Rombo. Mwalimu aliyemfundisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba jiografia darasa la nne, katika Shule ya Msingi Mapunda, Adolf Pantaleo ameibukia kwenye mkutano wake na kumkumbusha namna alivyokuwa akijibu maswali vizuri kuhusu Mlima Kilimanjaro.

Mwalimu huyo ni miongoni mwa watu waliokuwa kwenye foleni ya kuuliza maswali au changamoto kwa Waziri Mkuu, hata hivyo  amejitambulisha kama mwalimu wake, akampongeza kwa mafanikio yake ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.

Shangwe ziliibuka katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika leo Februari 19, 2026 baada ya kuweka jiwe la msingi katika eneo la Shule ya Amali ya Mwalimu Steven Memorial, kata ya Marangu Kitowo, baada ya mzee huyo kujitambulisha kama mwalimu wa Dk Mwigulu.

“Nikupongeze kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, vilevile nikupongeze kama mwanafunzi wangu wa Shule ya Msingi Mapunda, nilikuacha ukiwa darasa la nne na ukatimiza ahadi yangu. Nilikuja darasani kukufundisha jiografia, nikakuuliza swali, mlima gani ni mrefu kuliko yote, ukanijibu ni Mlima Kilimanjaro,” amesema mwalimu huyo mstaafu huku wananchi wakimpigia makofi.

Ameongeza kuwa: “Bahati nzuri, mimi nilikuwa nacheza mpira na wewe ulikuwa unacheza, tukaenda uwanjani, nilikuwa upande wa Simba na wewe Yanga. bahati mbaya, tukawafunga, ukaniita kuniambia ‘mwalimu, kweli nyie Simba mmetufunga’, nikakwambia ‘ndio’. Ukaniambia kinachofuata nitakuja Mlima Kilimanjaro niuone.”

“Kweli, umefanya jitihada kubwa na mahali ulipokaa unauona Mlima Kilimanjaro, hongera sana Mheshimiwa,” amesema mwalimu huyo mstaafu.

Amemuombea kwa Mungu asiishie hapo kwenye Mlima Kilimanjaro, bali Mwenyezi Mungu amuangazie, mambo yakiwa safi wataendelea kukutana tena kwa mambo makubwa zaidi,” amesema mwalimu huyo.

Dk Mwigulu amkumbuka

Akizungumza baada ya Mwalimu wake huyo, Dk Mwigulu amesema anamkumbuka mwalimu huyo na hata wimbo ambao alikuwa akiwaimbisha kwenye mchakamchaka, akauimba kwenye mkutano huo.

“Mwalimu usiende mbali, njoo ukae hapa, mleteeni kiti mwalimu wangu. Shikamoo Mwalimu. Mwalimu huyu tulikuwa tunakwenda naye mpaka kwenye mchakamchaka, nakumbuka na kawimbo kake, kaeeni eee kwani eee Tanzania kaeeni woote,” amekumbushia Dk Mwigulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *