Dar es Salaam. Katika kipindi cha siku mbili jumla ya mashauri 40 yanayohusu migogoro ya ndoa yamepokelewa katika Kliniki ya Sheria inayofanyika Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam, inayoratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Taarifa kutoka kwa mawakili waliopo katika kliniki hiyo ambayo imeanza Februari 16, 2026 na itamalizika Februari 22, 2026 zinaeleza  wengi wa wanaofika kuomba msaada ni kuhusu mgawanyo wa mali, matunzo ya watoto, unyanyasaji wa kijinsia pamoja na migogoro ya mirathi.

Akizungumza na Mwananchi Februari 19, 2026 Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Silindo Gumada amesema katika hayo mashauri 40 yaliyopokelewa mengi yanahusu mgawanyo wa mali baada ya wanandoa kutengana.

Amesema baadhi ya walalamikaji wamedai kutotambuliwa kwa mchango wao katika mali zilizopatikana wakati wa ndoa, hasa kwa wale waliokuwa wakijihusisha zaidi na kazi za nyumbani na malezi ya watoto.

“Wengi wanakuja wakitaka kujua haki zao kisheria baada ya ndoa kuvunjika,” amesema Gumada.

Pia, amesema kesi za matunzo ya watoto zimechukua nafasi kubwa baadhi ya wazazi wamelalamikiwa kwa kushindwa kutoa matunzo stahiki baada ya kutengana, hali inayowaathiri watoto moja kwa moja.

Amesema sheria za ndoa nchini zinatambuliwa kupitia Law of Marriage Act 1971, ambayo inaweka misingi ya haki na wajibu wa wanandoa pamoja na malezi ya watoto.

Mashauri mengine amesema yamehusisha malalamiko ya unyanyasaji wa kijinsia na kimwili, yakiwemo vipigo, matusi na udhibiti wa kupita kiasi.

“Malalamiko haya yamejitokeza katika kliniki baadhi ya waathirika wamefikia hatua ya kutafuta msaada wa kisheria baada ya kushindwa kuvumilia hali hiyo kwa muda mrefu,” amesema.

Mirathi ya wanandoa yazua migogoro

Aidha, migogoro ya mirathi imeendelea kuibuka, hasa baada ya kifo cha mmoja wa wanandoa. Baadhi ya wajane na wagane wameripoti kunyimwa haki ya mali na ndugu wa marehemu.

Gumada amesema hii kwa kiasi kikubwa inachangiwa na kutokuwepo kwa uwazi au uandikishwaji wa majina ya pamoja katika mali ikiwemo nyumba na magari jambo linaloongeza mzozo mmoja wa wanandoa akifariki.

“Muhimu kwa wanandoa kuzingatia mawasiliano ya wazi, kutafuta ushauri mapema wanapokumbana na changamoto na kujifunza misingi ya kisheria kabla na baada ya kufunga ndoa na kuwa na utaratibu wa kuandika majina ya pamoja kwenye mali zao,”amesema.

Amesema kabla yakufanyika jambo lolote kuna haja ya wanandoa kujua sheria zote ikiwemo za kidini (Kiislam na Kristo), Kiserikali na kimila ili kutoruhusu changamoto mmoja wapo anapofariki.

Mmoja ya mlalamikaji wa mgawanyo wa mali ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema amejikuta katika wakati mgumu wa matumizi ya mali alizochuma na mumewe kwa sababu hakuna jina lake kwenye nyaraka.

“Nimetengana na mume wangu miaka mitatu iliyopita na kwenye nyumba nimefuatilia anaishi na mwanamke mwingine wakati tulijenga na mume wangu  tukiwa kwenye ndoa,”amesema.

Amesema amefika eneo hilo kwa ajili ya kupata msaada ili apate jasho lake la ujenzi wa nyumba badala ya kutumiwa na mtu ambaye hakuwa na mchango wowote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *