
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa njama na vitendo vya uharibifu vilivyotekelezwa na utawala wa Israel dhidi ya mpango wa nishati ya nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu viliilazimisha Iran kuelekea kujitegemea kikamilifu katika sekta ya nyuklia. Alieleza kuwa mchakato huo ulikuwa ni jibu la moja kwa moja kwa shinikizo la muda mrefu na juhudi za makusudi za kuvuruga maendeleo ya nchi.
Akihutubia hafla moja mjini Tehran siku ya Jumatano, Mohammad Eslami alibainisha kuwa ugumu wa teknolojia za nyuklia uko katika kiwango cha juu sana. Amesema vifaa vya nyuklia si rahisi kupatikana, hasa katika mazingira ambayo njia za kimataifa za usambazaji zimeathiriwa na kutokana na kuwepo majasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ameongeza kuwa, “kwa sababu hiyo, Iran ililazimika kuunda ndani ya nchi mlolongo mzima wa utafiti, usanifu, ujenzi, majaribio, na ukomavu wa kiteknolojia, njia ambayo sasa imeanza kuzaa matunda.”
Afisa huyo alisema kuwa Iran leo inakabiliwa na hali ambapo adui, akitumia nguvu zake zote, zana, miundombinu na uwezo wake, anajaribu kuiporomosha nchi.
Akizungumzia juhudi za maadui za kulazimisha maslahi yao duniani kote, ikiwemo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, mkuu huyo wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametaja msukumo unaoendelea wa Marekani, kama ulivyoainishwa katika Hati ya Mkakati wa Usalama wa Taifa wa Washington wa mwaka 2026, wa kutekeleza maslahi yake ama kupitia diplomasia au kwa kutumia nguvu.
Amesema kwa miaka mingi hatua hizo zimejumuisha kulengwa kwa sekta ya nyuklia ya Iran kupitia mbinu mbalimbali za uhasama kama vile vikwazo vingi visivyo halali, mauaji ya wanasayansi wa nyuklia, vitisho vya mara kwa mara vya mashambulizi ya kijeshi, na hata kushambuliwa kwa vituo vya nyuklia.
Hata hivyo, licha ya kampeni hizo zote, Eslami amesema kuwa Iran sasa inamiliki sekta ya nyuklia ya ndani, imara na inayotegemeka. Amesema: “Leo, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran na wananchi wa Iran wanayo sekta ya nyuklia iliyo bora, ya kizalendo, na ya kuaminika.”
Eslami amehusisha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya Iran na Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na uongozi wa nchi kwa kusema: “Kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu, uongozi wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na mrithi wake Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na kwa kutegemea azma ya vijana wenye elimu, maarifa na kujitolea, Iran imefikia kiwango cha juu katika nyanja za sayansi na teknolojia za kisasa.” Amesema sekta ya nyuklia ni miongoni mwa vielelezo vilivyo wazi zaidi vya maendeleo.