
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba, mipango ya utawala ghasibu wa Israel ya kuimarisha udhibiti wa sehemu za Ukingo wa Magharibi inakwenda sambamba na kutwaa eneo hilo kimabavu.
Rosemary DiCarlo amesema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la umoja huo.
“Tunashuhudia hatua kwa hatua unyakuzi wa eneo la Ukingo wa Magharibi, kama hatua za Israel za upande mmoja zinavyozidi kubadilisha mazingira,” Rosemary DiCarlo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Mambo ya Siasa na Ujenzi aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu suala la Palestina.
“Zikitekelezwa, hatua hizi zitajumuisha upanuzi hatari wa mamlaka ya kiraia ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, ikiwa ni pamoja na katika maeneo nyeti kama al-Khalil.
“Juhudi za sasa zinapaswa kulenga kuimarisha usitishaji huo wa mapigano, kuongeza misaada ya kibinadamu na kuweka msingi wa amani ya kudumu kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema Bi. DiCarlo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, zaidi ya nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimelaani mpango wa Israel wa kupora na kuyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, na kuyatambua maeneo hayo ya Palestina kama “milki ya serikali” ya Israel.
Radiamali hizo za nchi 80 wanachama wa UN, Hamas, wadau wa kikanda na serikali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Iran, Bunge la Kiarabu, na Wizara za Mambo ya Nje za Qatar na Misri, zinasisitiza kuwa, mpango huo wa utawala wa Kizayuni utakuwa na matokeo makubwa hasi si tu kwa Palestina, bali kwa eneo lote la Asia Magharibi.