
Msemaji wa maneva ya kijeshi ya Iran na Russia, Admirali Hassan Maghsoudlou, amesema kuwa vikosi vya majini vya Iran na Russia leo Alkhamisi vitafanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.
Admirali Hassan Maghsoudlou ameeleza kwamba, manuva hayo ya kijeshi yatafanyika katika Bahari ya Oman na Bahari ya Hindi kaskazini, kwa lengo la kuimarisha usalama wa baharini na maingiliano endelevu ili kuhakikisha usalama katika maeneo haya nyeti.
Msemaji wa mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya majini ya Iran na Russia ameongeza kusema kuwa: “Mazoezi haya yatafanyika Bandar Abbas (kusini mwa Iran), na lengo lake kuu ni kuimarisha usalama na ushirikiano endelevu wa baharini katika Bahari ya Oman na kaskazini mwa Bahari ya Hindi.”
Ameongeza: “Lengo lingine la mazoezi hayo ni kukuza ushirikiano wa majini na kuimarisha uhusiano kati ya majeshi ya majini ya nchi mbili katika kubuni na kutekeleza shughuli za pamoja.”
Amebainisha kwamba “kufikia muunganiko na uratibu katika taratibu za pamoja ili kukabiliana na shughuli zinazohatarisha usalama na uthabiti wa baharini, hasa katika uwanja wa kulinda meli za kibiashara na meli za mafuta, pamoja na kupambana na ugaidi wa baharini, ni mojawapo ya nguzo kuu za mazoezi haya ya pamoja ya kijeshi.”
Admirali Maghsoudlou amesisitiza kwamba manuva haya ya kijeshi ya pamoja ya majini yanalenga kuimarisha uhusiano wa kirafiki, kuongeza ushirikiano wa kikanda huku kipaumbele kikipewa nchi jirani, na kuimarisha jukumu la nchi za eneo hilo katika kutoa na kuanzisha usalama wa baharini na ubaharia.