
Dar es Salaam. Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), linatarajiwa kuketi kesho Ijumaa, Februari 20, 2026 kupitisha hoja mbalimbali ikiwamo kutoa tiketi kwa majina ya wanachama waliokidhi vigezo vya kushiriki kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za juu ndani ya chama hicho.
Ingawa ratiba ya mkutano wa dharura haijawekwa wazi, taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza unatarajiwa kufanyika Jumamosi hii.
Nafasi zitakazowaniwa ni uenyekiti wa Taifa, Makamu wenyeviti wa bara na Zanzibar.
Hatua hizo zinachukuliwa katika kipindi ambacho chama hicho kimetumbukia katika mgogoro wa uongozi uliosababisha wanachama kugawanyika katika makundi mawili, kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa Februari 13, 2026 wa kutengua uchaguzi uliowaweka madarakani viongozi wa sasa, akiwamo Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake watano.
Wengine walioguswa na uamuzi huo katika uchaguzi uliofanyika Desemba 2024 ni makamu wenyeviti Mbarouk Seif Salim (Zanzibar) na Othman Dunga (Tanzania Bara), Katibu Mkuu Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu Magdalena Sakaya (Tanzania Bara), pamoja na Ali Juma Khamis (Zanzibar).
Sababu ya kutengua uchaguzi huo ni kwamba washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama inayomtaka mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali. Hivyo, mchakato huo ulipaswa kurudiwa.
Uamuzi huo umewagawa wanachama katika pande mbili. Upande unaoongozwa na Profesa Lipumba umetangaza kupeleka suala hilo mahakamani kutafuta haki, ukidai kuwa uamuzi wa Msajili haukuzingatia haki za msingi, ikiwamo haki ya kusikilizwa.
Kwa upande mwingine, wakiwamo waliowasilisha malalamiko dhidi ya uchaguzi wa Desemba 2024, wanaunga mkono uamuzi wa Msajili na wameamua kushiriki katika uchaguzi mpya kwa lengo la kuunda safu mpya ya uongozi.
Hata hivyo, baraza hilo linafanyika bila kutanguliwa na kikao cha kamati kuu inayoongozwa na katibu mkuu wa chama.
Kwa mujibu wa katiba ya chama, kamati kuu ina jukumu la kuandaa hoja na kuitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi.
Awali, baraza hilo lilipaswa kuketi jana Jumatano, Februari 18, 2026, lakini kilishindikana baada ya kushindwa kufikisha akidi ya wajumbe.
Kwa mujibu wa katiba ya chama, baraza kuu lina wajumbe 43 na ili mkutano uwe halali na uamuzi wake utambulike, angalau wajumbe 25 wanapaswa kushiriki.
Jana Jumatano, walifanikiwa kupata wajumbe 17 pekee, hivyo kuanza juhudi za kuwatafuta waliobaki ili kufikisha akidi na kuwezesha kufanyika kwa mkutano huo kesho.
Akizungumza na Mwananchi, leo Alhamisi Februari 19, 2026 kiongozi wa upande unaotarajia kushiriki katika uchaguzi huo, Abdullah Dadi Ubwa, amesema maandalizi ya kikao hicho yamekamilika, ingawa wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka upande unaopinga mchakato huo.
“Kesho tunakutana katika ofisi za chama, Ukumbi wa Shaban Mloo, kwa kikao cha Baraza Kuu ili kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa kufanya uchaguzi wa viongozi wapya kama alivyoelekeza Msajili wa Vyama vya Siasa,” amesema Ubwa.
Amesema tayari wametoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kikao hicho na wamepata mwongozo unaohitajika. Lengo ni kupitisha majina ya watakaopigiwa kura katika uchaguzi.
“Tumewataarifu wajumbe wote wa Baraza Kuu. Tatizo lililopo kuna kundi linalosambaza taarifa za kupinga kikao hicho kwa madai kuwa si rasmi kwa sababu hakijaitishwa na viongozi wa chama,” amesema.
Ubwa amesema, kwa mujibu wa hali ilivyo sasa, chombo chenye mamlaka ni Baraza Kuu, kwa kuwa uamuzi wa Msajili umefuta matokeo ya uchaguzi uliowaweka madarakani viongozi waliokuwapo.
“Wapo wanaodhani bado kuna Naibu Katibu Mkuu ofisini na wajumbe wa kamati tendaji wenye mamlaka ya kuitisha kikao, lakini kwa mujibu wa katiba yetu, hawana mamlaka hayo katika mazingira ya sasa,” amesema.
Amesema wajumbe wa baraza kuu wanapaswa kukutana wenyewe kujadili hali iliyojitokeza, hasa baada ya kupokea barua kutoka kwa wajumbe wenye mamlaka ya kuomba kuitishwa kwa mkutano wa dharura.
“Huwezi kupinga uamuzi wa mamlaka yako ya juu. Tumekubali kutekeleza agizo hilo, ndiyo maana tunaketi kesho kuandaa mkutano wa dharura,” amesema.
Alipoulizwa kama haoni uwezekano wa kutokea vurugu kutokana na mvutano uliopo, Ubwa amesema kikao hicho kitafanyika kwa misingi ya kidemokrasia, ambapo wengi wataamua.
“Kikao kinapoitishwa na kukiwa na makundi yanayopingana hivi, huangaliwa walio wengi na kama akidi imetimia. Tumejiridhisha kuwa akidi itafikiwa,” amesema.
Amesema wajumbe wengi wako tayari kutekeleza uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa na hawawezi kusubiri kundi moja lijiridhishe ndipo kikao kiitishwe.
“Si kweli kwamba Msajili anapanga uongozi. Baraza Kuu ndilo litakalofanya uamuzi. Tunawaalika wote waje tuamue pamoja, kwani tayari tumepata baraka zinazohitajika,” amesema.
Alichokisema Sakaya
Kwa upande unaopinga mchakato huo, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya amesema hana taarifa yoyote kuhusu kikao hicho, licha ya kuwa ni mjumbe halali wa Baraza Kuu.
“Msimamo wetu ni kwenda mahakamani kama tulivyosema. Kwanza, baraza hilo linaitishwa na nani? Mimi ni Kaimu Katibu Mkuu wa Taifa baada ya Katibu Mkuu kuondolewa, ninapaswa kutoa taarifa ya kikao hicho,” amesema.
Amesema amekuwa akipigiwa simu na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali wakitaka ufafanuzi kuhusu kikao hicho, huku yeye akisisitiza hakijaitishwa rasmi.
“Tumepokea barua ya Msajili na tulikuwa tunaandaa fedha za nauli ili kuwaita wajumbe kujadili barua hiyo, kwa kuwa chama hakina ruzuku,” amesema Sakaya.
Amesema, pamoja na kwamba wamepanga kwenda mahakamani, hawawezi kukubali kikao hicho kifanyike bila kufuata utaratibu, akisisitiza ni jukumu lake kuwaita wajumbe.
“Hatuwezi kukubali kupangiwa viongozi na Msajili. Tutachukua hatua kuzuia hilo; ni lazima taratibu zifuatwe,” amesema.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alipoulizwa kuhusu kikao hicho, amesema anafuatilia taarifa hizo:“Inawezekana wameshawasilisha taarifa. Ngoja nifuatilie.”