Wakati wa ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria, moja ya sura nyeusi na ya uhalifu mkubwa zaidi ilikuwa majaribio ya nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo na kwa watu wake.
Majaribio ya nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria, yaliyofanywa jangwani kuanzia 1960 hadi 1966, yalifikia kiwango cha mauaji ya halaiki ya kutumia mionzi. Maelfu ya watu wasio na ulinzi katika jangwa la Algeria waliaga dunia kutokana na majaribio hayo, na wengi zaidi waliathiriwa na mionzi hiyo, ambayo athari zake mbaya zinaendelea hadi hii leo. Maafa hayo yamerekodiwa kama mojawapo ya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu katika historia.
Ufaransa, ikiwa imedhoofika kisiasa na kijeshi baada ya Vita vya Pili vya Dunia, iliazimia kukarabati nafasi yake kama taifa kubwa duniani; na kupata silaha za nyuklia lilikuwa suala muhimu kwa mchakato huo.
Hata hivyo, ilikuwa karibu muhali kufanya majaribio kama hayo katika ardhi ya Ufaransa kutokana na hatari zake na unyeti wa maoni ya umma. Kwa upande mwingine, Ufaransa haikuiona Algeria kama koloni lake tu, bali pia kama sehemu ya ardhi yake; na kutokana na mtazamo wa ubaguzi wa rangi wa Wafaransa, idadi ya wakazi asilia wa Algeria ilitambuliwa kuwa ndogo kuliko inavyopaswa kuwa. Kwa hivyo, Algeria ilizingatiwa kuwa mahali pazuri pa kufanyia majaribio ya nyuklia. Jenerali Charles de Gaulle, Rais wa Ufaransa wa wakati huo, alichagua jangwa la Algeria kama “nchi isiyo na watu”, bila kuzingatia hatima ya maelfu ya watu waliokuwa wakiishi maeneo hayo.
Majaribio ya nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria yalifanywa katika awamu mbili kuu. Awamu ya kwanza ilihusisha majaribio manne ya angahewa (ya angani) kati ya 1960 na 1961 katika jangwa la Reggane katika jimbo la Adrar kusini mwa nchi hiyo. Jaribio la kwanza la silaha ya nyuklia lililopewa jina la msimbo “Blue Jerboa” lilifanyika mnamo Februari 13, 1960. Bomu hilo la plutonium lilikuwa na nguvu kwa uchache mara tatu zaidi ya bomu la atomiki lililodondoshwa na Marekani huko Nagasaki nchini Japan na kuibua wingu kubwa angani. Dakika 45 tu baada ya mlipuko huo, Charles de Gaulle alitangaza kwa fahari: “Idumu Milele Ufaransa!” Kwa utaratibu huo, Ufaransa ilitangaza kwa fahari kwamba imekuwa taifa lenye nguvu za nyuklia duniani, huku wenyeji wengi wa Algeria, wanajeshi na hata baadhi ya maafisa wa Ufaransa waliohudhuria tukio hilo wakiwa wamechafuliwa na mionzi ya majaribio ya silaha hizo na wengine wakiwa katika hali ya kukata roho.
Baada ya jaribio hilo, Ufaransa ilifanya jumla ya majaribio mengine 17 ya nyuklia nchini Algeria, ambapo 4 yalikuwa majaribio ya angani na 13 yalikuwa majaribio ya chini ya ardhi. Muda mfupi baada ya jaribio la kwanza, majaribio mengine yalifanywa katika jangwa la Algeria, kiasi kwamba eneo kubwa lilichafuliwa na mionzo yenye mada za nyuklia, na mawingu yenye sumu yalienea hadi katika nchi kama vile Senegal, Ivory Coast, Burkina Faso na hata Sudan.
Baada ya jamii ya kimataifa kukosoa uchafuzi uliotokana na majaribio ya silaha za nyuklia angani nchini Algeria, Ufaransa ilihamisha majaribio yake hadi eneo la “In Eker” katika Milima ya Hoggar na kufanya majaribio 13 ya chini ya ardhi kuanzia 1961 hadi 1966. Majaribio ya Ufaransa katika eneo la “In Eker” katika mkoa wa Tamanrasset, yalisababisha mlipuko wa chini ya ardhi wenye nguvu ya tani 150,000 za TNT, ambao ulivujisha gesi zenye mionzi zilizosababisha uharibifu kamili wa mfumo ikolojia. Majaribio haya yalipewa jina la msimbo “Vito vya Thamani”. Wakati wa jaribio la BĂ©ryl mnamo Mei 1, 1962, chumba cha chini ya ardhi hakikuwa kimefungwa vizuri na mada za radioactive zililipuka na kuchafua angahewa. Katika tukio hilo, wenyeji wa Algeria, wanajeshi na maafisa wa ngazi za juu wa Ufaransa walioalikwa kutazama jaribio hilo waliathiriwa vikali na mionzi.
Mojawapo ya vielelezo vya kutisha zaidi vya majaribio ya silaha za nyuklia za Ufaransa nchini Algeria ilikuwa kutumia wanadamu kama “mapanya wa maabara.” Wanajeshi wengi, wafanyakazi wa Algeria, na wafungwa wa kisiasa walitumika kama “mapanya wa maabara” katika majaribio hayo. Pia, watu waliokuwa wakiishi karibu na maeneo ya majaribio walikuwa katika hatari ya moja kwa moja. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 30,000 walikuwa wakiishi karibu na maeneo hayo, wakiwemo wahamaji wa Tuareg, wakulima na wanavijiji. Bila kujua hatari hiyo, raia hao walipata magonjwa na ulemavu kudumu, wao na wapendwa wao, watoto na wanyama wao. Ripoti zinaonyesha kuwa, wingu la mionzi ya nyuklia lililosababishwa na jaribio moja tu la mwaka wa 1962 liliwaathiri Waalgeria wasiopungua 30,000.
Majaribio ya nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria hayakusababisha vifo vya watu vya papo na hapo tu, bali pia yalikuwa na athari mbaya za muda mrefu kwa mazingira na afya ya watu ambazo zinaendelea hadi leo, huku watafiti wakisisitiza uwepo wa athari za uharibifu wa kijenetiki za mionzi hiyo hadi kwa vizazi vilivyofuata.

Uhalifu mwingine wa Ufaransa nchini Algeriia ni taka za nyuklia. Baada ya majaribio kukamilika, Ufaransa ilizika taka hizo kwenye mchanga wa jangwa la nchi hiyo na inaendelea kukataa kuipa serikali ya Algeria ramani ya kamili ya mahali taka hii hatari zilipozikwa.
Wanaharakati wengi wa kutetea haki za binadamu wanatambua vitendo hivyo vya Ufaransa katika ardhi ya Algeria kuwa ni kielelezo cha wazi cha “ukoloni wa nyuklia” na “uhalifu wa kivita” na wanaitaka Paris iombe msamaha rasmi, kuweka wazi kikamilifu kumbukumbu za matukio hayo na kusafisha maeneo yaliyochafuliwa na mionzi ya nyuklia ya majaribio ya silaha ya Ufaransa.
Majaribio ya nyuklia ya Ufaransa nchini Algeria si tu kwamba ni uhalifu wa kinyuklia, bali pia ni mfano halisi wa ukoloni wa nyuklia na mauaji ya kimbari ya kimya kimya ambayo yatabaki kuwa doa jeusi kwenye historia ya binadamu.