Njombe. Wakulima na wafanyabiashara mkoani Njombe wametakiwa kuongeza uzalishaji wa matunda ya parachichi na kuwekeza katika viwanda vya uchakataji, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuongeza thamani ya mazao yao.

Wito huo umetolewa kufuatia jitihada za Mkoa wa Njombe kujitangaza kimataifa kupitia zao la parachichi, ambalo linatajwa kuwa na mvuto mkubwa katika soko la dunia.

Akizungumza leo Alhamisi, Februari 19, 2026 katika mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara la Mkoa wa Njombe, Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka amesema ni wakati sasa kwa wakulima na wafanyabiashara kujikita katika uzalishaji wenye tija na kuachana na mijadala isiyo na manufaa ya kiuchumi.

Amesema makundi yote yenye mwelekeo wa kiuchumi katika mkoa huo yanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye uwekezaji na uzalishaji badala ya kutumia muda mwingi katika shughuli zisizo na mchango wa moja kwa moja katika kukuza uchumi wa mkoa.

“Makundi yote ya mkoa ambayo unadhani ni ya kiuchumi yanapaswa kujikita katika uwekezaji, si kushona suti na kwenda majumbani kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka,” amesema Mtaka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas amesema wilaya hiyo kupitia mpango maalumu wa uzalishaji imejipanga kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ili kuinua kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa.

Amesema katika malengo waliyojiwekea ifikapo mwaka 2027, wanatarajia kuongeza uzalishaji maradufu katika sekta ya kilimo, hatua itakayosaidia kuongeza mapato ya wakulima na kuchochea maendeleo ya wilaya.

“Wilaya ya Ludewa kupitia mpango wa uzalishaji tumejiwekea malengo kwamba kufikia mwaka 2027, kwa upande wa kilimo tuwe tumeongeza uzalishaji mara mbili,” amesema Thomas.

Naye mkulima wa parachichi mkoani Njombe, Alfred Luvanda ameomba Serikali kupitia taasisi inayosimamia ubora wa bidhaa na huduma kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanakidhi viwango vinavyotakiwa ili kuvutia soko la ndani na nje ya nchi.

Amesema ubora wa matunda ni muhimu katika kujenga soko la uhakika na kuwanufaisha wakulima pamoja na wadau wengine wa mnyororo wa thamani.

“Matunda yetu yazalishwe katika kiwango bora ambacho hata soko lake litakuwa na uhakika na kila mtu atanufaika,” amesema Luvanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *