Unguja. Serikali imesema vijana hususani wanafunzi wa elimu ya juu wanapaswa kuwa mstari wa mbele kueneza uelewa sahihi, kupinga maneno ya chuki na migawanyiko kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hayo yameelezwa leo Februari 19, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Masauni wakati akifungua kongamano kuhusu elimu ya Muungano kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu Zanzibar lililofanyika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza).
Amewataka kuulinda Muungano kwani ni nguzo ya umoja wa Watanzania ambao ilianzishwa kwa misingi ya upendo, heshima na nia ya kujenga Taifa lenye mshikamano huku wakieleza kwa ufasaha na umuhimu wake kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Vijana ndio nguvu, akili na matumaini ya taifa, walichonacho vijana ni zaidi ya elimu mnayoipata, hivyo ni wajibu kuhakikisha urithi wa amani, umoja na upendo vilivyoachwa na waasisi wa Taifa vinaendelea kudumu,” amesema Masauni.
Pia, amewataka kuheshimu na kutetea misingi ya Muungano wa Tanzania, kukuza uhusiano mwema kati ya Watanzania wa Bara na Zanzibar, kujifunza na kuthamini tamaduni na historia za pande zote na kuepuka kauli au vitendo vinavyodhoofisha umoja wa kitaifa.
Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali Zanzibar wakiwa kwenye kongamano la kuhusu elimu ya Muungano kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Zanzibar lililofanyika Chuo Kikuu cha Taifa (Suza).
Amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa Aprili 23, 2024 wakati akizindua kitabu cha miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais (1964 – 2024), Ikulu Chamwino, Dodoma.
Katika agizo hilo Samia alieleza kuwa asilimia kubwa ya Watanzania hawana uelewa wa kutosha kuhusu Muungano ambapo kwa muktadha huo, kuna haja na umuhimu wa elimu ya Muungano kutolewa kwa makundi mbalimbali ya jamii ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu ambao wengi wao wamezaliwa baada ya Muungano.
Akizungumza katika kongamano hilo kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Salhina Mwita Ameir amesema pamoja na mambo mengine litaendelea kutoa fursa na manufaa mbalimbali, ikiwemo kuelimisha na kuhamasisha vijana na vizazi vipya kuhusu masuala ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kongamano hilo pia litasaidia kuongeza uelewa kuhusu mafanikio yaliyopatikana tangu kuasisiwa kwa Muungano, changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake, pamoja na malengo na dira ya kuudumisha na kuuenzi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mkurugenzi wa Muungano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Juma Salum amesema kongamano hilo litakuwa chachu muhimu ya kuwapatia uelewa mpana kuhusu historia, misingi, faida na malengo ya Muungano huo, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuulinda na kuutetea.