
Nchi 24 za Magharibi zimeelezea wasiwasi wao kuhusu mauaji yanayoendelea kufanywa dhidi ya raia, uharibifu wa miundombinu na mashambulizi dhidi ya taasisi za misaada ya kibinadamu nchini Sudan, zikitoa wito kwa jeshi la Sudan na wapiganaji wa kundi la waasi la Rapid Support Forces kusitisha mapigano.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na nchi hizo jana Jumatano, iliashiria kwamba mashambulizi ya anga na ya ndege zisizo na rubani dhidi ya watu waliokimbia makazi yao, vituo vya afya na misafara ya chakula yamesababisha idadi kubwa ya vifo na majeraha ya raia, na yamezuia utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Taarifa hiyo imesema kwamba mashambulizi ya makusudi dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya kibinadamu au magari yao ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ni uhalifu wa kivita.
Vilevile imesisitiza udharura wa kufanyika uchunguzi wa haraka na huru kuhusu ukiukwaji huo wa sheria, na kufikishwa mbele ya sheria wahusika wa uhalifu huo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na nchi 24 za Magharibi imesisitiza kwamba majimbo ya Darfur (magharibi) na Kordofan (kusini magharibi mwa Sudan) yanasumbuliwa na mgogoro mbaya zaidi wa binadamu duniani, ikiashiria njaa na unyanyasaji wa kingono, pamoja na kukimbia watu 100,000 katika miezi ya hivi karibuni huko Kordofan pekee.
Katika muktadha huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ameelezea wasiwasi wake kuhusu ripoti za raia zaidi ya 50 kuuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani nchini Sudan siku za Jumapili na Jumatatu wiki hii.
Afisa huyo wa UN ametoa wito kwa pande zote kusitisha mashambulizi akisisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za haraka za kuwalinda raia, ikiwa ni pamoja na “kujizuia kuwatumia raia kwa madhumuni ya kijeshi.”