtoto kuna njia tofauti za kufuata kuna mawakili walioteuliwa na mahakama, hivyo inabidi nizungumze na wakili wake ili nipate ruhusa ya kumchukua,” alisema 50 Cent na kuongeza.

“Uhusiano kati ya fedha zangu na mama yake umebadilika. Alisema mambo mengi mabaya kunihusu ambayo sikuwahi hata kuyatarajia kutoka kwake,” alieleza rapa huyo 2008.

MMNYU 04

Katika makubaliano ya mwisho kuhusu malezi, 50 Cent alipata haki ya kumuona mtoto, akiruhusiwa kuwa naye mwishoni mwa wiki moja kila mwezi pamoja na kipindi cha sikukuu na likizo.

Hata hivyo, chanzo kimoja kililiambia Jarida la People hapo 2018 kuwa, licha ya kumsaidia mwanaye kifedha hadi alipofikisha umri wa miaka 18, 50 Cent amekuwa hana mawasiliano ya karibu naye kwa miaka mingi.

Mwaka 2017, Marquise aliuambia mtandao wa Rap-Up kuwa uhusiano na baba yake uliharibika alipokuwa na umri wa miaka 10 au 11. Alieleza hakuwa karibu naye vya kutosha, na kadri muda ulivyoenda na matukio mbalimbali kutokea, uhusiano wao ulidhoofika.

MMNYU 06

“Binafsi nilianza kumuangalia tofauti kwa sababu nilipokuwa mdogo, baba yangu alikuwa shujaa wangu. Alikuwa anaonekana kwenye televisheni, anafanya hivi na vile, alikuwa akinipeleka shule,” alieleza.

“Ilikuwa kama kuwa na baba aliye na nguvu za ajabu. Lakini unapokua, unaanza kugundua mambo au kuona mifumo fulani ya maisha, na hilo linaathiri uhusiano wako na watu.

MMNYU 02

“Hicho ndicho kilichotokea kati yangu na baba yangu. Bado yuko hai, lakini siwezi hata kukuambia mara ya mwisho tulizungumza au hata kuwa na mazungumzo ya kawaida ilikuwa lini,” alisema Marquise.

Mnamo Desemba 2018, uhusiano wao ulifikia hatua mbaya zaidi pale 50 Cent alipotoa kauli iliyozua hasira na maoni mseto kwa mashabiki kwenye picha ambayo Marquise aliiposti Instagram.

MMNYU 05

Marquise aliposti picha akiwa na mtoto wa Kenneth ‘Supreme’ McGriff ambaye ni mpinzani wa muda mrefu wa 50 Cent, kitu ambacho kilimkasirisha sana rapa huyo.

Ikumbukwe McGriff anatuhumiwa kuhusika katika njama ya kumuua 50 Cent, tukio lililosababisha rapa huyo kupigwa risasi mnamo Mei 2000. Kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha jela kwa makosa mengine yasiyohusiana na tukio hilo.

Katika picha hiyo ya Marquise akiwa na mtoto wa McGriff, 50 Cent alitoa maoni makali ambayo yaliwakera wengi, akisema kuwa asingejali chochote endapo watoto hao wangepata ajali!

MMNYU 03

Chanzo kimoja baadaye kilidai Marquise hufanya mambo ya aina hiyo ili kumchokoza baba yake, na kwamba kila mara 50 Cent anapokuwa na mgogoro na mtu kwenye mitandao, mwanaye hujitokeza kwa makusudi.

Baada ya kukosolewa vikali na wengi kuhusu kauli yake, 50 Cent aliandika kwenye mtandao wa X akisema hana chuki wala nia mbaya kwa mtu yeyote aliye hai.

“Watu anaowatazama kama mfano, ni wenye mitazamo hasi dhidi yangu. Nimempa mama yake Dola 1,360,000 (Sh3.3 bilioni) kama msaada ili kumpa fursa ambazo mimi sikuwahi kuzipata,” alieleza 50 Cent.

Mvutano kati ya 50 Cent na Marquise uliendelea tena Oktoba 2022, pale Marquise alipompa baba yake ofa ya Dola 6,700, wastani wa Sh16.5 milioni ili wakutane na kuwa pamoja kama familia. 

“Mtu mmoja amwambie baba yangu nitamlipa Dola 6,700 kwa saa 24 tu za muda wake ili tufanye kila kitu nilichotamani kufanya naye nikiwa mtoto,” alieleza Marquise katika Instagram.

Baadaye mwezi huo huo, 50 Cent alipohojiwa kwenye kipindi cha The Breakfast Club, alidai kuwa mwanaye hataki kukaa naye mezani ili wazungumze.

“Kama umemtumia mtu zaidi ya dola milioni moja, halafu hana heshima yoyote kwako, unadhani unatakiwa umpe kiasi gani ili angalau akupe heshima kidogo?” Alihoji 50 Cent.

Baada ya mahojiano hayo, Marquise aliandika kwenye Instagram akisema hana namba ya baba yake na hata alipojaribu kumpata kwa njia nyingine kama mitandao ya kijamii, aliishia kuzuiliwa (block).

“Mimi si mtoto tena, hakuna mama anayehusika hapa. Sitaki wala sihitaji fedha zako. Ninasimama kwa miguu yangu mwenyewe. Sipendi kutafuta umaarufu; nilikuwa na fursa nyingi za kufanya hivyo lakini niliamua kutozitumia,” alieleza. 

“Niliangalia mahojiano yako, hayakuonyesha uwajibikaji  kulikuwa na majivuno, kulaumu na kuzungumzia zaidi fedha, kana kwamba wewe ndiye mtoto kwenye sakata hili. Nimekusamehe kwa hilo, niko tayari wakati wowote utakapoamua kukaa chini tuzungumze,” alisema Marquise.

Licha ya yote hayo, Marquise amefuata nyayo za baba yake katika muziki. Alitoa wimbo wake wa kwanza, Different (2017) na tangu wakati huo ameachia nyimbo kadhaa ingawa bado hajapata uungwajii mkono kutoka kwa mashabiki wengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *