Dar es Salaam. Asilimia 65.2 ya mauzo ya bidhaa za misitu yaliyofanyika katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2025 yalibebwa na mbao, ripoti ya uchumi wa Kanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inaeleza.

Ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha katika kipindi husika, mauzo yote ya bidhaa za misitu yalikuwa Sh282 bilioni huku mbao pekee zikipata mauzo ya Sh183.52, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh179.88 bilioni iliyokuwapo Septemba mwaka uliotangulia.

Hiyo inatajwa kuchangiwa na ukuaji wa soko la bidhaa hizo linachochewa na mahitaji ya ujenzi wa nyumba za makazi pamoja na majengo ya biashara.

Mauzo ya mbao ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vinavyotajwa na ripoti hiyo kuwa vimechangia ukuaji wa thamani ya bidhaa za misitu zilizouzwa kwa kipindi husika, ambapo ukuaji ulikuwa wa asilimia 4.9.

Mbali na mbao bidhaa nyingine zilizochangia ongezeko hili ni nguzo, mkaa na magogo. Uhitaji mkubwa wa ndani na nje ya nchi, pamoja na usimamizi wa karibu katika uvunaji na uuzaji wa bidhaa za misitu, ulichangia matokeo hayo chanya.

Kanda zote, isipokuwa Dar es Salaam na Kanda ya Kusini Mashariki, ziliripoti ongezeko la thamani ya bidhaa za misitu, huku Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ikichangia asilimia 95.2 ya jumla ya thamani hiyo.

Ripoti hiyo inaonyesha, nguzo za umeme mauzo yake yalifikia Sh43.502 bilioni, mkaa ulibeba Sh7.09 bilioni, magogo yalibeba Sh4.608 bilioni, mbao za kutengenezea samani zilikuwa za Sh48.7 milioni, kuni ziliuzwa za Sh169.2 milioni huku bidhaa nyingine za misitu zikibeba mauzo ya Sh42.67 bilioni.

“Siku hizi biashara imechangamka kwa sababu wanaohitaji mbao siyo wanaojenga nyumba pekee, wapo pia wanaobadili mifumo ya ujengaji wa sehemu za biashara kutoka kutumia matofali hadi mbao, hii imefanya soko kuongezeka,” amesema Mohammed Ali Mohammed mfanyabiashara wa mbao.

Amesema kuongezeka kwa soko hilo kumeongeza pia idadi ya watu wanaotamani kufanya biashara hiyo, kwani wamekuwa wakishuhudia kuongezeka kwa watu wanaotaka kujifunza na namna wanavyoweza kupata bidhaa.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania inahitaji takribani nyumba 390,981 kila mwaka ili kukabiliana na upungufu uliopo kutokana na ongezeko la idadi ya watu linaloshuhudiwa kila.

Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa uchumi, Dk Lutengano Mwinuka amesema kukua kwa mauzo ya mbao ni ishara kuna sekta nyingine inakua zaidi ikiwemo ile ya miliki ya majengo.

Amesema hiyo ni kutokana na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali tofauti na kuezekea ikiwemo milango, samani za mbao.

“Ni faida kwa sababu tunafahamu mtiririko wa mbao hadi inapozalishwa ambao lazima uwe umelima mti hadi umekomaa ili uweze kuvunwa, lakini ni vyema kufanya utafiti kuona kilimo cha miti ya mbao kikoje japokuwa tumeona kumekuwa na uendelevu wa maliasili,” amesema.

Amesema changamoto iliyopo ni kama sekta ya ujenzi na miliki ikikua kwa kasi inaweza kuleta shida ya upungufu wa mbao ambao unaweza kulazimisha kuanza kuagiza kutoka nje ya nchi, jambo ambalo bado halijaonekana.

“Lakini bado kuna fursa ya zaidi, inahitajika kuendelea kufanya bidhaa nyingine zitambulike kwani misitu ina fursa za kutoa bidhaa nyingi ambazo zinaweza kushindana, ikiwemo asali na kuna vingine vilivyojificha katika kuchakata mabaki yanayotokana na bidhaa za misitu kama malanda,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *