
Dar es Salaam. Mwanamuziki mkongwe wa Dansi, Zahir Zorro, ametoa ufafanuzi kufuatia ujumbe aliouandika kwenye akaunti yake ya Facebook na kuibua taharuki kwa mashabiki na wadau wa muziki.
Katika ujumbe uliosambaa kwa kasi mitandaoni, Zorro aliandika: “Nahitaji mashine saba za kuzima moto nizikwe nazo kwanini? Nafahamu niendako.”
Pia akaandika: “Chilling Kisota. Marafiki wamenitakia Toba leo. Nisiende na mashine 7 za kuzima moto!”
Kauli hizo zimewafanya wengi kudhani huenda msanii huyo anapitia changamoto za kiafya au maisha.
Mwananchi imezungumza na Zahir Zorro ambapo amesema ujumbe kama huo ni sehemu ya ubunifu wake wa maudhui. Akisisitiza kuwa mashabiki hawapaswi kuwa na taharuki.
“Ujumbe ninaoposti kwenye akaunti yangu ya Facebook ni vibonzo. Watu waache taharuki, akaunti yangu ni biashara, mimi ni creator (muundaji), vitu vyote ninavyoweka ninavitengeneza nalipwa na Facebook,” amesema Zorro.
Ameeleza kuwa, akaunti yake ni sehemu ya kazi na chanzo chake cha kipato, kwani analipwa kutokana na maudhui anayoyaweka, hivyo kila anachochapisha kinakuwa ni sehemu ya ubunifu wa kuvutia watu.
“Akaunti yangu ni biashara, ni peji ya visa, mimi ni creator. Vitu vyote ninavyoposti ninavitengeneza. Nikisema naumwa au nikaandika ujumbe fulani, watu wanashangaa na kuzungumza. Lakini huo ndio ubunifu, mimi nalipwa na Facebook,” aliongeza.
Mbali na hilo, msanii huyo pia amegusia picha yake mpya aliyoiweka hivi karibuni, inayoonyesha amepungua mwili tofauti na alivyokuwa zamani.
Amesema lengo la kuweka picha hiyo lilikuwa ni kuwaonyesha mashabiki mabadiliko yake ya sasa, kwani wengi bado wanamfahamu akiwa na mwili mkubwa.
“Watu wengi walikuwa wanajua bado niko vile zamani, bonge la mtu, nilivyoweka picha yangu ya sasa, kila mtu alishangaa,” amesema.
Aidha, Zorro amewatoa hofu mashabiki wake kwa kusema yuko mzima wa afya na anaendelea vizuri. Akijikita zaidi katika kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, huku akiwa na mpishi maalum anayemwandalia chakula nyumbani.
Kauli yake imekuja wakati mashabiki wengi wakiendelea kufuatilia kwa ukaribu maudhui yake, ambayo yamekuwa yakizua mijadala na kuvutia hisia tofauti mitandaoni.