Dar es Salaam. Baada ya siku moja Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kumaliza mgogoro wa nyumba iliyopo mtaa wa Mkunguni na Bonde, Kariakoo kwa kumkabidhi mnunuzi, miongoni mwa wanafamilia wamepinga uamuzi huo na kukimbilia katika Kliniki ya Sheria kwa ajili ya kupata msaada.

Familia hiyo ya marehemu Abdalla Mtambo aliyefariki dunia tangu mwaka 1964 imefika katika eneo la Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam ambako Kliniki ya Sheria inafanyika tangu Februari 16, 2026 kutafuta msaada wa kisheria, kufuatia uamuzi wa Mkuu huyo wa mkoa kukabidhi nyumba yenye mgogoro kwa mnunuzi.

Akizungumza na Mwananchi Februari 18, 2026, Asha Ausi amesema wamelazimika kutafuta ushauri wa kisheria baada ya kuhisi hawakutendewa haki katika mchakato wa madai ya umiliki wa nyumba hiyo.

Asha Ausi ambaye amezungumza kwa niaba ya Maraya Abdalla (96), amesema msingi wa malalamiko yao ni madai kwamba nyumba hiyo haikuwahi kuuzwa kwa mnada halali kama inavyodaiwa.

“Tunasema wazi, mnada haukufanyika, hakukuwa na tangazo rasmi, wala hatukushirikishwa wanafamilia wote kuanzia mama yetu, watoto hadi serikali ya mtaa hawajawahi kusikia huo mnada,” amesema Asha.

Amesema kuhusu nyumba hiyo kuuzwa kwa mnada wamesikia kwenye mkutano wa Mkuu wa Mkoa akiwa na waandishi wa habari ambapo wao hawakupewa fursa ya kuzungumza chochote, licha ya kupaza sauti ya kutokuwepo kwa jambo hilo.

“Hatuelewi hili jambo limekuwaje maana Mkuu wa Mkoa alikuja nyumbani Januari tukaongea naye na tukamwelewesha kila kitu na akasema ataunda kamati lakini jana tumeona kaja na watu na kutoa huo uamuzi na hawakutaka tuseme chochote,” amesema Asha.

Kutokana na uamuzi huo, amesema hawana imani na kamati ya mkuu wa mkoa iliyofuatilia kesi hiyo kwa sababu kumekuwa na kasoro nyingi ikiwemo madai ya uuzwaji wa nyumba kwa njia ya mnada mwaka 2011.

Amesema mgogoro wa nyumba hiyo ni wa muda mrefu na waliotaka nyumba iuzwe ni wajukuu ambao wazazi wao walishafariki dunia na hadi kufikiwa hatua hiyo watoto waliokuwa hai kati ya sita walikuwa wawili ambapo mmoja amefariki dunia mwaka 2025.

“Waliokubali nyumba kuuzwa ni wajukuu, lakini mama yetu na mdogo wake walikataa na tunapinga kwa sababu utaratibu haukufuatwa. Nyumba ni ya marehemu ambaye aliacha watoto sita, kwa hiyo kila mmoja ana haki ya kusikilizwa,” amesema Asha.

Awali, Mkuu huyo wa mkoa aliunda kamati maalumu ya kuchunguza mgogoro huo baada ya kufika eneo la tukio Januari 19, 2026 ambao unamhusisha mtoto wa marehemu Maraya Abdalla na mnunuzi Salim Salim ambaye alinunua nyumba kwa njia ya mnada kutokana na amri ya mahakama iliyotaka kuuzwa kwa nyumba hiyo.

Akisoma historia ya mgogoro, Mwenyekiti wa Kamati na Mwanasheria wa Ofisi ya Mkoa huo, Fabiola Mwingira alisema chanzo cha mgogoro huu kinatajwa ni kifo cha Mtambo ambaye aliacha mali zikiwamo nyumba hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana wakati wa uchunguzi, warithi na wasimamizi wa mirathi walishindwa kuelewana ambapo mgogoro ulianza kwa warithi wa marehemu kutoridhishwa na mgawanyo wa mapato ya kodi ya upangishaji wa nyumba na kuiomba mahakama kusimamia uuzwaji wa nyumba hiyo.

Hata hivyo, ombi hilo halikufanikiwa kutokana na baadhi ya warithi kutaka nyumba hiyo isiuzwe.

Mwingira alisema ilipofika mwaka 2011 ulifanyika mnada wa hadhara ambapo Salim alifanikiwa kununua nyumba hiyo kwa Sh250 milioni.

“Tangu mwaka 2011 hadi Februari 2026 mnunuzi wa nyumba hiyo hajawahi kuingia na kutumia nyumba yake kutokana na vurugu ambazo zinakwamisha zoezi la kukabidhi nyumba hii,” amesema.

Amesema vurugu hizo zilitoka kwa msimamizi wa mirathi ambaye ni Maraya Mtambo na familia yake ambaye alikataa kutoka katika nyumba hiyo kwa madai ya kutoshirikishwa katika uuzwaji wa nyumba.

Mwingira amesema suala hilo limeamriwa katika ngazi ya mahakama kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama Kuu ambapo kwenye ngazi zote za uamuzi mnunuzi alipewa haki.

Amesema kamati ilibaini kuwa kampuni ya udalali iliyosimamia uuzaji wa nyumba hiyo haikuwa mwaminifu katika utunzaji wa fedha za warithi.

Aidha, katika mahojiano yaliyofanywa na kamati, iligundulika kuwa sehemu ya fedha hizo ilitumika kwa matumizi binafsi, jambo lililochochea mgogoro huo.

Mwingira amesema dalali angegawa pesa kwa wakati kusingekuwa na mgogoro huo uliojitokeza.

Pia, amesema baada ya kupitiwa kwa nyaraka kamati imebaini zoezi la uondoaji wa watu lilikamilika tangu Januari 19, 2026 kwa maana mnunuzi alishapewa barua na dalali aliyetumwa na mahakama.

Kutokana na changamoto hiyo, amesema kamati ilitoa ushauri wa dalali kukamatwa na kutakiwa kulipa pesa zote za warithi ambao hawakuchukua na madalali wa mahakama wafanye kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

Akieleza sababu za kutajwa kwenye kamati dalali wa uuzaji wa nyumba, Kampuni ya Sombo, Ashraf Sombo amesema pesa yote iliingia kwenye akaunti waliyoitoa na ilikuwa Sh250 milioni ambapo wachache walichukua kwa sababu ya kuridhia uamuzi wa mahakama huku wengine wakikataa uuzwaji wake.

“Waliokubali uuzwaji na kuchukua pesa ni wengi kuliko waliokataa na pesa zilizokuwa zimebaki ni Sh60 milioni,” alisema Sombo.

Dalali huyo alisema pesa hiyo kwa kipindi hicho ilikuwa kwenye benki ya Serving and Finance na sasa zipo katika Benki ya NMB na wakienda watazikuta japokuwa utaratibu wa sasa pesa inakwenda kwenye akaunti ya mahakama.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na Mwenyekiti wa kamati kwa kusema taarifa walizonazo pesa zilizobaki ni Sh64.5 milioni ambazo zilitakiwa kugawiwa katika familia mbili za Maraya na dada yake Rajabu.

“Pesa nilibaki nazo kwa ajili ya kuwalipa wahusika lakini nilisahau kwa bahati mbaya kwa sababu kulikuwa na kesi na sikuenda kutoa taarifa mahakamani,” amesema.

Amesema kesi iliyopo mahakamani inahusu uuzwaji wa nyumba ambapo mkuu wa mkoa alimuuliza kama inazuia shughuli iliyowapeleka hapo ya kutoa haki kwa mnunuzi ambapo dalali alijibu haizuii.

Kumaliza mgogoro

Februari 17, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kupitia mkutano wa wazi aliamua kuumaliza mgogoro huo wa nyumba kwa kumpatia haki mnunuzi wa nyumba ya marehemu Mtambo akieleza kuwa alinunua kihalali mwaka 2011.

Alisema akiwa na viongozi wa Wilaya ya Ilala yaani Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya hiyo, wanasheria na wananchi wamejiridhisha kuwa Maraya hana haki peke yake.

“Unaporithi mali haimaanishi hiyo mali ni yako peke yako, mpo wengi msikilizane mgawane ndiyo maana mahakama imeuza.

“Kwa mantiki hiyo kwa nini hawakwenda kuchukua pesa baada ya familia hiyo kulumbana baadhi ya watu wanachukua kodi na hawawalipi wenzao, wale wachache ambao walikataa nyumba isiuzwe ndiyo waliogoma kwenda kuchukua mgawo ili wao waendelee kuchukua kodi kwenye maduka,” amesema Chalamila.

Amesema kwa maana hiyo wamejiridhisha pesa iliyokuwa ikipatikana hapo haikuwa ikigawanywa kwa wengine na walikuwa wajanja walikuwa wakichelewesha mgogoro kwa kujua wakichukua kodi watapata pesa nyingi kuliko walizogawana.

Chalamila amesema baada ya kujiridhisha kuwa nyumba hiyo ni mali ya mirathi na kwamba kulikuwa na mashauri mahakamani yaliyotolewa uamuzi, pamoja na kukamilika kwa mchakato wa uhamisho wa nyaraka kwa mnunuzi kupitia Ofisi ya Ardhi, alifika Februari 17, 2026 kufafanua na kusimamia utekelezaji huo, akisisitiza kuwa Maraya si mmiliki halali wa nyumba hiyo.

Aliongeza kuwa, kwa mtazamo wao, watoto na wajukuu wa Maraya wamekuwa wakichelewesha mchakato huo kwa muda mrefu kwa manufaa yao binafsi, na si kwa faida ya mtu mwingine yeyote.

“Natumia uwanja huu wa Kariakoo kuonya sana tabia hii, mwisho wa siku mnakuja kumwingiza kwenye hatia huyu bibi wa miaka mingi kwa sababu ya ulafi na uroho wa mali za urithi,” amesema.

Kwa upande wa Ofisi ya Ardhi, amesema baada ya nyumba kuuzwa kwa njia ya mnada Salim alifanya taratibu za kumilikishwa kwa njia ya ‘Transmission by Operation of Law’ ambapo alipatiwa hati.

“Kwa mujibu wa usajili wa hati ni mali ya mnunuzi ndugu Salim Salehe Salim tangu Juni 2, 2011.”

Kutokana na maelezo hayo, Chalamila alimtaka mnunuzi kuanza kupafanyia kazi na jambo hilo limeanza utekelezaji wake Februari 19, 2026 kwa mnunuzi kupeleka wavunjaji katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu wa Kliniki ya Sheria, Ipyana Mlilo amesema wapo kwa ajili ya kusaidia jamii, hivyo wananchi wawe na imani nao kwenye kasoro wataeleza na kwenye msaada watasaidia.

“Tunapokea watu wa aina zote na kliniki yetu haihusiani na kamati ya mkoa, hivyo tunaomba watuamini kwani tupo hapa kwa ajili ya msaada na kwa yeyote atakayehitajika kutoa maelezo ataitwa na kufika eneo hilo,” amesema Mlilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *