Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Saudi Arabia wamefanya mazungumzo na kujadili uhusiano wa pande mbili na mchakato wa mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amefanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud na kujadili uhusiano wa pande mbili na matukio ya hivi karibuni katika mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Wakati wa mazungumzo ya simu, Araghchi alizungumzia kuhusu matukio ya hivi karibuni yanayohusiana na mazungumzo ya Iran na Marekani, akielezea misimamo ya Tehran na mchakato unaoendelea wa kidiplomasia.

Kwa upande wake, Faisal bin Farhan alimshukuru waziri wa mambo ya nje wa Iran kwa maelezo yaliyotolewa na kuelezea matumaini kwamba, mazungumzo yanayoendelea mchakato wake utaendelea hadi matokeo chanya yatakapopatikana.

Iran na Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni zimeelekea kurejesha na kupanua ushiriki wa kidiplomasia, zikisisitiza mazungumzo na ushirikiano wa kikanda.

Umuhimu wa ushirikiano kati ya Iran na Saudi Arabia katika matukio ya kieneo ni muhimu sana, kwa sababu nchi hizi mbili zina nafasi muhimu katika masuala ya kijiografia, kisiasa, kidini, kiuchumi na kiusalama ya eneo hili.

Saudi Arabia inatekeleza Dira ya 2030 ili kubadilisha uchumi wake, huku Iran ikitafuta kuvutia uwekezaji wa kigeni na kupanua biashara ya kikanda. Ushirikiano katika nyanja za nishati, usafirishaji, utalii wa kidini (Hija na Ziyara), na miradi ya miundombinu inaweza kuwa na faida kwa nchi hizo mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *