
Kigoma. Meli kongwe ya Mv Liemba iliyokuwa ikifanya safari zake kuzunguka mwambao wa Ziwa Tanganyika ikiwemo Kigoma, Katavi, Rukwa pamoja na nchi jirani ya Zambia, inatarajia kuanza safari zake tena Julai 2026 mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wake.
Meli ya Mv Liemba ilisimama kufanya safari zake mwaka 2018 kutokana na uchakavu ikiwemo mitambo yake, ambapo ukarabati wake ulianza Julai,2024 kwa kipindi cha muda wa miezi 24 kwa gharama ya zaidi ya Dola za Marekani 13 milioni na kutarajiwa kukamilika Julai 2026.
Akizungumza leo Februari 19, 2026 mjini Kigoma wakati Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alipotembelea bandari ya Kigoma na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo maendeleo ya ukarabati wa meli hiyo, Meneja mradi, Mhandisi Elias Kivara amesema ukarabati bado unaendelea na kwasasa umefikia asilimia 55.
“Ukarabati wa Meli yetu kongwe hadi kufikia sasa umefikia asilimia 55, na tunatarajia kufikia Juni 2026 tutafanya safari ya majaribio ambapo Julai 2026 itakuwa tayari kuanza safari zake rasmi kwani tutakuwa tushaikabidhi kwa mamalaka,” amesema Kivara.
Kivara amesema asilimia 45 zilizobakia kwa sasa ni ya kufunga vifaa ambayo vyote ni vipya ndani ya meli hiyo na kwamba kila kifaa kilichokuwa kimeagizwa kutoka nje ya Tanzania kimefika, hivyo hakuna kikwazo kitakachowafanya wao kushindwa kukabidhi meli hiyo kwa wakati.
“Meli hii imeboreshwa na kuwa ya kisasa kwani kuna baadhi ya vitu ambavyo havikuwepo awali tumeviweka ikiwemo viti vya kukalia vya kisasa, kutakuwa na sehemu ya burudani na kupata vinywaji itakayoweza kubeba watu 53, vyumba vya kulala kuwa na kiyoyozi na vifaa vya kiusalama kwa abiria akiwa safarini,” amesema Kivara.
Kaimu Meneja Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) Tawi la Kigoma, Humphrey Mwambungu amesema kukamilika kwa meli hiyo kutasaidia kuongeza uchumi wa mkoa kwa wafanyabiashara hasa wadogo wadogo.
Amesema wafanyabiashara wadogo wengi hawana uwezo wa kukodi gari ya kubeba biashara zao za vyakula kutoka mikoa ya Rukwa na Katavi, hivyo meli hiyo ikikamilika itawarahisishia kwa kuwapunguzia gharama na muda.
Naibu Waziri Kihenzile, pamoja na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo, amesema Mkoa wa Kigoma upo kimkakati na lengo ni kuteka masoko ya nchi za jirani ili wananchi wa Tanzania waweze kunufaika.
“Pamoja na kutembelea ujenzi wa meli Mv Liemba pia nimetembelea mradi wa ujenzi wa gati la abiria na gati la mizigo katika bandari ya Kigoma, bandari ndogo ya Kibirizi yenye ujenzi wa soko na kituo cha polisi, upanuzi wa kiwanja cha ndege pamoja na kukagua boti ya utafutaji na uokoaji, miradi hii yote inaenda kuifungua Kigoma,” amesema Kihenzile.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kiza Mayeye amesema miradi inayotekelezwa kwa ndani ya mkoa huo itaweza kuifungua Kigoma katika nchi za maziwa makuu ambapo wao kiu yao ni kuona Kigoma mpya yenye mabadiliko.
“Kufunguka kwa mkoa huo kutaweza kupunguza changamoto za ajira kwa vijana kwa sababu wawekezaji watawekeza na mwingiliano wa kibiashara baina ya nchi jirani utakuwa mkubwa,” amesema Mayeye.
Historia ya Mv Liemba
Ukarabati wa meli kongwe ya Mv Liemba iliyokuwa ikifanya safari zake kutoka Kigoma kwenda Zambia, umefikia asilimia 42 baada ya kusimama kufanya safari zake mwaka 2018 kutokana na uchakavu wa mitambo yake, ambapo ukarabati huo unagharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 13 kwa muda wa miezi 24.
Mv Liemba, meli iliyotumika vita vya kwanza vya dunia ina zaidi ya miaka 100 ambapo ilitengenezwa mwaka 1913 nchini Ujerumani na ikapewa jina la Graf von Goetzen, likiwa ni jina la gavana wa jimbo moja nchini humo.
Baada ya kutengenezwa ilifunguliwa vipande vipande na kisha kupakiwa kwenye maboksi 5,000 na kusafirishwa kwa meli mpaka Dar es Salaam Tanzania kisha kusafirishwa mpaka Tabora na kubebwa na watumwa mpaka Kigoma.
Baada ya kufika Kigoma ikaingizwa kwenye Chelezo na mwaka 1915 ikaanza kazi rasmi ikiwa na mizinga miwili mbele na nyuma. Pia, ilikuwa inatumika kusafirisha wanajeshi wa Ujerumani kuwapeleka katika bandari tofauti tofauti kwa ajili ya kupigana vita ikiwa ni pamoja na Bandari ya Kassanga na Mbala iliyopo nchini Zambia.
Mwaka 1957 ilibadilishwa jina na kuitwa Liemba, neno linalotoka kwenye jamii ya kifipa likiwa na maana ya maji. Mwaka 1961, ilikabidhiwa kwa Serikali ya Tanganyika na ikafanyiwa marekebisho yaliyojumuisha kubadilisha mfumo wa injini wa awali uliokuwa unatumia mvuke na kuweka mfumo wa Injini unaotumia dizeli.