Baada ya mwanzoni kuonekana kuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kutokana na tofauti kubwa ya pointi walizokuwa nazo dhidi ya wapinzani wao, sasa upepo umebadilika ndani ya Arsenal baada ya timu hiyo kuanza kupoteza makali yake ya kupambania taji hilo la EPL.
Kocha, Mikel Arteta, ameonyesha kukerwa na kiwango cha wachezaji wake kufuatia matokeo ya sare dhidi ya Wolves, akisema timu yake inapaswa kuonyesha kiwango kinachotakiwa katika mbio za ubingwa.
Arsenal wameshindwa kulinda uongozi wa mabao 2-0 na kuruhusu bao la kusawazisha dakika ya 94 dhidi ya Wolverhampton Wanderers, jambo lililowagharimu nafasi ya kujitanua kileleni mwa msimamo.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, akionekana kushangazwa na matokeo baada ya Wolves kusawazisha mabao mawili katika mechi ya Ligi Kuu England. Picha na Mtandao
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Arteta amesema lawama na ukosoaji wowote ni halali kutokana na kiwango walichoonyesha.
“Nadhani swali lolote, ukosoaji wowote au maoni yoyote, leo tunapaswa kuyakubali. Risasi yoyote, pokea, kwa sababu hatukucheza katika kiwango kinachotakiwa,” amesema kocha huyo wa Arsenal.
Ameongeza kuwa timu yake ilikuwa butu katika umiliki wa mpira na ilifanya makosa mfululizo yaliyowapa Wolves nafasi ya kurejea mchezoni.
“Baada ya kufunga bao la pili, tulipotea mchezoni. Tulikuwa tunapoteza mipira mara kwa mara. Kipindi cha pili hatukucheza katika kiwango kinachohitajika kushinda mechi ya Ligi Kuu,” amesema.
Alipoulizwa kama presha ya mbio za ubingwa dhidi ya Manchester City inawaathiri kisaikolojia, Arteta hakukataa.
“Chochote anachosema mtu kinaweza kuwa sahihi, kwa sababu hatukufanya tulichopaswa kufanya,” amesema, akisisitiza kuwa uimara wa timu utaonekana katika namna watakavyojibu mechi ijayo, si kwa maneno.
Kiungo wa Arsenal, Declan Rice akionekana mwenye huzuni baada ya mechi dhidi ya Wolves kuisha kwa sare ya mabao 2-2. Picha na ,Mtandao
Kwa matokeo hayo, Arsenal inaweza kubaki na tofauti ya pointi mbili tu endapo Manchester City watashinda mechi yao dhidi ya Newcastle.
Kwa upande wa Wolves, kocha Rob Edwards ameusifia moyo wa kupambana wa wachezaji wake baada ya kurejea kutoka nyuma.
“Ilikuwa ni wakati mzuri sana. Ni sare tu, lakini kurejea kutoka 2-0 dhidi ya moja ya timu bora Ulaya ni jambo la kipekee,” amesema Edwards.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto walizopitia msimu huu, hawajakata tamaa na wataendelea kupambana hadi mechi ya 38 ya msimu.
“Tunahitaji kujenga mwendelezo na muunganiko. Najua kuna presha, lakini wachezaji wanapambana kwa bidii. Leo kulikuwa na nguvu nzuri sana uwanjani, tunapaswa kuendelea nayo,” amesema.
Sare hiyo imezua maswali mapya kuhusu uwezo wa Arsenal kuhimili presha ya mbio za ubingwa, huku mashabiki wakisubiri kuona kama watajibu kwa ushindi katika mechi zijazo au wataendelea kuyumba katika hatua za mwisho za msimu.