Kigoma. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimewaahidi wananchi wa Uvinza mkoani Kigoma kufuatilia kwa ukaribu mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kata ya Nimpenda Kitongoji cha Msoma, Kijiji cha Mpeta na mwekezaji.
Kwa mujibu wa wakazi wa Mpeta, katikati ya sakata hilo, mwekezaji huyo anadaiwa kuwakodisha ardhi wananchi kwa gharama ya Sh150,000.
Ahadi hiyo, imetolewa kwa nyakati tofauti na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi wakati akizungumza na wananchi majimbo ya Kigoma Kaskazini na Kusini leo Alhamisi Februari 19, 2026 katika mkutano wa hadhara.
Kabla ya kutoa ahadi hiyo, Kihongosi amewaambia wananchi wa Kigoma kuwa wajibu wa CCM ni kusikiliza wananchi na kila aina ya shida itasikilizwa bila upendeleo wala ubaguzi.
“Hapa panaonekana kuna mgogoro mkubwa unaohitaji ufumbuzi. Niwaambie kama mna haki yenu katika sakata hili mtaipata mapema kwa sababu Rais Samia Suluhu Hassan ni muumini wa kusimamia haki,” amesema Kihongosi.
Kuhusu ukodishaji Kihongosi amesema, ” kama hilo jambo lipo, basi batili kwa sababu hakuna mwekezaji anayechukua ardhi kisha kuwakodisha tena wananchi, bali anatakiwa kuwekeza, CCM itafuatilia.
“Tutafuatilia uwekezaji wake umeanza lini, gharama zake, amewekeza ekari ngapi? Tutakwenda kujiridhisha kwa sababu yapo maeneo yanayohodhiwa ndani ya nchi, lakini hayaendelezwi, ndio maana Serikali iliwanyang’anya,” amesema Kihongosi.
Mwenezi huyo, amesema kuna viongozi wanaotajwa kuwa na maeneo na kuchochea mgogoro huo, akiahidi kufuatilia suala hilo kwa kina ili kujua ukweli halisi.
Hata hivyo, mwenezi huyo ameuagiza uongozi wa mkoa wa Kigoma kuandaa taarifa inayoanisha kiini cha mgogoro huo na utatuzi wake upoje na kama kuna jambo limekwenda kinyume waliohusika wachukuliwe hatua.
“Hapa ofisi ya mkoa inipe ripoti kabla sijatoka Kigoma, kuhusu taarifa ya mgogoro huu. Naomba muwe watulivu na kuwa na imani na Serikali, hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe jingine katika kuminya haki za wananchi,” ameeleza.
Chimbuko la ahadi hiyo, ilitokana na salamu za Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM) Nuru Kashakari ‘ Kandahari’ aliyezungumza kwa niaba ya wananchi akidai wakazi wake Musoma wanadhulumiwa haki zao na kuondolewa katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Kandahari, baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, bado kuna changamoto kubwa ya ardhi akidai wananchi wanadhulumiwa ikiwemo kuondolewa na kunyang’anywa.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi akizungumza na wanachama na wananchi waliojitokeza wakati mwenezi huyo alipokwenda kutembelea shina la 11 la chama hicho la Kidahwe Jimbo la Kigoma Kaskazini
“Wananchi wa jimbo la Kigoma Kusini wamekuwa kama manamba, tunaomba kupata haki zao si kunyang’anywa ardhi na wawekezaji waliopewa ardhi hawajaiendeleza,” amesema Kandahari.
Kihongosi amewaambia wananchi wa Kidahwe jimbo la Kigoma Kaskazini kuwa ziara yake pamoja na mambo mengine imejikita kutatua kero zinazowakabili wananchi na kuangalia uhai wa chama hicho tawala.
Pia, Kihongosi amesema Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara yenye lengo la kuimarisha na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji mkoani Kigoma.
“Asiwadange mtu maendeleo huwezi ukalala yakaja, bali ni mchakato leo unajenga barabara kesho miundombinu ya elimu na umeme kisha maji,” amesema Kihongosi.