WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar kuwa mstari wa mbele kulinda, kuuenzi na kuutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa Taifa.

Ameyazungumza hayo wakati akifungua Kongamano kuhusu Muungano kwa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Zanzibar lililofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) leo Februari 19, 2026.

Masauni amesema vijana ni nguvu kazi na ni tumaini la taifa, hivyo wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha urithi wa amani na upendo ulioasisiwa na waasisi wa Taifa unaendelea kudumu.

Amesema kongamano hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa Aprili 23, 2024 wakati wa uzinduzi wa kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali ya jamii, hususan vijana.

“Idadi kubwa ya Watanzania ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano, hivyo ni muhimu wapate uelewa mpana kuhusu historia, misingi na manufaa yake ili wawe mabalozi wazuri wa kuulinda,” amesema Masauni.

Masauni amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na waasisi wa Taifa letu Julius Nyerere na Abed Amani Karume, umeendelea kudumu kwa zaidi ya miaka 61, ukiwa nguzo ya amani na utulivu nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame amesema kongamano hilo limewezesha kupata maarifa na uelewa zaidi kuhusu upekee wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Amesema kongamano hilo litasaidia kuongeza uelewa kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuasisiwa kwa Muungano, changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake, pamoja na malengo na dira ya kuudumisha na kuuenzi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Naye, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Zanzibar (SUZA), Juma Omar Nkwede amesema kongamano hilo limekuja wakati sahihi kwao kwa kuwapa elimu ya historia kuhusu taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *