
Dar es Salaam. Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imelielekeza Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamia sheria, kanuni na taratibu zinazowataka wawekezaji wakiwemo wa Serikali kuhakikisha hawaanzi kutekeleza miradi kabla ya kufanyiwa tathmini ya athari ya mazingira na kupata cheti.
Pia, imewahimiza wadau wa mazingira, hasa washauri elekezi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha tathmini za mazingira zinaangalia namna bora ya uwekezaji ulio endelevu na unaozingatia utunzaji wa mazingira, ikiwa pamoja na kuzuia athari ya mabadiliko ya tabianchi katika miradi mbalimbali ya maendeleo yenye tija kwa jamii.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Februari 19, 2026 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Mteri alipomuwakilisha waziri wa wizara hiyo, Hamadi Masauni katika mkutano mkuu wa saba wa Chama Cha Washauri Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA).
“Ili kuhakikisha azma hii inafikiwa tumekuwa tukifanya marekebisho ya kanuni na sheria mfano EMA 2025 pale tunapoona inahitajika ili kufikia uwekezaji endelevu kwa utunzaji bora wa mazingira.”
“Kutokana na marekebisho hayo tumeongeza vipengele vya kuangalia athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo imekuwa moja ya changamoto kubwa katika kufikia maendeleo endelevu yanayotokana na uwekezaji unaojali utunzaji wa mazingira,” amesema.
Amesema walifanya hayo ili kuboresha Tathmini za Athari za Mazingira (TAM) huku akitaka wazingatie kuangalia athari zinazoweza kusababisha mabadiliko ya tabianchi wanapofanya kazi.
Aidha, Mteri amesema ameitaka NEMC kuendelea kusimamia kwa weledi shughuli za mazingira kote na kuhakikisha uwekezaji huo endelevu unaojali utunzaji wa mazingira unafanyika kila mahali nchini.
“Waelimisheni wawekezaji, wananchi na wanamazingira ili kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa kuzingatia weledi. Chukueni hatua kwa wale wote wanaokiuka sheria za utunzaji wa mazingira hasa kuhusu maswala ya uwekezaji,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa TEEA, Emmanuel Hanai ameomba taasisi hiyo itambuliwe kisheria kupitia Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Usajili na Utendaji wa washauri elekezi) za mwaka 2021.
Kutambuliwa kwake kutasaidia chama kutambuliwa na taasisi zingine nchini ikiwemo serikali za mitaa, na kuwapa ushirikiano pindi wanapokwenda kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali kwa manufaa ya Taifa.
Vilevile amesema taasisi za Serikali zinatekeza miradi bila kufuata utaratibu wa kufanya TAM, hivyo huwakosesha fursa ya kushauri namna bora ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.
Naye Katibu mkuu TEEA, Reuben Makalla akielezea lengo la mkutano huo wa mwaka amesema ni kwa ajili ya kuwaleta wadau na kuzungumza lugha moja kuhusu mazingira.
Kwa upande wake, Mshauri elekezi wa Mazingira, Zafarani Madai kutoka TEEA amesema changamoto walizozibaini ni kukosa kushirikishwa katika masuala muhimu ya maendeleo nchini.
“Mfano katika mipango miji unakuta kwamba washauri elekezi hawashirikishwi ipasavyo kwa sababu sisi tunavyoshirikishwa tunaweza kusema kwamba hapa panafaa au hapafai na tukatoa ushauri wetu namna gani mradi utatekelezwa mahali pale au mipango miji ifanyike, wakati tukiangalia masuala ya mazingira,” amesema.