
Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema mwitikio wa kampuni zinazojitokeza kuwekeza katika vitalu vya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia bado si wa kuridhisha, licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa kutangaza fursa hizo ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Februari 19, 2026 na Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mboja Ramadhan Mshenga, wakati akijibu swali la nyongeza katika mkutano wa Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar.
Mshenga alikuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Bakar Hamad Bakar (ACT–Wazalendo), aliyetaka kujua tathmini ya Serikali kuhusu mwitikio wa wawekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia.
Akijibu swali hilo, Mshenga amesema mwitikio wa kampuni si mzuri, japokuwa kwa sasa kuna kampuni moja iliyoonesha nia ya kuwekeza katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.
Katika swali lake la msingi, mwakilishi huyo alitaka kufahamu hatua zilizofikiwa katika mchakato wa utafutaji wa rasilimali hiyo muhimu, akieleza kuwa wananchi wana shauku kubwa kuona mchakato huo unakamilika ili waanze kunufaika na rasilimali hizo.
Akitoa ufafanuzi, Mshenga amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuchukua hatua madhubuti na za kimkakati kuendeleza utafutaji wa rasilimali za mafuta na gesi asilia, kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi na kuhakikisha wananchi wananufaika kwa maendeleo ya muda mrefu.
Amesema Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, kupitia Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA), imegawa vitalu 10 kwa ajili ya uwekezaji. Kati ya hivyo, vinane vipo baharini na viwili nchi kavu.
Amefafanua kuwa vitalu hivyo tayari vimetangazwa katika majukwaa mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ili kuvutia kampuni za mafuta na gesi asilia kuwekeza Zanzibar.
Aidha, amesema Serikali kupitia Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar ambapo Januari mwaka huu iliingia mkataba na kampuni ya African Geophysical Services (AGS) ya Oman, kwa ajili ya uchukuaji wa taarifa za mtetemo wa njia ya 3D katika maeneo ya nchi kavu.
Kwa mujibu wake, kukamilika kwa utafiti wa 3D kutaiwezesha Serikali kubaini maeneo mahsusi yanayofaa kuchimbwa visima vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, hatua itakayotoa mwelekeo sahihi wa kuendeleza sekta hiyo kwa tija zaidi.