
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imewaonya watu wanaokiuka sheria wakati wa mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, pamoja na wanaojadili mwenendo wa kesi hiyo mitandaoni kwa namna inayodaiwa ni ya kupotosha umma.
Katika onyo hilo, mahakama imesema imekuwa ikishuhudia vitendo visivyostahili vikifanyika wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa. Imeeleza kuwa kwa sasa imekuwa ikivumilia hali hiyo, lakini imesisitiza itafika wakati itachukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu na sheria za mahakama.
Onyo hilo limetolewa leo Alhamisi, Februari 19, 2026, kabla ya kuanza kwa usikilizaji wa kesi hiyo, kufuatia hoja iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ambayo hata hivyo ilipingwa na Lissu.
Tundu Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu. Shtaka hilo linatokana na maneno anayodaiwa kuyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Lissu anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Leo, kabla ya mahakama kuanza kupokea ushahidi wa shahidi wa 12 wa upande wa mashtaka, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude amewasilisha malalamiko kuhusu mwenendo wa baadhi ya watu nje ya mahakama.
Wakili Mkude amedai kuwa wakati kesi hiyo ikiendelea, kumekuwa na kauli mbalimbali zinazotolewa kuhusu mashahidi na ushahidi wao, pamoja na mwenendo wa kesi hiyo kujadiliwa katika mitandao ya kijamii.
Amedai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakizungumza na vyombo vya habari na kujadili ushahidi uliotolewa, hata kuhoji ustahiki wake jambo alilodai kuwa ni kinyume cha sheria.
Amefafanua kuwa hali hiyo imekuwa ikiendelea kwa muda mrefu, huku akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kifungu cha 114(1)(a) na (d).
Kwa mujibu wa kifungu hicho, mahakama ina mamlaka ya kuchukua hatua pale itakapoona kuna ukiukwaji wa taratibu unaoweza kuathiri mwenendo wa kesi.
Wakili Mkude amedai endapo hali hiyo itaachwa iendelee bila mahakama kutoa uamuzi au kuchukua hatua, inaweza kuhatarisha mwenendo wa kesi hiyo ambayo ipo katika hatua ya kupokea ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Naye Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amesema mahakama hiyo ilishatoa amri ya baadhi ya mashahidi walindwe na kuzuia kuchapishwa kwa taarifa za utambulisho, lakini kuna wafuasi wa chama fulani wanatoa taarifa kuwa mashahidi wanaolindwa, watahakikisha wanawajua.
“Hivyo ndio maana tunaomba mahakama ichukua hatua kwa mujibu wa sheria,” amesema Wakili Katuga na kusisitiza:
“Mtu anaitisha press kwenye eneo la mahakama inaonyesha inaweza kuingilia uhuru wa mahakama, kwani kama Jamhuri tunaona kuna vitu hazipo sawa na tuomba mahakama itolee uamuzi kwa sababu yenyewe ndio sehemu sahihi ya kutoa uamuzi.”
Amesema kuwa mambo hayo yamekuwa yanafanywa hata mawakili tena wengine ambao ni mawakili wakubwa tu wenye heshima.
Hata hivyo, Lissu amepinga hoja hizo na akaiomba mahakama isikubali kuzipokea kuwa sehemu ya mwenendo wa kesi hiyo.
“Waheshimiwa majaji nawaomba msiyakubali haya kwa sababu hamjayaona hayo yanayolalamikiwa yakitokea mbele ya mahakama, bali ni mambo ya nje ya mahakama,” amesema Lissu.
Amesisitiza kuwa majaji wasikubali kuletewa kesi za jinai ya namna hiyo ndani ya kesi hiyo bali kama mawakili wanaona kuna kosa la jinai, wakafungue kesi na kwamba kama kuna mawakili walifanya kosa, kuna utaratibu wa kushughulika na maadili ya mawakili.
“Majaji mnaalikuwa katika uwanja ambao hauna rooms za kisheria. Nasema hayo kwa sababu mimi nipo gerezani sijui social media zinavyoendelea,” amesema Lissu na kuhoji:
“Wanataa kesi hii kubwa iwe giazani? Haiwezekani, wanataka mjadalaa huu wa umma uende gizani? Majaji msipotezewe muda twende kwenye usikilizwaji wa kesi.”
Akijibu hoja za Lissu, Wakili Katuga amesisitiza mahakama iyafanyie kazi malalamiko hayo huku akidai kuwa hata mshtakiwa mwenyewe amekuwa akiwasilisha mahakamani mambo ya gerezani na yanafanyiwa kazi na akahoji kuwa kwa nini akatae hoja zao.
“Kitendo cha wao kusema mashahidi ambao ni wa kificho watawatafuta mpaka wawajue hicho ni kitisho,” amesema Katuga kuwa ndio maana Maahakama ilitoa amri ya kutokuchapisha taarifa za mashahidi wa kificho.
Akizungumzia madai hayo, Jaji Ndunguru amesema hata mahakama imekuwa ikiyaona mambo mbalimbali yasiyostahili yanafanyika ndani ya mahakama hata wakati kesi inaendelea na kwamba imekuwa ikiyavumilia lakini sasa itafikia hatua italazimika kuchukua hatua za kisheria.
Amesema mahakama imekuwa ikisisitiza watu wasitumie vifaa vya mawasiliano isivyostahili na akasema kuwa wanasisitiza watu wazingatie hayo.
“Tumekuwa tukivumilia sana mambo yanayoendelea hapa mahakamani. Tulisema tumevumilia sana, hivyo itafika hatua tutachukua hatua, japo sitaki tufikie huko,” amesema Jaji Ndunguru.
Miongoni mwa mambo ambayo mahakama iliwahi kuonya ni matumizi ya simu, na ilishawahi kusema kuwa imekuwa ikiwaona watu wakitumia simu zao kupiga na au kujipiga picha mahakamani wakati kesi inaendelea.
Kuhusu hoja ya Lissu kwa mambo ya yanayotokea nje ya mahakama, Jaji Ndunguru amesema kifungu cha hicho 114 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ambacho Jamhuri ilikirejea ni kipana.
Kifungu hicho kinaipa mamlaka mahakama kuchukua hatua hata kwa mambo yanayofanyika nje ya mahakama au eneo la mahakama kuhusiana na kesi inayoendelea, ikiwemo kutoa au kuchapisha taarifa uwongo au upotoshaji.
Kuhusu kauli ya Lissu kuwa kama kuna makosa ya jinai yanayofanywa nje ya mahakama basi mawakili wa Serikali wafungue kesi, Jaji Ndunguru amesema chini ya kifungu walichotaja mahakama ikiona kuna ukiukwaji, inaweza kuchukua hatua bila kisubiri mambo mengine.
Baada ya onyo na maelekezo hayo ya mahakama, ndipo mashahidi wa Jamhuri wakaendelea na ushahidi wao.