Waziri wa Nishati wa Marekani amesema, nchi hiyo itaanza tena kurutubisha madini ya urani
Kwa mujibu wa Pars Today, Waziri wa Nishati wa Marekani Chris Wright ametangaza kwamba, Washington itaanza tena mpango wake wa kurutubisha urani ndani ya nchi hiyo. Wright ametoa tangazo hilo katika mkutano uliofanyika mjini Paris, Ufaransa.
Waziri wa Nishati wa Marekani amesema, mpango huo, kwa kiwango fulani utatekelezwa kwa ushirikiano na baadhi ya washirika wa ndani ya Ufaransa. Matamshi hayo yametolewa huku Marekani na washirika wake wa Ulaya wakitafuta njia za kupunguza utegemezi wao kwa wauzaji wa nje wa fueli ya nyuklia hususan Russia.
Mnamo mwezi uliopita, kampuni ya fueli ya nyuklia ya Ufaransa ya Orano ilifanikiwa kupata fungu la hadi dola milioni 900 kutoka wizara ya nishati ya Marekani ili kushiriki katika ujenzi wa kituo cha kurutubisha urani katika jimbo la Tennessee. Mradi huo ni sehemu ya juhudi kubwa zaidi zinazofanywa na Washington ili kuimarisha uwezo wake wa ndani katika uchakataji wa mzunguko wa fueli ya nyuklia.

Tangazo la kurutubishwa urani ndani ya Marekani, kwa hakika linadhihirisha mgongano na undumakuwili wa wazi kabisa wa sera za nje za nchi hiyo. Kwa sababu, kwa upande mmoja, Washington inaitaka Iran isimamishe kikamilifu na bila masharti yoyote urutubishaji wa urani, lakini kwa upande mwingine, yenyewe inaanzisha tena mipango yake ya kurutubisha madini hayo kwa madhumuni ya kibiashara na ya kimkakati. Muelekeo huo wa Washington umeibua maswali mazito kuhusu undumakuwili huo wa msimamo wa Marekani pamoja na misingi ya kisiasa na kisheria ya sera za nchi hiyo kuhusiana na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia, NPT.
Kwa kweli tangazo la waziri wa nishati wa Marekani kwamba nchi hiyo itaanza tena kurutubisha urani, wakati Washington inatoa mashinikizo makali kabisa dhidi ya Iran ya kuitaka isimamishe kikamilifu mchakato huo, ni mfano wazi kabisa wa sera za kiundumakuwili na kibaguzi katika uga wa kimataifa. Muelekeo huo, sio tu unatilia shaka itibari na ukweli wa ahadi za Marekani za kutopanua miradi ya silaha za nyuklia, lakini pia unaibua changamoto kubwa kwa mazungumzo ya nyuklia inayofanya hivi sasa na Iran.
Msimamo rasmi wa Washington kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran umevuka mipaka iliyowekwa kwenye makubaliano ya JCPOA. Wakati JCPOA iliiruhusu Iran irutubishe urani hadi kiwango cha asilimia 3.67, serikali ya sasa ya Marekani imeweka sharti la “urutubishaji wa sifuri” na kufungwa kikamilifu shughuli za kurutubisha urani ndani ya ardhi ya Iran. Katika mazungumzo ya hivi karibuni nchini Oman, maafisa wa Marekani walibainisha suala hilo kuwa ndilo sharti lao kuu, na hata wakapendekeza kwamba, urani ya Iran iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu (asilimia 60) ihamishiwe kwenye nchi ya tatu. Washington inatetea na kuhalalisha msimamo huo, kwa hoja ya kuwa na wasiwasi wa kuenea silaha za nyuklia na ulazima wa kuizuia Iran isiwe na uwezo wa kinyuklia.
Katika kile kinachoonyesha mgongano wa wazi wa takwa hilo, serikali ya Marekani imechukua hatua ya kutekeleza sera ya ustawishaji na uanzishaji tena shughuli za urutubishaji urani ndani ya nchi hiyo. Lengo la kuchukuliwa hatua hiyo limetajwa kuwa ni kudhamini fueli ya nyuklia kwa ajili ya vinu vya nyuklia nchi hiyo na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nchi nyingine ikiwemo Russia. Uamuzi huo unaonyesha kuwa, Washington inauchukulia urutubishaji urani kuwa ni shughuli halali na ya dharura kwa ajili ya kulinda maslahi yake ya taifa, lakini haiitambui kuwa nayo haki hiyo Iran, ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji Silaha za Nyuklia (NPT). Sera hii ya kizandiki na ya undumakuwili ndio chanzo cha mgongano katika muelekeo wa Marekani; yaani “urutubishaji ni kwa ajili ya mimi, na ni marufuku kwa wewe”. Mkabala na msimamo huo, Iran imeeleza kwamba, inaweza kulegeza msimamo kuhusiana na viwango vya urutubishaji, lakini vyovyote itakavyokuwa, haitaachana na haki yake ya kuendelea kurutubisha urani.
Kwa mtazamo wa Tehran, muelekeo huo ni ishara ya wazi kabisa ya uzandiki na kutoaminika nia ya Marekani. Viongozi wa Iran wamesisitiza kwamba, haki ya kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani, ni haki “isiyokanushika” kulingana na Mkataba wa NPT kwa nchi zote wanachama, ikiwemo Iran. Wakati Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araghchi alipohutubia Mkutano wa Utokomezaji Silaha uliofanyika makao makuu ya Umoja wa Mataifa ya Ulaya huko Geneva mnamo Februari 17, alisisitiza kwamba haki ya Iran ya kutumia nishati ya nyuklia haiwezi kujadiliwa. Mnamo Februari 8, Araghchi alibainisha kuwa, Iran haitaachana kamwe na mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani pamoja na urutubishaji wa urani, na akasisitiza kwamba, sharti la kufanikiwa mazungumzo na Marekani ni kukubaliwa “haki hiyo.”

Inavyoonekana, sera ya undumakuwili ya Washington kuhusiana na urutubishaji wa urani chimbuko lake ni muelekeo uitwao “kiwango cha juu kabisa” wa Marekani, ambao unalenga kuiburuza Iran ibadilishe kikamilifu mwenendo wake katika kila kitu, ikiwa ni pamoja na mpango wake wa makombora na sera yake ya kikanda, ukiwa unakwenda mbali zaidi na kuvuka mpaka wa kadhia ya nyuklia. Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, matakwa hayo ya “kiwango cha juu kabisa”, -ambayo yameambatana na hatua kadhaa, ikiwemo kuchukua hatua kubwa za kijeshi kandokando ya mipaka ya Iran, hususan kutumwa manowari ya kubebea ndege za kivita ya Abraham Lincoln ikifuatiwa na ya Gerald Ford, sambamba na kutolewa vitisho vya mashambulizi ya kijeshi, na yanafanyika zaidi kama wenzo wa mashinikizo katika mazungumzo- hayawezi kupatikana.
Kwa ujumla ni kwamba, sera ya undumakuwili ya Marekani kuhusiana na urutubishaji wa urani imeibua changamoto kubwa kwa mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana ya nyuklia na ya uondoaji vikwazo. Maadamu Washington ingali na imani kwamba, inaweza kwa upande mmoja kulinda haki yake ya urutubishaji, na kwa upande mwingine kutotambua na kukubali haki ya Iran juu ya suala hilo, ni baidi kwamba makubaliano ya kudumu yataweza kufikiwa. Mgongano huu unadhoofisha itibari ya NPT, ambayo inatambua rasmi haki ya nchi zote wanachama ya kuendesha miradi ya nyuklia kwa malengo amani, ikiwa ni pamoja na kurutubish urani, na unashadidisha pia hali ya kutoaminiana katika mahusiano ya kimataifa…/