
Mwanza. Serikali imesema Sh200 bilioni zilizoahidiwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana tayari zimetolewa na kusambazwa katika wizara za kisekta ili kuwafikia kulingana na shughuli wanazofanya.
Ahadi hiyo ilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wajasiriamali.
Akifungua jukwaa la vijana Mkoa wa Mwanza, leo Alhamisi Februari 19, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amesema fedha hizo zilikabidhiwa katika wizara hiyo kwa ajili ya uratibu na tayari zimepelekwa katika wizara zinazotekeleza miradi ya vijana.
Amesema vijana ni kundi la mtambuka linalopatikana katika sekta mbalimbali, hivyo Serikali imeona ni vema fedha hizo zipelekwe moja kwa moja katika wizara za kisekta ili kila kijana apate kupitia eneo analofanyia kazi.
“Vijana wapo kwenye uvuvi, madini, kilimo, biashara na teknolojia. Ili kuwafikia kwa usawa, fedha hizi zimeelekezwa katika wizara husika badala ya kubaki sehemu moja,” amesema.
Amesema baadhi ya wizara zilizopokea fedha hizo ni Wizara ya Madini kupitia programu ya ‘Mining for a Better Tomorrow’, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mawasiliano, pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amesema fedha hizo zitasimamiwa kwa utaratibu maalumu ili ziweze kuwafikia walengwa na kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali.
Katika uzinduzi huo, Nanauka amekabidhi mkopo nafuu wa Sh200 milioni kwa vikundi viwili vya vijana mkoani Mwanza baada ya kushinda andiko mradi waliloliwasilisha wakati wa kongamano la vijana lililofanyika mkoani humo Desemba, 2025.
Vikundi hivyo vilivyopata Sh100 milioni kila kimoja ni Kitwima Youth Group cha ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kilichopo Luchelele wilayani Nyamagana na kikundi cha waendesha bajaji za mizigo kilichopo wilayani Ilemela.
Katika hatua nyingine, waziri huyo amezielekeza sekretarieti za mikoa na halmashauri zote nchini kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya vijana.
Amesema majukwaa ya vijana yanapaswa kuendelezwa kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya na viongozi wahakikishe wanashirikisha wadau wa maendeleo waliopo katika maeneo yao ili kuimarisha utekelezaji.
Mwenyekiti wa kikundi cha Kitwima Youth Group, Suzana Sayi amesema waliandaa andiko la mradi lililowawezesha kupata fedha hizo akiwataka vijana kushiriki kwenye makongamano kwa ajili ya fursa mbalimbali.
“Tuliandika andiko la mradi, si kwa koneksheni bali tulichangamkia fursa ilvyojitokeza…Vijana jitokezeni fursa zinapotangazwa,” amesema.
Naye Wilbert Malale, ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi cha waendesha bajaji za mizigo amesema umoja na kuwa na vikundi imara kumewasaidia kufikia fursa hiyo.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema mkoa huo una zaidi ya vijana milioni 1.4 wenye umri wa miaka 15 hadi 35.
Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, zaidi ya Sh18.155 bilioni zimetolewa kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi zaidi ya 2,401.
Amesema kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh6 bilioni zimetolewa kwa vijana, wanawake wamepata Sh9.4 bilioni na watu wenye ulemavu Sh2.3 bilioni.
Ameongeza kuwa zaidi ya Sh8.9 bilioni zimetolewa katika sekta ya uvuvi wa vizimba mkoani humo, zikinufaisha vijana wengi kwa kuwapatia zana za kufugia samaki.