
Rais wa zamani wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol amepatikana na hatia leo Alhamisi, Februari 19, ya kuongoza uasi kwa kuweka sheria ya kijeshi kwa muda mfupi na kupeleka jeshi Bungeni mnamo Desemba 2024. “Kuhusu mshtakiwa Yoon Suk-yeol, kosa la kuongoza uasi limethibitishwa,” Jaji Ji Gwi-yeon wa Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul amesema alipokuwa akisoma hukumu hiyo. Amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Tunamhukumu Yoon kifungo cha maisha jela” kwa kuongoza uasi, Jaji Ji Gwi-yeon wa Mahakama ya Wilaya ya Kati ya Seoul amesema alipokuwa akisoma hukumu hiyo siku ya Alhamisi, Februari 19. Kiongozi huyo wa zamani wa kihafidhina aliepuka adhabu ya kifo, ambayo iliombwa na upande wa mashtaka, ingawa hakuna adhabu yoyote ya kifo iliyotekelezwa nchini Korea Kusini tangu mwaka 1997.
Yoon Suk-yeol ni mkuu wa tano wa nchi ya Korea Kusini aliyehukumiwa na mahakama tangu mwaka 1996, lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba hukumu yake haitatekelezwa kikamilifu, anaripoti mwandishi wetu huko Seoul, Célio Fioretti. Ingawa Korea Kusini haisiti kuwahukumu wakuu wake wa nchi, inajulikana pia kwa kuwasamehe au kupunguza vifungo vyao miaka michache baadaye chini ya msukumo wa serikali mpya.
Licha ya uamuzi wa mahakama, jamii ya Korea Kusini bado imegawanyika sana. Chama cha Conservative, ambacho rais huyo wa zamani anatokea, kinabaki kuwa mwaminifu kwake kwa kiasi kikubwa. Na baadhi tayari wanamtaka arudi kwenye maisha ya kisiasa.
Katika hotuba ya kushtukiza jioni ya Desemba 3, 2024, Yoon Suk-yeol alitangaza sheria ya kijeshi na kuamuru jeshi kuvamia Bunge. Hata hivyo, idadi ya kutosha ya wabunge waliweza kuingia ndani ya chumba hicho, ambacho kilikuwa kimezungukwa na wanajeshi, na kupitisha azimio dhidi ya mapinduzi, na kumlazimisha rais wa wakati huo kurejelea hatua yake.
Serikali ya kiraia hatimaye ilisimamishwa kwa saa sita tu, lakini mapinduzi hayo yalisababisha mgogoro mkubwa na wa muda mrefu wa kisiasa nchini. Yoon Suk-yeol, ambaye alifikishwa mahakamani akiwa kizuizini, alitimuliwa mamlakani mwezi Aprili kwa vitendo hivi.
Mawaziri wa zamani pia wamelihukumiwa
Akiwa na umri wa miaka 65, Yoon Suk-yeol yuko anakabiliwa na kesi zingine kadhaa. Daima amekuwa akikana kosa lolote, akidai kwamba alichukua hatua ya “kuhifadhi uhuru” na kurejesha utaratibu wa kikatiba dhidi ya kile alichokiita “udikteta wa kisheria” wa upinzani, ambao ulitawala Bunge na kuzuia mapendekezo yake.
Alikuwa tayari amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa makosa madogo yanayohusiana na mapinduzi yake. Washirika wa zamani, ambao walikuwa wakihudumu wakati wa uamuzi wake wa kushangaza, pia wamepokea vifungo jela au wanasubiri kesi.
Akipatikana na hatia na mahakama, Waziri wa zamani wa Ulinzi Kim Yong-hyun alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Mwishoni mwa mwezi Januari, Waziri Mkuu wa zamani Han Duck-soo alipokea kifungo cha miaka 23 (ikilinganishwa na kifungo cha miaka 15 kilichoombwa na upande wa mashtaka), na Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Lee Sang-min, alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela wiki iliyopita kwa majukumu yao katika kashfa hiyo.