Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema, wana wasiwasi mkubwa kuhusu madhara yanayoweza kuwapata waathirika waliotajwa katika nyaraka zinazojulikana kama “Mafaili ya Epstein” (Epstein Files), na kueleza kwamba mchakato wa utoaji wa taarifa hizo haukulinda ipasavyo faragha na usalama wao.

Wataalamu hao aidha, wametaka hatua stahili za kisheria zichukuliwe kwa wale wote waliotajwa katika nyaraka hizo kwa mujibu wa sheria.

Katika taarifa yao iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi wataalamu hao wa haki za binadamu wa UN wamesema, kushindwa kulinda taarifa nyeti za waathirika wakati wa kuhariri nyaraka hizo kumeweka manusura katika hatari ya kulipiziwa kisasi, kunyanyapaliwa na kupata maumivu mapya ya kisaikolojia. Baadhi ya madhara yalitokea hata kabla kumbukumbu zilizo na taarifa nyeti kuondolewa rasmi.

Kwa mujibu wa wataalamu, “Mafaili ya Epstein” yana ushahidi wa kushtua na unaoaminika wa udhalilishaji wa kingono, biashara haramu ya binadamu na unyonyaji wa wanawake na wasichana kwa mtindo wa kimfumo na wa kimataifa.

Vitendo vilivyobainishwa kwenye mafaili hayo vinaweza kujumuisha utumwa wa kingono, ukatili wa uzazi, kutoweka kwa lazima, mateso, vitendo vya kinyama na vya kudhalilisha utu, pamoja na mauaji ya wanawake.

Wataalamu hao wamebainisha kuwa, uhalifu huo ulitendeka katika mazingira yaliyojaa ubaguzi wa rangi, rushwa, chuki kali dhidi ya wanawake, na mtazamo wa kuwafanya wanawake na wasichana kuwa bidhaa pamoja na kuwavua utu wao.

Kundi moja la manusura hivi karibuni lilikutana na Mtaalamu Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, likieleza hisia za kurejea katika maumivu ya awali na kile walichokiita “udanganyifu wa kitaasisi” kufuatia kusuasua kwa uwazi na uchunguzi mpana.

Halikadhalika, wataalamu hao wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamewapongeza waathirika kwa ujasiri na ustahimilivu wao katika kudai haki, licha ya gharama kubwa binafsi wanazobeba…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *