Rombo. Serikali itawalipa fidia wananchi 1,142 ili kupisha ujenzi wa barabara ya Lower iliyopo Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, yenye urefu wa kilomita 10 ambayo itagharimu zaidi ya Sh28 bilioni hadi kukamilika kwake.

Hayo yamebainishwa leo Februari 19, 2026 na Meneja wa Wakala Barabara (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambaye anafanya ziara ya kikazi mkoani humo.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo ambayo kwa awamu ya kwanza inajengwa kwa kilomita 10, mpakani mwa Kenya na Tanzania, itakuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi na kiusalama kwa nchi.

Kyando amesema tayari Serikali imefanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa barabara hiyo.

Amesema  barabara hiyo itajengwa kwa kipande hicho cha lami za kilomita 10 kuanzia Ikuini hadi Kirongo chini.

“Barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami kilomita 52.8 na sasa hivi ipo katika ujenzi wa kiwango cha changarawe. Barabara hii ambayo inajengwa kwa kilomita 10 kuanzia Ikuini – Kirongo chini ambayo itagharimu zaidi ya Sh28 bilioni,” amesema Kyando.

Amesema katika utekelezaji wa barabara hiyo, wananchi 1,142 wataathirika na ujenzi huo na Serikali itawalipa fidia ya Sh14.6 bilioni.

Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema barabara hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa shughuli za kiuchumi, kijamii, utalii na kwamba ni salama kwa mpaka katika nchi ya Tanzania na Kenya.

“Ni barabara muhimu kwa uchumi na utalii na kiusalama, lakini haina miinuko wala kona na itatusaidia kusafirisha mizigo kutoka Holili Arusha, kwenda Kenya,” amesema Kasekenya.

Jenifa Shayo, mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, amesema barabara hiyo itakuwa ni msaada mkubwa kwao kwa kuwa itachochea shughuli za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *