
Dar es Salaam. Ufungaji wa kamera za siri katika maeneo ya faragha kama vyumba vya hoteli, nyumbani, ofisini au maeneo ya faragha kama chooni bila ya kutoa taarifa kumetajwa kama sehemu ya kuingilia faragha za watu.
Ingawa wapo wanaodai kamera hizo huwasaidia kugundua wizi, kulinda mali na hata kujua tabia za wanaowazunguka, kukusanya ushahidi, kudhibiti tabia zisizofaa lakini, kuweka kamera bila ridhaa ya wahusika ni kutoheshimu faragha zao.
Kumekuwa na matukio kadhaa kwenye jamii ya watu kulalamikia kudukuliwa faragha zao hali ambayo imekuwa ikiibua mjadala mkali pale mhusika anapobaini.
Miezi michache nyuma kuliibuka mjadala mtandaoni baada ya kusambaza kwa video ikimuonesha, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Revocatus Chipando maarufu Babalevo, akimbaini binti wa kazi akimtesa mtoto wake kupitia kamera ya siri ya chumbani.
Kutokana na kitendo hicho, Babalevo alikuwa na sababu ya kuchukua hatua ya kumfukuza kazi binti huyo, lakini kwa upande mwingine, hoja ziibuka binti naye angeweza kushitaki kwa kosa la kufunga kamera ndani ya chumba bila ridhaa.
Ikumbukwe, chumba cha mtu binafsi ni sehemu ya faragha, hivyo kuweka kamera bila ridhaa inaweza kuchukuliwa kama uvunjaji wa haki za faragha hasa kama kamera hizo zinaonesha matukio ya mtu akiwa faragha.
Pia, makala iliyochapishwa na BBC Februari 7, 2026 ikihusu mhusika (Eric) kugundua video zake za chumbani alizorekodiwa bila yeye kufahamu ambapo katika makala hayo Eric anasema wiki tatu kabla ya tukio hilo, yeye na mpenzi wake walikuwa kwenye mapumziko katika hoteli moja mjini Shenzhen kusini mwa China, bila kujua kwamba walikuwa wanachunguzwa na kurekodiwa ni miongoni mwa matokeo ya kamera za siri zinazoingilia faragha.
Hata hivyo, suala la kufunga kamera lipo kisheria nchini Tanzania na yapo masharti ya maeneo zinakopaswa kufungwa, sio kila mahali, kwa mujibu wa Jimmy Makonde, ambaye ni mwanasheria.
Miongoni mwa masharti hayo, anasema ni kulindwa kwa faragha za watu, kama ilivyoabainishwa katika Ibara ya 16(1) ya Katiba ya Tanzania inayosema, “Kila mtu anastahili heshima ya maisha yake binafsi na faragha yake.”
Masharti ya ufungaji wa kamera hizo hayakuishia kwenye Katiba ya nchi pekee, anasema hata kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kinabainisha hilo.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, ni marufuku kukusanya, kurekodi au kusambaza taarifa za mtu bila ruhusa yake na kinaeleza adhabu yake ni faini hadi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.
Si hivyo tu, Makonde anasema hata Sheria ya Kanuni za Adhabu Kifungu cha 138B, kinazungumzia hilo, kikizuia kufuatilia au kumrekodi mtu akiwa kwenye mazingira ya faragha ni kosa la unyanyasaji wa kingono.
Lakini, ufungaji wa kamera hizo, anasema unahalalishwa na Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2017, inasema ushahidi lazima uwe halali kwa njia ya kisheria.
Hata hivyo, inasema ushahidi wa video iliyorekodiwa kwa uvunjaji wa faragha hupoteza uhalali, inaweza kutupiliwa mbali mahakamani na hata aliyeirekodi akafunguliwa kesi mpya.
Kifungu cha 4(d) cha Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, kinatoa msisitizo wa kuweka utaratibu wa kisheria na kitaasisi wa kulinda taarifa binafsi.
Sambamba na yote hayo, anaeleza kuwa Tanzania imeridhia mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR) ambao kifungu 17, kinasema “hakuna mtu anayepaswa kuingiliwa faragha yake bila sababu”.
Jinsi ya kutambua kamera hizo za siri
Wataalamu wa Teknolojia wanaeleza ni muhimu kujua mbinu za kugundua kamera zilizofichwa kwa ajili ya kulinda faragha binafsi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kinara Technologies, Given Edward anasema, unapoingia sehemu unayohisi kuna kamera kagua kwanza kabla ya kufanya chochote.
“Kama ni hoteli angalia kwenye kona, kwenye pembe za juu kulia. Kama sehemu kuna taa za kusimama au maua angalia pia inasaidia ukiziama taa. Kwa sababu kuna baadhi ya kamera zinatoa mwanga.
“Pia unaweza kuzima taa kisha ukawasha kamera ya simu. Unaimulika katika maeno mbalimbali chumbani kwa sababu kamera ya simu inatabia ya kunasa kamera kama imewashwa sehemu,” amesema Given.
Licha ya Given kufafanua hilo, Mchambuzi wa masuala ya Teknolojia, Emmanuel Benard amesema jamii inapaswa kuwa makini kwani kuna aina nyingine za kamera hazionekani kwa urahisi.
“Sasahivi kuna kamera zipo kama vifungo, miwani. Kwahiyo kama ni CCTV kwenye iPhone kuna sehemu ambayo unaweza kuskani. Lakini niliziona kamera Dubai hizo hata ukiskani hauoni kama ni kamera.
“Kamera ya miwani ipo kawaida sana hauwezi kujua kamera yake ilipo. Lakini kwenye yale maungio ya miwani na sehemu inayoshika sikio pale ndipo kamera inafichwa, hivyo siyo rahisi kujua. Tunatakiwa kuchunguza kila kitu na ndiyo teknolojia ipo huko,” amesema Emmanuel.
“Changamoto ni kwamba kuna aina ya kamera hata uzime taa hauwezi kuona. Tunasema kuzima taa ni kwasababu kuna zile nyingine ukizima zenyewe zinawasha kwa ajili ya kuchukua matukio.
Lakini zipo ambazo hazifanyi hivyo. Binafsi nimebahatika kuiona miwani ya kamera zaidi ya mara moja. Bei ni kuanzia Sh1.5 milioni.
“Wapo baadhi wanavaa kwa lengo zuri, zinakuwa zimeunganishwa na simu hata likitokea lolote watu wajue alikumbwa na nini. Lakini kila mtu ana malengo yake. Tunatakiwa kuwa makini tusiende kila sehemu, tusiwe na kila mtu,” amesema Emmanuel.
Amesema sehemu husika kama hoteli kubwa, kabla ya watu kuingia kuongezwe ukaguzi. Kwasababu kamera hizo hutegemea betri hivyo kupitia skana zenye uwezo mkubwa zinaweza kugundulika.
Licha ya kuwa, baadhi ya kamera hizo huuzwa bei ghali, zipo zinazouzwa hadi Sh30,000 kama anavyosema mfanyabiashara wa kamera Kennedy Desiderius;
“Kamera za siri bei yake inatofautiana zipo kuanzia Sh30,000. Zinaenda hadi Sh1,000,000. Mimi huwa nawaelekeza wateja wangu kamera zitumike maeneo ya wazi. Siyo kuweka chooni, chumbani na maeneo mengine ya faragha. Lakini wapo ambao wananunua kwaajili ya kukusanyia ushahidi,” amesema Kennedy.
Miriam Ibuge, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam amesema jamii ielimishwe zaidi kuhusu matumizi ya vifaa hivyo. Kwani vinapatikana kwa urahisi.
Tatu John amesema teknolojia hii imekuwa sumu kwake, yeye ni mwathirika katika jambo hili, “Nilifungiwa kamera na aliyekuwa mpenzi wangu bila mimi kujua. Kwa bahati mbaya kuna vitu aliona hakupenda. Nilijaribu kumuelewesha hakunielewa mwisho tumeachana.
Naye, Richard Mrema amesema wauzaji wa bidhaa hizo ikiwezekana wawe na vibali maalum kwakuwa upatikanaji wa urahisi unaweza kufanya watu kutumia wanavyotaka.