Dar es Salaam. Licha ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutoa tangazo la kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, hali halisi inaonyesha shughuli hizo bado zinaendelea katika baadhi ya mitaa ya Kariakoo kama kawaida.
Tangazo hilo lililosainiwa na Mkurugenzi wa Jiji, Elihuruma Mabelya, lilibandikwa Jumanne Februari 17, 2026 kwenye nguzo za umeme za zege katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo ikiwemo Livingstone, Tandamti na Congo.
Lilielekeza wafanyabiashara wanaopanga na kuuza bidhaa katikati ya barabara na njia za waenda kwa miguu bila kupangwa kuondoa bidhaa zao mara moja.
Mbali na wafanyabiashara, tangazo hilo pia liliwahusu waendesha bodaboda na bajaji, likiwataka kuegesha katika vituo rasmi huku wale wasio na vituo wakiahidiwa kupangiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri.
Aidha, wafanyabiashara wenye maduka waliagizwa kuondoa bidhaa zote zilizopo nje ya maduka yao kinyume na taratibu za biashara.
Wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga wakiendelea na shughuli zao katika Mtaa wa Msimbazi licha ya uwepo wa tangazo la Halmashauri ya jiji kutoendelea na shughuli zao katika maeneo hayo
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyoyatoa Februari 8, 2026 wakati wa ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo, uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Chalamila alisema kuanza kwa huduma katika soko hilo kutaambatana na kufunguliwa kwa barabara zote zinazoingia na kutoka sokoni humo.
Hata hivyo, Mwananchi imefuatilia utekelezaji wa shughuli hiyo leo Alhamisi Februari 19, 2026 katika mitaa ya Uhuru na Msimbazi umebaini baadhi ya wafanyabiashara bado wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, wakipanga meza na bidhaa kandokando ya barabara na katika njia za waenda kwa miguu.
Akizungumza na Mwananchi katika kona ya Msimbazi na Narung’ombe, mfanyabiashara Abas Issa amesema hawajapata taarifa rasmi ya kuondoka.
“Sijaliona hilo tangazo wala hatujasikia tangazo la gari kusema tuondoke ndiyo maana unaona tunaendelea na shughuli zetu. Ikitokea tuingie ndani tutabanana sana,” amesema Issa.
Naye Rukia Mohamed, mfanyabiashara wa nguo katika mtaa wa Msimbazi na Muhonda, amesema wameona gari la jiji likipita na kubeba meza za baadhi ya wafanyabiashara, lakini hawajafahamu ni maeneo gani hasa yanaguswa na operesheni hiyo.
“Wakishabeba meza tunahamia kwenye mikono, wengine wanaweka bidhaa kwenye viroba, tukiona wanaanza kupita tunaingia ndani, wakiondoka tunaendelea maana hatuna sehemu nyingine ya kwenda. Kariakoo ndiyo sehemu yetu pekee kwa sasa,” amesema Rukia.
Wafanyabiashara wadogo maarufu Machinga wakiendelea na shughuli zao katika Mtaa wa Msimbazi licha ya uwepo wa tangazo la Halmashauri ya jiji kutoendelea na shughuli zao katika maeneo hayo
Katika mtaa wa Uhuru, mfanyabiashara mwingine, Salma Shomari, ambaye huuza bidhaa za umeme amekiri kuweka bidhaa nje ya duka lake ili kuvutia wateja.
“Ndani hakuna nafasi ya kuonesha bidhaa zote, nikiziacha ndani mauzo yanashuka kwa sababu wateja wengi hununua kwa kuona kilicho nje. Tunaomba jiji litupangie utaratibu mzuri badala ya kuchukua uamuzi wa kutoruhusu kuweka nje,” amesema Salma.
Kwa upande wa mwendesha bodaboda, Johari Sebastian amesema baadhi yao husimama Kariakoo si kwa kuwa ni vituo vyao rasmi, bali kwa kuvizia abiria baada ya kushusha wengine.
“Nimesimama hapa nasubiri abiria wa haraka, siwezi kurudi Mbagala nikiwa mwenyewe baada ya kuleta abiria lazima nipate hata pesa ya mafuta,” amesema Sebastian.