Shinikizo la kisiasa la vyama vikuu vyenye mielekeo ya Kiislamu nchini Pakistan kwa serikali ya nchi hiyo la kuitaka ijiondoe katika kile kiitwacho ‘Bodi ya Amani’ ya Trump limeongezeka.
Kwa mujibu wa Pars Today, Maulana Fazlur Rehman, Amir wa Jamiat Ulema-e-Islam (Tawi la Fazl), na Hafiz Naeem-ur-Rehman, Amir wa Jamaat-e-Islami, ambavyo ni vyama viwili vikuu vya Kiislamu nchini Pakistan, wamefanya kikao cha pamoja cha kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio yanayojiri katika Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa Islamabad katika ‘Bodi ya Amani’ ya Trump.

Viongozi hao wa vyama viwili vikubwa vya siasa nchini Pakistan, wametoa onyo kali kwa serikali kuhusu matokeo hasi ya kushiriki katika kinachoitwa ‘Bodi ya Amani’ ya Trump wakibainisha kwamba, kuundwa kwa bodi hiyo ni hatua ya hila na hadaa inayolenga kulinda maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwakandamiza wananchi madhulumu wa Palestina; na wakasisitiza kuwa hawataruhusu Islamabad igeuzwe wenzo wa kutumika kwa niaba ya madola makubwa.
Aidha, wamekosoa vikali kuhudhuria Pakistan katika bodi hiyo na kutahadharisha kwamba, Wamarekani hawajawahi hata mara moja kuonyesha kuwa wana nia njema, na kwamba lengo lao kuu ni kulinda maslahi ya utawala wa Kizayuni kwa gharama ya kuwakandamiza Wapalestina na kupanua uvamizi na ukaliaji ardhi kwa mabavu unaofanywa na Israel.
Baada ya mkutano wao, Fazlur Rehman na Hafiz Naeem walitangaza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari huko Islamabad: “Tunaionya serikali ya Pakistan isijiingize kwenye mchakato wowote unaosimamiwa na Trump, vinginevyo tutaendelea kutangaza upinzani wetu kwa sura ya mikusanyiko mikubwa na kwa kuitisha maandamano ya nchi nzima.
Huku wakiashiria mkutano wa kwanza wa bodi hiyo ya amani uliofanyika huko Washington na kuhudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Pakistan, viongozi hao wa vyama vyenye mielekeo ya Kiislamu wamesema: “Suali letu sisi ni: je, Pakistan inakusudia kuungana na Israel katika kuwakandamiza Wapalestina?”

Hayo yanajiri katika hali ambayo, vyama vingi maarufu na wawakilishi wengi wa Bunge la Pakistan nao pia wameonyesha kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu malengo ya nyuma ya pazia ya Trump na waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu, na wamepinga Islamabad kutoa mchango wowote katika mchakato huo.
Upinzani wa vyama vikubwa vya siasa vya Pakistan kuhusiana na ushiriki wa nchi hiyo katika bodi ya amani iliyopendekezwa na Donald Trump kwa ajili ya Ghaza, zaidi ya kitu chochote kile, umetokana na mchanganyiko wa wasiwasi wa kimkakati, shinikizo la maoni ya umma, na masuala ya kisiasa ya ndani.
Jambo la kwanza lililochangia kuibuka kwa hali hiyo ni kutokuwa na imani kihistoria sehemu kubwa ya vinara wa kisiasa wa Pakistan na namna Marekani inavyojihusisha na migogoro ya Asia Magharibi. Vyama vingi vya Pakistan vinaamini kuwa, mipango yote inayowasilishwa na Marekani huwa haiwi ya kutopendelea upande wowote, na kivitendo haiwezi kuakisi matakwa ya Wapalestina kwa kiwango ambacho Islamabad inakiona kuwa ni cha haki na uadilifu. Kwa mtazamo huo, kujiunga rasmi kwa Pakistan na mpango uliobuniwa na Trump, yaani bodi ya amani, kunatafsiriwa kuwa ni sawa na kuidhinisha kitu ambacho wakosoaji wengi wanaamini kwamba kitaunufaisha zaidi upande mmoja.
Lakini mbali na hilo, vyama muhimu vya siasa nchini Pakistan kama vile Muslim League-Nawaz na Pakistan People’s Party vinaamini kuwa suala la Ukanda wa Ghaza inapasa lishughulikiwe kupitia mfumo wa taasisi za pande kadhaa na kwa mwafaka wa pamoja wa Ulimwengu wa Kiislamu; si kupitia mipango inayoongozwa na dola moja kubwa maalumu. Vyama hivyo vina wasiwasi kwamba kushiriki Pakistan katika mpango wa Trump kwa ajili ya Ghaza kutadhoofisha msimamo wa jadi wa nchi hiyo katika kuunga mkono haki za Wapalestina na kuibua mpasuko kati ya serikali na maoni ya umma.

Jambo la pili ni kuhusu shinikizo la kijamii na uhasasi mkubwa ilionao jamii ya Pakistan kuhusiana na kadhia ya Palestina. Anga ya kisiasa ya nchi hiyo ni ya namna ambayo, hatua yoyote ya serikali katika uga wa sera za nje huwa inatafsiriwa na kutolewa hukumu na maoni ya umma. Katika hali kama hiyo, kuunga mkono mpango wa Marekani kuhusu Ghaza kunaweza kutafsiriwa na wapinzani wa ndani kuwa ni ukengeukaji wa misingi iliyotangazwa wazi katika sera za nje za Pakistan. Suala hili ni changamoto pia kwa serikali inayoongozwa na Shahbaz Sharif, kwa sababu inalazimika kuweka mlingano wa mizani kati ya ushirikiano wake wa kidiplomasia na madola yenye nguvu duniani na kulinda nafasi na uhalali wake wa kisiasa ndani ya nchi.
Na jambo la tatu linahusiana na ushindani wa kisiasa wa ndani. Vyama vya upinzani huitumia maudhui ya sera za nje kuikosoa serikali. Kwa hiyo msimamo wa kupinga kushiriki Islamabad katika kiitwacho bodi ya amani ya Trump unatafsiriwa kama wenzo wa kudhihirisha uhuru wa kisiasa wa Pakistan na kulinda maslahi ya taifa ya nchi hiyo. Vyama hivyo vinasisitiza kwamba, lazima Pakistan idumishe nafasi yake ya mtetezi wa haki za Wapalestina na kuepuka kujiingiza kwenye mifumo kama kile kiitwacho mpango wa amani wa Trump kuhusu Ghaza na bodi yake ya amani, ambavyo kwa hakika ni nyenzo alizojimilikisha rais huyo wa Marekani na zinaweza kukinzana na sera ya nje ya Pakistan kuhusiana na suala la Palestina na uungaji mkono wake kwa Wapalestina…/