Dar es Salaam. Katika kikao chake cha Februari 19, 2026, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam limepitisha ya Sh192.6 bilioni kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo.

Bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2026/2027, imependekezwa kwa sauti moja huku madiwani hao wakieleza inakwenda kutekeleza shughuli za maendeleo ambazo zinasimamiwa na halmashauri kwa mujibu wa miongozo ya Serikali.

Ikifafanua matumizi ya fedha hizo, Ofisi ya Mkurugenzi wilayani humo imebainisha asilimia 30 ya fedha hiyo itaelekezwa katika miradi ya kawaida na asilimia 70 ikitumika kwa miradi mikubwa.

Aidha, imeelezwa Sh75.4 bilioni zimetokana na makusanyo ya mapato ya ndani ya halmashauri hiyo. Walipojiwa kwa ajili ya kuipitisha bajeti hiyo madiwani wote wameunga mkono kwa asilimia 100.

Wakati wananchi wa manispaa hiyo kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakihitaji ujenzi wa barabara, miundombinu ya elimu, afya miongoni mwa mengi, Meya wa Halmashauri hiyo, Uzairu Athumani amepongeza bajeti hiyo akiitaja kuwa inakwenda kujibu mahitaji hayo.

“Naomba niwapongeze madiwani na wataalamu wetu wote na Mkurugenzi wetu kwani asilimia 70 ya bajeti yote inakwenda kwenye miradi ya maendeleo, huku asilimia 30 pekee ikiendelea kwenye matumizi mengine ya kawaida.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Uzairu Athumani akifafanua vipaumbele vya bajeti ya Halmashauri hiyo baada ya kupitishwa kwa asilimia 100 na madiwani Februari 19, 2026.

“Yaani kwenye sekta ya elimu imetengwa kujenga madaraja ya maghorofa, kukarabati madawati na miundombinu huku kwenye afya ujenzi wa hospitali kubwa za ghorofa tano,” amesema.

Aidha, imeelezwa mwaka 2024/2025, makusanyo ya ndani yalikuwa asilimia 70 pekee tofauti na Sh75.4 bilioni za mwaka huu.

“Naona kazi nzuri kwenye makusanyo ya mapato inafanyika na wananchi wa Temeke wanatuunga mkono katika mipango yetu kama tulivyopanga kwenye bajeti hii, twendeni tukatimize,” ameongeza Meya Uzairu.

Akizungumza muda mfupi baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Katibu tawala msaidizi wa ukaguzi na ufuatiliaji Mkoa wa Dar es Salaam, Sudi Mpili amewapongeza madiwani hao kwa kupitisha bajeti yao kwa asilimia 100 akiwataka kuhakikisha wameweka vipaumbele vya kukidhi mahitaji yaliyopo.

Akizungumzia bajeti hiyo, Diwani wa Mbagala, Abdulkarim Piza, ameeleza kuridhishwa kwake na bajeti hiyo akiweka wazi kuwa imegusa mahitaji mengi ya kata hiyo inayokua kwa kasi katika manispaa ya Temeke.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *