Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ameeleza mtazamo wake kuhusu dhana ya kustaafu siasa, akisema neno kustaafu ni maalumu kwa utumishi wa umma.

Hoja hiyo ya Wasira (80) inajibu maswali kadhaa ya wadau wa siasa ambao mara nyingi wanahoji umri wake na wakongwe wengine kuendelea kushika nyadhifa ndani ya vyama na Serikali, ilhali kuna vijana wanaotajwa kuwa na uwezo.

Wengine wanakwenda mbali zaidi na kusema ni vema watu wazima wakastaafu siasa za uongozi ndani ya vyama na Serikali, kuwapisha vijana.

Wasira ametoa mtazamo huo alipozungumza na Mwananchi wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Chama cha Mapinduzi Lumumba, jijini Dar es Salaam.

‘Wanastaafu watumishi’

Katika maelezo yake, kiongozi huyo wa juu wa CCM amesema dhana ya kustaafu ni maalumu kwa utumishi wa umma, lakini si siasa.

“Mimi sielewi maana ya kustaafu. Kustaafu ni hoja iliyopo katika utumishi wa umma, ukifika miaka 60 unaambiwa sasa umestaafu, na kweli unastaafu, unatoka ofisini na hurudi tena,” amesema Wasira aliyezaliwa Julai mosi, 1945.

Katika siasa, amesema kuna aina mbili za utendaji, ikiwemo siasa ngumu na siasa nyepesi, akifafanua kwa umri wake na nafasi aliyonayo ndani ya CCM, anafanya siasa nyepesi.

Amesema siasa ngumu ni kama kuusaka ubunge na urais, ambako kuna kushindwa, lakini siasa nyepesi ni kushauri kama nafasi aliyonayo sasa ndani ya chama chake.

“Mimi ni Makamu Mwenyekiti. Kazi yangu ni kushauri na kumshauri Mwenyekiti, kwa kuwa mimi ni makamu wake na si mtendaji wake. Nafanya siasa laini, na ukiona tunavyofanya ni kama hobi. Ukisema tustaafu, itafikia hatua utasema tusipige hata kura. Lakini kura ni siasa, wanapiga majaji na wanajeshi,” amesema.

Katika maelezo yake, Wasira amesema kuna wanaohoji kwa nini amepewa wadhifa wa Makamu Mwenyekiti CCM Bara ilhali ni mtu mzima.

“Wanashindwa kujua kuwa umakamu una sifa zake. Kwanza, lazima uwe na uzoefu wa kutosha, asije akapewa mtu cheo halafu akakimbia. Anaongoza watu wa CCM, ni makamu gani huyo? Lakini wao wanajua umri wangu, wananipa heshima, na vilevile wanaiheshimu historia yangu na maadili ninayoyasimamia,” amesema.

Wasira amesema ndani ya chama hicho anasimamia maadili, eneo gumu ambalo huwezi kulisimamia bila kuwa na maadili binafsi. Unaweza kutaka kumwajibisha mtu, lakini baadaye akakuuliza, “Mbona na wewe ulifanya?”

“Ni nafasi laini, lakini ina sifa za uzoefu zinazokusaidia kukibeba chama. Pia unakuwa kama refa mzuri asiye na upande,” amesema.

Nipo, nitakuwepo

Alipoulizwa kuhusu utani wa Makongoro Nyerere unaomweleza yupo tu, amesema, “Nipo kwa sababu Mungu ametaka niwepo. Ukiwa hai, utatoa mchango kulingana na mazingira yaliyopo. Hata nisingekuwa kiongozi, ningekuwapo tu, ningekuwa nyumbani kwangu, bado mngekuja kuniuliza maswali yanayotokana na kile ninachokijua.”

Amesema hata akiacha uongozi, ataendelea kuwapo na kuishi na jamii. Ikihitaji mawazo, itaendelea kuyapata. Hilo haliwezi kuwa hoja, maana kuna mwingine anaweza kuuliza kwa nini hajafa.

Wasira amesema si kweli kwamba amehudumu katika awamu zote za uongozi, isipokuwa amefanya kazi katika Serikali tatu pekee, kuanzia enzi za Julius Nyerere alipokuwa bado angali kijana.

“Niliingia bungeni nikiwa na miaka 25 baada ya kuchaguliwa, na baadaye nikaingia katika uteuzi wa Rais Nyerere nikiwa na miaka 27. Ninasema hivi kwa sababu kuna wanaodhani Wasira ni mtu wa zamani sana au kunifananisha na rika la kina Rashidi Kawawa,” amesema.

Kwa mujibu wake, alianza siasa akiwa kijana, aliingia bungeni akiwa na umri wa miaka 25, na baadaye alipofikisha miaka 27 aliteuliwa na Rais Nyerere kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

“Niliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara nikiwa na miaka 30. Tangu wakati huo miaka imekuwa ikisonga, wengine wamezaliwa wakinikuta madarakani na kunisikia. Leo wanauliza Wasira ni nani. Wasira ni mtu wa kawaida tu, isipokuwa ni kiongozi na mtumishi wa umma,” amesema.

Amesema amekuwa mtumishi wa umma katika Serikali za Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, na Jakaya Kikwete na kwamba hakuhudumu katika Serikali ya Benjamin Mkapa wala ya John Magufuli, na kwa sasa hayupo katika Serikali ya Samia Suluhu Hassan.

Katika kipindi chote hicho, amesema, amekuwa mwanachama wa CCM. Enzi za Mwalimu alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu kwa kuwa alikuwa Katibu wa chama cha Tanganyika African National Union (Tanu), wakati ambao wakuu wa mikoa pia walikuwa makatibu wa chama.

Amefafanua kuwa alikuwa katibu wa chama na Mkuu wa Mkoa wa Mara kuanzia mwaka 1975 hadi 1982, kushika nyadhifa hizo kulimfanya awe moja kwa moja mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama.

“Nilikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Tanu kuanzia 1975 hadi 1977, hivyo nilishiriki kuvunja Tanu na kuanzisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuunganisha na Afro-Shirazi Party (ASP),” amesema.

Amesema alipoingia katika utawala wa Mwinyi, aligombea nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu akiwa Waziri wa Kilimo, ingawa wakati wa Mkapa hakushiriki kwa kiwango kikubwa katika shughuli za kichama.

“Katika kipindi chote cha miaka 10 ya utawala wa Kikwete, nilikuwa waziri na pia mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, na baadaye Kamati Kuu. Niliendelea kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa hadi wakati wa Magufuli, na baadaye nikaingia katika uongozi chini ya Rais Samia hadi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara,” amesema.

Mzee Wasira mkali?

Katika majibu yake, amekiri kuwa ni mkali katika mambo yasiyoenda vizuri. Hata hivyo, amesema ukali huo unatokana na ahadi ya mwanachama wa CCM kwamba binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja.

“Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote. Nitaitumia nafasi yangu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa, na dhuluma. Haya huwezi kuyatekeleza bila ukali wa kiasi. Lakini ukali usio na mipaka unamfanya mtu kuwa wa ajabu. Kuhusu rushwa, sitatoa wala kupokea. Huwezi kupinga rushwa huku ukibembeleza watu,” amesema.

Wasira kuitwa Tyson

Amesema kuitwa kwake Tyson ni utani, na wala hakuhusiani kwa namna yoyote na mchezo wa masumbwi, hajui kupiga ngumi hata kidogo, na si kweli kuwa ana uhusiano wowote na mchezo huo.

“Kuitwa Tyson ni utani tu. Kuna mwaka mmoja niliwahi kugombea ubunge dhidi ya mzee Joseph Warioba. Wakati huo kulikuwa na bondia aliyeitwa Mike Tyson, na tukio hilo lilitokea Bunda. Baada ya kushinda uchaguzi huo, jina la Tyson likaanza kuzoeleka kwangu, kama unavyowajua vijana wa siku hizi,” amesema.

Amesema baadaye alikutana na Jakaya Kikwete, akidai naye ni msanii kidogo. Akaanza kumuita Tyson, na jina hilo likaendelea kusambaa. Baada ya kuona hali hiyo, aliwapiga marufuku waandishi wa habari wasimuite kwa jina hilo.

“Kwa sababu mkiendelea kuniita Tyson, jina langu halisi litapotea. Siku hizi kuna watu wanaitwa majina ambayo si yao kabisa, hivyo nilipambana kuzuia hali hiyo ili nisipoteze utambulisho wangu,” amesema.

Kuwa na muendelezo

“Sasa hiyo si hoja yangu, hiyo ni hoja ya Mungu. Huwezi kuniuliza kwa nini nimekuwa na muendelezo. Ni namna Mungu alivyonijalia hekima na busara ninazozitumia bila kuzua mgogoro,” amesema.

Amesema wanaotaka kujua alisema nini jana na leo anasema nini, atawajibu aliutumia vizuri uanasiasa wake kwa kusema mambo huku akijua kuwa kesho mambo hayo anayoyasema yanaweza kumshtaki.

“Unatakiwa kusema kwa uangalifu, na Mungu amenijalia uwezo huo. Ni kipaji. Wengine wanapofikia umri kama wangu hupoteza kumbukumbu, mimi sijapoteza. Wala mimi si mkubwa kuliko wengine, kuna kaka zangu wengi hapa waliokuwa na Mwalimu au katika utumishi wa umma na kwenye chama, na bado wapo,” amesema.

Amesema watu hao, bila kuwataja majina, wamekuwa wakitoa maoni na hawajapoteza kumbukumbu. Hata hivyo, katika maelezo yake aligusia video mjongeo inayosambaa mitandaoni inayoeleza Wasira bado yupo.

Katika ufafanuzi wa majibu yake, amesema: “Huo ni utani wa Makongoro Nyerere. Makongoro ni msanii, hivyo alitumia usanii wake wakati ule alipokuwa anagombea urais na mimi nilikuwa nagombea. Labda aliona inaweza kumsaidia,” amesema.

Amesema baada ya kauli hiyo walikaa na Makongoro, wakazungumza, na wakaona ulikuwa utani wa kisiasa, na jambo hilo likaisha. Amefafanua kuwa ni kipande cha video ambacho watu wanakitumia, lakini hakina maana yoyote.

“Nipo kwa sababu Mungu ametaka niwepo. Ukiwa hai, utatoa mchango kulingana na mazingira yaliyopo. Hata nisingekuwa kiongozi, ningekuwapo tu, ningekuwa nyumbani kwangu, bado mngekuja kuniuliza maswali yanayotokana na kile ninachokijua,” amesema.

Amesema hata akiacha uongozi, ataendelea kuwapo na kuishi na jamii. Ikihitaji mawazo, itaendelea kuyapata. Hilo haliwezi kuwa hoja, maana kuna mwingine anaweza kuuliza kwa nini hajafa.

“Hoja ya mimi kutokufa itajibiwa na Mungu, si mimi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *