Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa Akili Mnemba au AI wenye thamani ya dola bilioni 3, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inawanufaisha watu wote duniani, badala ya kuwa mali ya mataifa machache au kampuni chache zenye nguvu.
Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili Athari za AI unaofanyika huko New Delhi nchini India, Katibu Mkuu Guterres amemshukuru Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kwa kuitisha mkutano huo muhimu akisema kuwa “mustakabali wa AI haupaswi kuamuliwa na kundi dogo la nchi au kuachwa mikononi mwa matajiri wachache wa teknolojia, bali unapaswa kujengwa kwa ushirikiano wa kimataifa.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akiwa kwenye mkutano wa athari za AI uliofanyika nchini India.
Hatua Mbili Muhimu za UN
Katibu Mkuu alikumbusha kuwa mwaka 2025 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilichukua hatua mbili muhimu.
Mosi, kuanzishwa kwa Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu AI, ambalo sasa limekamilika kuteuliwa. Jopo hilo lina wataalamu 40 kutoka kanda na taaluma mbalimbali, likiwa na ujumbe mmoja wazi: “AI ni ya kila mtu.”
Alisisitiza umuhimu wa kuondoa hofu na upotoshaji kuhusu AI kwa kuzingatia ushahidi wa pamoja na kuziba pengo la maarifa, akizihimiza nchi wanachama, sekta binafsi na asasi za kiraia kushiriki kikamilifu katika kazi za jopo hilo.
Pili, Umoja wa Mataifa umezindua Majadiliano ya Kimataifa kuhusu Usimamizi wa AI ndani ya mfumo wa UN. Kikao cha kwanza kitafanyika mwezi Julai jijini Geneva, Uswis kikitoa fursa kwa kila nchi kushiriki katika kuweka miongozo ya pamoja ya usalama, kulinda haki za binadamu na kuzuia matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.
World Food Programme Booth katika AI Summit 2024, India
Wito wa Mfuko wa Kimataifa wa AI
Katibu Mkuu alionya kuwa “bila uwekezaji wa makusudi, nchi nyingi zitaachwa nyuma katika zama za AI.”
Ndiyo maana amependekeza kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa AI utakaosaidia kujenga uwezo wa msingi duniani kote, ikiwemo mafunzo ya ujuzi, upatikanaji wa data, gharama nafuu za nguvu za kompyuta na mifumo shirikishi.
Guterres amesema “dola bilioni 3 ni chini ya asilimia moja ya mapato ya mwaka ya kampuni moja kubwa ya teknolojia, ….. ni gharama ndogo kulinganisha na manufaa ya kuhakikisha AI inasambaa kwa usawa duniani.”
Aidha, ameeleza kufurahishwa na mwitikio wa nchi wanachama katika kuunda Mtandao wa Kimataifa wa Kubadilishana Uzoefu na Ushirikiano katika Kujenga Uwezo wa AI.
AI kwa Maendeleo Endelevu
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, “ikiwa itatumika kwa usahihi, AI inaweza kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kusaidia uvumbuzi wa kitabibu, kupanua fursa za elimu, kuimarisha usalama wa chakula, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na majanga, pamoja na kuboresha huduma za umma.”
Hata hivyo, ameonya kuwa “AI inaweza pia kuongeza pengo la usawa, kuendeleza upendeleo na kusababisha madhara iwapo haitasimamiwa vizuri.”
Aligusia pia ongezeko la matumizi ya nishati na maji yanayohusishwa na vituo vya kuhifadhi taarifa kwa njia ya mtandao (data), akisisitiza haja ya kutumia nishati safi na kuepuka kubebesha gharama jamii zilizo hatarini.
Ulinzi na Uwajibikaji
Katibu Mkuu alisisitiza kuwa “AI lazima iheshimu utu wa binadamu, iwe chini ya usimamizi wa kibinadamu, na kuwepo kwa uwajibikaji wa wazi.”
Alionya dhidi ya unyonyaji, udanganyifu na matumizi mabaya ya AI, akisema hakuna mtoto anayepaswa kuwa majaribio ya teknolojia isiyodhibitiwa.
“Matokeo halisi yanamaanisha teknolojia inayoboresha maisha na kulinda sayari,” amehitimisha kwa kutoa wito wa kujenga AI kwa ajili ya wote, huku utu ukiwa msingi wake.