Jua lilipotua juu ya Gaza siku ya Jumanne, safu za waumini zilisimama kuswali, si ndani ya misikiti, bali juu ya magofu yake.

Kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa vita vya miaka miwili vya Israel dhidi ya eneo hilo, Wapalestina waliukaribisha mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani chini ya usitishaji dhaifu wa mapigano, wakiswali Sala za Tarawehe katika nyua zilizojaa vifusi na katika maeneo ya ibada ya dharura yaliyotengenezwa kwa turubai na mbao.

Misikiti mingi katika Ukanda wa Gaza haipo tena.

Shirika la Habari la Anadolu limenukulu Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza, ikisema zaidi ya misikiti 1,015 iliharibiwa au kuathiriwa wakati wa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya eneo hilo. Angalau misikiti 835 ilisambaratishwa kabisa, huku mingine kadhaa ikibaki ikiwa ni mabaki matupu ya yale yaliyokuwa vituo muhimu vya kijamii na kidini katika mitaa yao.

Badala ya kuba na minara, sasa hutundikwa turubai za plastiki. Badala ya sakafu za marumaru, waumini hupiga magoti juu ya saruji isiyo sawa na mchanga.

Droni za kijasusi Israel ziliendelea kuzunguka angani katika maeneo kadhaa ya Gaza wakati sala zilipoanza, hali iliyoashiria utulivu wa mpito na usio na uhakika uliofuata miezi ya mashambulizi makali.

Katika Mtaa wa Kale wa Jiji la Gaza, wakazi walirejea katika Msikiti wa kihistoria wa Al‑Omari, mojawapo ya misikiti mikubwa na ya zamani zaidi nchini Palestina. Msikiti huo, ulioanzishwa zaidi ya karne 14 zilizopita, uliharibiwa kwa kiwango kikubwa katika shambulio lililoripotiwa mwezi Desemba 2023.

Sehemu za jengo hilo zimefunikwa kwa vifaa vya muda ili kuruhusu upatikanaji wa kiwango kidogo kwa waumini.

Kote Gaza, mandhari kama hayo yalijirudia. Hema za sala zilizosimamishwa juu ya vifusi zilijaa haraka. Baadhi ziliangaziwa kwa muda mfupi na jenereta ndogo zilizowashwa kwa saa chache tu.

Ramadhani mbili zilizotangulia zilipita chini ya mashambulizi na njaa kali, huku familia nyingi zikiwa hazina uwezo hata wa kuandaa milo ya msingi ya futari mlo wa kufungua saumu au suhoor, mlo wa kabla ya alfajiri.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yamekuwa yakitekelezwa Gaza tangu Oktoba 10, 2025, yakisitisha vita vya miaka miwili vya Israel ambavyo vimeua zaidi ya Wapalestina 72,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kujeruhi zaidi ya 171,000 tangu Oktoba 2023.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, tangu makubaliano hayo yaanze kutekelezwa Oktoba 10, majeshi ya Israel yamefanya mamia ya ukiukwaji kupitia mashambulizi ya mizinga na risasi, na kuua Wapalestina 603 na kujeruhi wengine 1,618.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *