Taarifa iliyotolewa hii leo OHCHR jijini Geneva, Uswisi iansema ripoti ni ya matukio ya kuanzia tarehe 1 Novemba 2024 hadi tarehe 31 Oktoba 2025 na inaeleza kuwa mashambulizi makali, uharibifu wa kimfumo wa mitaa mizima na kuzuiwa kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza vinaonekana kulenga kubadili muundo wa idadi ya watu kwa kuwahamisha kabisa wapalestina.
Halikadhalika, mamia ya raia wameendelea kuuawa au kukatwa viungo vyao, njaa imesambaa, miundombinu ya kiraia imeharibiwa na hivyo kuweka mazingira ambamo kwamo wapalestina kama kundi watashindwa kuendelea kuishi Gaza.
Idadi kubwa ya watu huko Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao mara kadhaa.
Ukosefu wa uwajibikaji unachochea ukiukwaji wa haki
Ripoti hiyo ya kurasa 17, inaeleza kuwa watu wasiopungua 463, wakiwemo watoto 157, wamefariki kutokana na njaa baada ya misaada kuzuiwa kuingia Gaza kuzuiwa kwa msaada kuingia Gaza. Ripoti hiyo inaonya kuwa matumizi ya njaa kama silaha ya vita yanaweza kuwa uhalifu wa kivita na hata uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Katika Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Mashariki mwa mji wa Yerusalemu, ripoti inaeleza matumizi makubwa ya nguvu, kukamatwa kiholela, mateso gerezani na ubomoaji wa nyumba za wapalestina, hali inayodaiwa kuchangia kuwahamisha watu kwa nguvu.
Aidha, ripoti imetaja kuendelea kushikiliwa kwa mateka na makundi ya kipalestina, pamoja na vifo vya wapalestina 79 wakiwa kizuizini nchini Israel.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk, amesema ukosefu wa uwajibikaji unachochea ukiukwaji zaidi wa haki za binadamu na kusisitiza kuwa haki kwa manusura ni msingi wa amani ya kudumu.
Watoto katika Gaza wanashiriki katika masomo katika nafasi ya kujifunza ya muda iliyoanzishwa na UNRWA.
Mapendekezo ya ripoti
Ripoti inapendekeza mataifa yote kusitisha uuzaji na uhamishaji wa silaha kwa Israeli, silaha ambazo inasema zinaweza kuchangia ukiukwaji wa sheria za kimataifa.
Halikadhalika zihakikishe uwajibikaji kwa wahusika wa ukiukwaji huo, na kuruhusu ushiriki wa haraka wa wapalestina katika mipango ya uongozi na ujenzi upya wa Gaza.
Ripoti hii inatolewa leo wakati Rais wa Marekani, Donald Trump leo anaitishia kikao cha kwanza cha Bodi ya Amani aliyoiunda mwezi Novemba mwaka jana, Bodi ambayo iliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.