Rio De Janeiro, Brazil. Kiungo Philippe Coutinho aliyewahi kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi katika historia ya soka ana hali mbaya akiwa na klabu ya Vasco da Gama ambako mashabiki wamekuwa wakimzomea kila aingiapo uwanjani hali inayosababisha kutaka kuvunja mkataba wake.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa akishuka kiwango kila siku na hajawahi kurudi katika kiwango chake tangu afanye uhamisho wa Pauni 145 milioni kutoka Liverpool kwenda Barcelona mwaka 2018.

Coutinho alirejea Vasco ambayo ni timu yake ya utotoni msimu uliopita kwa mkataba wa miaka mitatu, lakini inaonekana safari hiyo tayari inaelekea mwisho baada ya kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Brazil, staa huyu anapanga kusitisha mkataba wake na tayari rais wa klabu Pedrinho ameshawaambia baadhi ya wafanyakazi staa huyo anataka kuondoka.

Kiungo wa zamani wa Barcelona na Liverpool, Philippe Coutinho ambaye pia aliwahi kucheza Inter Milan, Bayern Munich na Aston Villa. Picha na Mtandao

Inaelezwa uongozi wa klabu ulishtushwa na uamuzi huo na kocha alijaribu kumshawishi Coutinho abadilishe msimamo, lakini alikataa.

Vasco inatarajiwa kutoa tamko rasmi muda si mrefu na inaelezwa Coutinho anaondoka kwa sababu haoni upendo kutoka kwa mashabiki.

Kutoelewana kati ya Coutinho na baadhi ya mashabiki kumekuwa kukiongezeka hivi karibuni na inasemekana mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil aliumizwa na kuzomewa katika Uwanja wa São Januário wakati wa mechi dhidi ya Bahia wiki iliyopita.

Baada ya mechi hiyo, kocha mkuu Diniz alimwelezea Coutinho kama “mchezaji wa kipekee” na “zawadi” kwa Vasco, huku akikubali pia kuwa mashabiki wana haki ya kumzomea mchezaji yeyote wanayemtaka.

Iwapo Coutinho ataondoka Vasco, itakuwa ni tukio jingine la kusikitisha katika maisha yake ya soka ambayo imekuwa ikididimia kila uchao.

Baada ya kufeli katika viunga vya Nou Camp, Coutinho alitua kwa mkopo na Bayern Munich na Aston Villa na baadae alisaini nayo mkataba wa kudumu mwaka 2022.

Philippe Coutinho akishangilia pamoja na wachezaji wenzake wakati alipokuwa Liverpool. Picha na Mtandao

Katika kipindi cha mkopo cha miezi sita akiwa Villa Park, alifunga mabao matano na kutoa pasi tatu za mabao. Hata hivyo, katika msimu wake kamili wa kwanza alifunga bao moja pekee katika mechi 22, kabla ya kujiunga kwa mkopo na klabu ya Qatar, Al-Duhail msimu wa 2023–24.

Coutinho alisajiliwa na Vasco kwa mkopo mwaka jana, akifunga mabao matano na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi 26 za mashindano yote, huku klabu hiyo ikimaliza nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Brazil.

Msimu huu amefunga mabao saba katika mechi 28, rekodi ambayo inaonekana kuwa nzuri kwake.

Coutinho alikulia katika akademi ya Vasco da Gama kabla ya kuonekana na vigogo wa Serie A Inter Milan mwaka 2008, alionyesha kiwango bora katika viunga vya San Siro kabla ya kutua Liverpool mwaka 2013, ambako alikaa kwa miaka mitano kabla ya kuhamia Barcelona katika mojawapo ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kutokea kwenye soka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *