Dar es Salaam. Uamuzi na msimamo wa Serikali juu ya matumizi ya stendi mpya ya daladala ya Buza Kwamama Kibonge jijini Dar es Salaam tangu ulipotolewa Julai 2025 umeendelea kuzua vuta nikuvute kati ya wananchi na mamlaka za Serikali.

Serikali ilitangaza kuanza rasmi matumizi ya stendi hiyo iliyopo Buza, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, uamuzi uliombatana na kufungwa kwa baadhi ya vituo vya barabarani kikiwemo kile cha Kwamama kibonge na Buza Kanisani, ambavyo Serikali imevitangaza kuwa si rasmi.

Februari 10, 2026, akihutubia baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda aliagiza watendaji na madiwani kuhakikisha magari yote yanayofanya safari zake Temeke yanatumia stendi hiyo mpya iliyojengwa pembezoni mwa barabara ya Buza–Kwampalage.

“Maelekezo haya yanatoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameyarudia vilevile. Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu hivyo hatutaruhusu watu kuvunja utaratibu stendi hii lazima itumike kikamilifu,” alisistiza Mapunda.

Magari yakipishana katika barabara ya kuingia na kutoka Stendi mpya ya Buza kwa Mama Kibonge, Jumatano Februari 18, 2026.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa utekelezaji huo, mvutano umeendelea kushuhudiwa katika maeneo hayo ambapo magari yamekuwa yakisuasua kuingia stendi mpya, mengine yanaingia na baadaye kuendelea hadi Buza Kanisani, huku mengi yakiendelea kuishia Tandika, yakiwemo yale ya Tabata, Muhimbili, Kigamboni na Vikindu.

Aidha, licha ya kufungwa rasmi kwa kituo cha KwamamaKibonge, wananchi wameendelea kufurika eneo hilo wakigombania daladala na bodaboda ambazo zinapakia kwa kukwepana na askari wanaoimarisha doria.

Jumanne, Februari 17, 2026, Serikali ilianza kusimamia kwa nguvu zaidi utekelezaji wa maagizo hayo, hatua ambayo imeongeza mwitikio wa magari yanayoingia stendi mpya.

Wakazi wa Kwalulenge na Buza Kanisani Walivyoguswa

Wakati mkazo ukionesha mafanikio katika utekelezaji wa maelekezo ya Serikali, yameibuka malalamiko mapya kutoka kwa wananchi.

Wakazi wa Kwalulenge na Buza Kanisani wameeleza msimamo huo mpya umewaacha pembeni ya usafiri wakitaja kuwa awali daladala zilikuwa zikifika karibu na makazi yao, lakini sasa wanalazimika kutembea umbali mrefu au kulipia bodaboda kufika stendi mpya.

Malalamiko hayo yamekuwa yakipelekwa hadi kwa viongozi wa serikali za mitaa, ambao wameliambia Mwananchi kuwa wananchi wamekuwa wakifurika ofisi za mitaa na hata majumbani kwa viongozi wao wakitaka msaada juu ya hilo.

Baadhi ya fremu katika stendi mpya Buza kwa Mamakibonge zikiwa zimefungwa, hazijaanza kutumika Februari 18, 2026.

 “Wananchi hawaoni sababu ya kusitishiwa daladala za Buza Kanisani na kufutwa kwa kituo cha Kwamama Kibonge. Wanaona walikuwa wanapata huduma karibu zaidi na makazi yao, wanakuja kwa wingi kulalamika,” amesema mmoja wa wenyeviti wa mitaa katika kata hiyo akizungumza na Mwananchi lilipotaka ufafanuzi wake kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam, Shifaya Anaselema anaiomba Serikali kuruhusu daladala kwenda hadi Buza Kanisani ili kuwasaidia wakazi wa maeneo hayo kuepukana na taabu wanayoipata sasa.

“Kama ni sharti la kuingia stendi liachwe litatekelezwa lakini daladala ziruhusiwe kufika hadi Buza Kanisani ili kuwasaidia wakazi wa kule kuondokana na shida ya usafiri,” amesema.

“Kwa hali ilivyo sasa ni ngumu kwa wakazi hao kutoka kule hadi kufika stendi na wakitaka kufanya hivyo wataingia gharama nyingine labda ya kupanda bajaji au kutembea umbali mrefu.

“Na uamuzi wa kusema daladala ziishie stendi umeleta malalamiko sana, napigiwa simu nyingi kutoka kwa watu tofauti,” amesema.

Fremu za biashara

Katika stendi hiyo mpya, upo pia mjadala kwenye fremu za biashara, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wameliambia Mwananchi kuwa upatikanaji wa fremu umekuwa changamoto, wakidai kuwa nyingi zimechukuliwa na watu wachache wenye ambao hawafanyi biashara moja kwa moja bali wanazipangisha kwa gharama kubwa kwa wenye uhitaji.

Mfanyabiashara wa vinywaji, aliyejitambulisha kwa jina la Mama Neema, amesema fremu hizo licha ya kuwa zimelipiwa zote, hazifanyi kazi kwakuwa wengi waliozichukua wanapangisha kwa gharama ya zaidi ya milioni moja.

“Femu nyingi unazoziona hapa stendi zimechukuliwa na watu wenye fedha,  wanatupangishia kwa bei kubwa, sana, jana ndugu yangu amechukua fremu akalipia Sh2 milioni naona hivi,” amesema mama huyo.

Malalamiko hayo ambayo viongozi wa serikali za mitaa katika kata ya Buza wamekiri kuyapokea kutoka kwa wafanyabiashara hao, yameeleza taswira ya ushindani wa kiuchumi unaotokana katika kumiliki fremu ambapo wanaowahi awali wanachukua nafasi nyingi na kupangisha upya wakiwanyonya waliochelewa kushika nafasi.

Kushuka kwa biashara

Wafanyabiashara wengine wameeleza kuwa biashara zao zimedorora kutokana na mvutano huo wakidai kuwa utata wa watumiaji wa daladala na mgawanyiko wa vituo umeathiri mtiririko wa wateja hivyo kufanya maisha yao kuwa magumu.

“Nilipokuwa Kwamama Kibonge nilikuwa namaliza sado mbili na nusu kwa siku lakini hapa hata sado moja siimalizi, magari bado ni machache huku na abiria bado wanagawanyika,” amesema Rehema Mustapha, anayeuza samaki wa kukaanga stendi hapo.

Shughuli za kibiashara zikiendelea katika stendi mpya Buza Kwamama Kibonge, Jumatano Februari 18, 2026

Kauli hiyo imeakisi wasiwasi wa wafanyabiashara wanaotegemea wingi wa abiria kama mtaji wao kwa mauzo ya siku.

Changamoto ya miundombinu

Mbali na changamoto hizo, kero nyingine imeibuliwa na wananchi hao katika miundombinu ya barabara inayoingia na kutoka stendi hiyo.

Baadhi ya watumiaji wa stendi hiyo wakiwemo madereva wamesema barabara moja inayotumika kuingia na kutoka stendi hapo inayosababisha magari kufungana na kuzalisha msongamano.

“Tunataka kufuata utaratibu wa Serikali, lakini barabara ya kuingia na kutoka ni moja, magari yakishakuwa mengi hapa safari zitakuwa zinachelewa maana patazaliwa foleni kubwa hapa,” ameeleza dereva wa daladala, Jumanne Hassan.

Kwa upande wake, dereva wa bajaji, Rashid Hamza amesema, watumiaji wa bajaji nao wamepungua akiweka wazi kuwa bajaji zinakaa muda mrefu kusubiri abiria wachache wanaoshuka kwenye magari kituoni.

Aidha, wananchi hao wamependekeza kujengwa barabara ya pili ili kutenganisha magari yanayoingia na yanayotoka, wakiamini hatua hiyo itapunguza msongamano na kuongeza ufanisi.

Serikali yashikilia msimamo

Katika kuweka namna ya utumiaji wa huduma hizo, Serikali kupitia Halmashauri ya Temeke imeendelea kusisitiza Kwamama Kibonge si kituo rasmi na kwamba magari yote yanayofanya safari zake Buza  yanapaswa kutumia stendi mpya hiyo.

Akirejea msimamo huo ambao tangu mwaka jana uliwekwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, mbele ya madiwani na watendaji wa kata na mitaa, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sixtus Mapunda alisisitiza akisema, watendaji watakaoshindwa kusimamia vyema majukumu yao ikiwemo matumizi sahihi ya vituo na stendi za daladala watachukuliwa hatua ikiwemo kuondolewa kwenye nafasi zao.

Wito wa ushirikishwaji

Akizungumzia kiini cha migogoro ya aina hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abel Kinyondo alisema migogoro mingi ya miradi ya umma hutokana na kukosekana kwa ushirikishwaji wa wananchi katika hatua za maamuzi.

Magari yakishusha na kupakia abiria ndani ya Stendi mpya ya Buza Kwamama Kibonge, Jumatano Februari 18, 2026

“Unapotekeleza mradi bila kuwahusisha wananchi kikamilifu katika kupanga matumizi yake, unazalisha sintofahamu. Ushirikishwaji huwafanya watu kuimiliki miradi na kuondoa mivutano nao,” alisema Profesa Kinyondo.

Aliongeza viongozi wanapaswa kusikiliza sauti za wananchi na kuwapa nafasi ya kushiriki katika maamuzi ili miradi ya maendeleo isigeuke kuwa chanzo cha mvutano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *