Wakati tuhuma za Epstein zikiwa zimezagaa, Wexner hakutaka kusikia lolote, na hakuchukua uamuzi wowote kujitenga na mhalifu huyo wa ngono kwa mabinti wadogo.

Mbali na kuwa msimamizi wa mali za bilionea Wexner, Epstein alikuwa ndiye mshauri mkuu wa masuala ya kifedha wa tajiri huyo, vilevile mdhamini wa Taasisi ya Wexner. Nafasi hizo zilikuwa nyeti, na zilipaswa kumshitua Wexner kipindi Epstein alipokuwa anaandamwa na kashfa mfululizo.

Agosti 2019, Epstein akiwa ameshikiliwa mahabusu na kabla mhalifu huyo wa ngono kwa mabinti wadogo hajafariki dunia, Taasisi ya Wexner, ilitoa taarifa ya maandishi kuwa Epstein alitumia vibaya nafasi alizoaminiwa na Wexner, hivyo kuchota fedha nyingi bila idhini. Taarifa hiyo ilieleza kwamba Epstein alichota fedha hizo kutoka kwenye akaunti ya Wexner, na ya familia ya Wexner.

Kesi ya Wexner inafanana mno na ya bilionea wa Wall Street, Leon Black. Kwa muda mrefu, Epstein alikuwa akipokea mamilioni ya dola kutoka kwa Black. Kuanza kutolewa kwa Mafaili ya Epstein mwaka 2019, ulikuwa mwanzo wa kugundulika kwa uhusiano baina ya Black na Epstein.

Oktoba 18, 2025, gazeti la New York Times, lilikuwa mbele ya muda, liliporipoti barua pepe ambazo zilinaswa kwenye Mafaili ya Epstein. Barua pepe hizo zilionyesha jinsi Epstein alivyokuwa akimtisha Black kumpa fedha. Ilibainika kuwa Black alikuwa akimlipa Epstein, makumi mamilioni ya dola kila mwaka. Ulipofika mwaka 2026, Black alisita kuendelea kulipa.

Katika barua pepe hizo, Epstein alimwambia Black kwamba alikuwa akicheza na moto wenye hatari. Kwa mujibu wa New York Times, vitisho hivyo vilikuwa na majibu, kwani Black alilegea na kuendelea kumlipa. Mpaka wakati wanapitia taarifa, tayari Black alikuwa ameshamlipa Epstein dola 150 milioni (Sh390 bilioni).

Kwa mujibu wa Mafaili ya Epstein, taarifa iliyopatikana ndani ya kurasa milioni tatu, zilizoachiwa Januari 30, 2026 na Wizara ya Haki Marekani (DOJ), kati ya mwaka 2012 na 2017, Black alimlipa Epstein dola 158 milioni (Sh410.8 bilioni). Hii maana yake ni kuwa baada ya barua pepe za vitisho kutoka kwa Epstein, Black alinywea na kumlipa dola 8 milioni zaidi (Sh20.8 bilioni).

Nadharia ni ileile kuwa Epstein alimwingiza Black kwenye mtego, akashililia siri zake, kwa hiyo akawa anamwendesha atakavyo. Mwaka hadi mwaka, Epstein alitengeneza makumi mamilioni ya dola, moja kwa moja kutoka kwa Black. Dhahiri, Epstein aliwafanya matajiri kuwa mateka wake kwa kumiliki siri zao zenye kushikilia aibu kubwa kwao kijamii.

Utetezi wa Black ni kuwa uhusiano wake na Epstein ulikuwa mbali. Na kipindi chote alichomfanya Epstein kuwa mshauri wake wa kifedha, aliweza kuokoa dola 1.3 bilioni (Sh3.4 trilioni). Alikuwa anajaribu kuhalalisha malipo ya dola 158 bilioni alizotoa. Zaidi, fedha hizo (dola 158bilioni), ni kwa miaka mitano tu. Uhusiano baina yao ulifika miongo minne. Je, ni kiasi gani cha dola  Epstein alivuna kutoka kwa Black?

Machi 2021, mwanamke anayeitwa Guzel Ganieva, alianzisha mashambulizi dhidi ya Black kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akidai alibakwa mfululizo na bilionea huyo. Black alijitetea kuwa alishiriki mapenzi na Guzel kwa makubaliano, na kwa hiyari kabisa. Guzel aliongeza malalamiko kwamba Black alimlazimisha pia kufanya ngono na Epstein.

Tuhuma hizo za Guzel kuwa alishawishiwa na Black kujamiiana na Epstein ni simulizi ya kipekee ndani ya Mafaili ya Epstein. Maana, ushuhuda wa waathirika wengi na ushahidi uliokusanywa, kila hatua, Epstein ndiye anatajwa kuwatafutia washirika wake warembo (mabinti wadogo), na kuwapa nafasi ya kustarehe nao kwenye makasri yake, kisha kuwarekodi na kutunza ushahidi.

Katika Mafaili ya Epstein, inaonyesha kuwa kesi ya Guzel dhidi ya Black, ilimalizwa na Epstein kimafia. Epstein alimshawishi Guzel kukutana na Black kwa ajili ya mazungumzo. Walipokutana, Guzel alirekodiwa bila kujua. Kila alichokizungumza kwenye mkutano huo kilirekodiwa. Kisha, Guzel alionywa endapo angetoa tuhuma nyingine, angekwenda na maji. Ni mpaka Machi 2021, Epstein akiwa ameshafariki dunia, ndipo Guzel aliibukia X kuwashambulia Black na Epstein.

Mwanamke mwingine, Cheri Pierson, alifungua mashitaka dhidi ya Black mwaka 2022, akilalamika kubakwa na bilionea huyo kwenye kasri la Epstein, lililopo New York. Angalau, malalamiko ya Cheri yalifanana na waathirika wengine, waliodai kwamba waliingizwa kwenye makasri tofauti ya Epstein, na kushurutishwa kuwafanyia masaji wateja wa mhalifu huyo, halafu hatima yake ilikuwa kutendewa ukatili wa kingono.

Julai 25, 2022, Black alifunguliwa mashitaka ya kumbaka mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miaka 16. Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, tukio hilo lilitokea mwaka 2002, kwenye kasri la Epstein, lililopo Manhattan, New York. Ilielezwa kuwa binti huyo alikuwa na changamoto ya utindio wa ubongo, na udumavu.

Kwa tuhuma hizo, na ushahidi kuwa alimlipa Epstein fedha, makumi mamilioni ya dola, Black alilazimika kujiuzulu uongozi wa taasisi zake, Apollo Global Management na Museum of Modern Arts. Kabla ya kujiuzulu, aliitaka Bodi ya Apollo na akaipa mkataba kampuni huru ya kisheria, Dechert LLP, kufanya mapitio ya uhusiano baina yake (Black) na Epstein.

Majibu yalipotolewa na Dechert LLP, yalionyesha kuwa ni kweli Black alimlipa Epstein makumi mamilioni ya dola. Hata hivyo, kupitia mikakati ya kifedha na kodi ya Epstein, ambayo Black aliitumia, aliweza kuokoa mabilioni ya dola. Mantiki hapo ni kuwa Epstein alikuwa na maarifa mengi kwenye eneo la fedha na kodi. Na alimsaidia Black. Shida ni ushirikiano wao wa uhalifu wa kingono, tena kwa mabinti wadogo.

Mambo yalipogeuka rangi kuwa meusi, kila aliyeshirikiana na Epstein, si tu alimkana, bali pia alitoa taarifa hadharani ya kujutia uhusiano huo. Kama Wexner. Ndivyo hivyohivyo kwa Black, naye hatimaye alitamka majuto yake ya kujenga uhusiano na ushirikiano na Epstein. Mwaka 2023, Black alilipa fedha dola 62.5 milioni (Sh162.5 bilioni) kwa Visiwa vya Virgin, kushughulikia malalamiko yaliyohusiana na Epstein.

Julai 2023, Kamati ya Fedha ya Seneti, ilitangaza kuanza uchunguzi kubaini mikakati ya Epstein ya ukwepaji kodi, vilevile Black akivyohusika kibiashara na Epstein. Julai 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Seneti, Seneta Ron Wyden, alitoa maagizo kwa wakala wa Huduma ya Mapato ya Ndani (IRS), kuchunguza mikakati ya Epstein, ya ukwepaji kodi. Wyden aliishutumu IRS kwa kushindwa kufanya ukaguzi kwenye miamala ya Epstein kati ya mwaka 2012 na 2017.

Wyden aliitaka Wizara ya Haki Marekani (DOJ), itoe notisi ya kuomba rekodi zote zinazohusiana na Epstein, kwenye taasisi za kifedha, kuanzia Benki ya Marekani, benki ya JPMorgan Chase na Benki ya Deutsche AG. Ni baada ya kuthibitika kuwa Epstein alizitumia zaidi benki hizo ndani ya Marekani kupitisha miamala yake, na kuhifadhi pia pesa zake.

Januari 23, 2026, mshirika wa Epstein, Les Wexner, wakili wa Epstein, Darren Indyke, na mhasibu wa Epstein, Richard Kahn, walipewa notisi ya kimamlaka (subpoenas), kwenda kutoa ushahidi mbele ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Usimamizi wa Serikali, kuhusu wanachokifahamu kuhusu Epstein. Mafaili ya Epstein yaliwataja kama watu waliokuwa karibu na mhalifu huyo wa ngono kwa mabinti wadogo.

Mwakilishi Robert Garcia wa California (Democrat), alitoa ahadi kwa umma kwamba hawatanyamaza wala kusitisha ufuatiliaji mpaka majibu yapatikane, na wote waliomo kwenye Mafaili ya Epstein, haki itendeke dhidi yao.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *