
NYOTA wa kikapu wa aliyetamba na Pazi msimu uliopita wa Ligi ya Kikapu Dar es Salaam, Josephat Peter ‘Tekenya’ amekuwa mchezaji wa kwanza wa mchezo huo picha yake kutumika kama logo kwenye mpira.
Akizungumza na Mwanaspoti, nyota huyo ambae amewahi pia kutamba na Dar City na JKT alisema heshima hiyo imetokana na ubora wake na kufuatiliwa kwa karibu na Mtanzania Hamid Suleiman anayeishi Marekani anayesimamia Kampuni ya HSW.
Alisema Suleiman amekuwa akimfuatilia katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) na kuvutiwa na kiwango chake na kuamua kumpa heshima hiyo kubwa.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Mtanzania kuwekwa picha yake kama logo ya bidhaa na aliyekuwa nyota wa soka nchini, Jella Mtagwa picha yake ilitumika katika stempu za barua.
Akizungumzia kuhusu mchezo huo hasa msimu wa 2026, alisema anatarajia utakuwa na ushindani mkubwa huku akiwa amejipanga kwani anajifua vizuri.
“Kwa kweli maandalizi yangu yananiweka vizuri kutokana na wachezaji ninaokutana nao mazoezini, wengi wao wanacheza pia Ligi ya BDL katika timu tofauti,” alisema Peter na kuongeza, ligi hiyo imekua kwa kasi kutokana na uwepo wa nyota wa kigeni wanaowapa mzuka wazawa kujituma.
“Kipindi cha nyuma, kabla ya wachezaji wa kigeni kuanza kucheza Ligi ya BDL, viwango vya wachezaji wazawa vilikuwa chini, kuwepo kwao kwa sasa viwango vimeonekana kupanda.”
Nyota huyo anayecheza nafasi ya namba 1 (Point Guard), aliwataka wachezaji wajitume katika mazoezi kwani bila ya kufanya hivyo wanaweza kukosa timu ya kuwasajili kwa Ligi hiyo ya Mkoa.