Dar es Salaam. Katika hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa mitaji kwenye sekta ya elimu na biashara ndogo na za kati (SMEs), Benki ya Mwalimu Commercial Bank (MCB) imefanikiwa kupata mkopo binafsi wa Sh9 bilioni kutoka kwa mwekezaji wa kijamii mwenye makao yake Uholanzi, Oikocredit.

Mkopo huo wa muda wa kati hadi mrefu unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa benki hiyo kupanua wigo wa vyanzo vya mtaji, zaidi ya utegemezi wa amana za wateja, huku ukitarajiwa pia kuchochea mpango wake wa upanuzi wa huduma.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa MCB, James Joseph, amesema benki hiyo imekamilisha rasmi upatikanaji wa mkopo huo, uliowezeshwa na washauri wa miamala, Africapital na Noblestride Capital ya Kenya.

“Tuko hapa kuthibitisha kuwa tumepata mkopo huu wa muda wa kati hadi mrefu kutoka Oikocredit,” amesema Joseph. “Huu si mwisho, bali ni mwanzo wa mtiririko zaidi wa mitaji unaoendana na dhamira yetu.”

MCB, yenye leseni ya kutoa huduma za kibenki nchi nzima, imejijengea taswira kama benki maalumu inayolenga mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya elimu, kuanzia wazazi, walimu na shule hadi wasambazaji na SMEs zinazohusiana na sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Joseph, fedha hizo zitatumika kutoa mikopo kwa wadau wa elimu, ikiwamo kufadhili upanuzi wa miundombinu ya shule binafsi, kutoa mtaji wa uendeshaji kwa wasambazaji wa vifaa vya elimu pamoja na mikopo mahsusi kwa walimu.

“Mnyororo mzima wa elimu unahitaji ufadhili. Sisi tupo kuunga mkono dhamira hiyo,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Africapital, Burak Buyuksarac, amesema huu ni mwanzo wa awamu kadhaa za mitaji zitakazoingia MCB katika kipindi kijacho.

“Hii ni awamu ya kwanza kati ya nyingine zijazo. Kuna mengi zaidi yanakuja,” amesema, akibainisha kuwa imani ya wawekezaji kwa benki hiyo imeongezeka kwa kasi katika miezi ya karibuni.

Ametolea mfano kupanda kwa bei ya hisa za MCB kutoka takribani Sh300 wakati mazungumzo ya ufadhili yakianza hadi kufikia Sh1,050 wiki hii, ishara ya kuimarika kwa matarajio ya soko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Noblestride Capital, Evans Wesonga, alisema uamuzi wa Oikocredit kuwekeza MCB unaashiria imani ya kimataifa kwa sekta za benki na elimu nchini.

“Uwekezaji huu unatoka kwa moja ya vyama vikubwa vya ushirika barani Ulaya, ambacho kimefadhili benki kadhaa katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara,” amesema.

Ameongeza kuwa kabla ya kuwekeza, taasisi hiyo ilifanya tathmini ya kina ya shughuli na mwenendo wa benki hiyo, hatua inayodhihirisha uaminifu wake katika soko.

Katika taarifa yake, Ofisa Uwekezaji wa Oikocredit, Lewis Nyaga, amesema vipaumbele vya ufadhili vya MCB vinaendana na dhamira ya taasisi hiyo ya kusaidia maendeleo ya kijamii kupitia taasisi za kifedha zenye uwajibikaji.

“Ushirikiano huu unaweka msingi imara wa kurejea kimkakati katika soko la Tanzania, na kuimarisha nafasi ya Oikocredit kama mshirika wa muda mrefu anayelenga kupanua fursa za kifedha kwa jamii zisizofikiwa kwa urahisi,” amesema Nyaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *