Dar es Salaam.  Siku moja baada ya Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kutangaza kuanza mchakato wa kutoa diploma kwa wafanyakazi wa nyumbani, wadau wamesema itafanya fani hiyo iheshimiwe na kusaidia katika kuboresha malezi.

Pia, wametaka kuwepo elimu ya maadili na malezi sambamba na wanafunzi hao kufundishwa namna wanavyoweza kuzuia ukatili wanaoweza kuwafanyia watoto au kushughulikia ukatili uliofanywa dhidi ya watoto wanaowalea.

Wadau walisema hayo jana kuhusu kuanzishwa kwa mtalaa huo Veta kwa wafanyakazi wa majumbani ili kupambana na changamoto kadhaa ikiwamo kukosa weledi wa namna ya kufanya kazi zao.

Mzizi wa kuja na wazo hilo umetokana na mafanikio yaliyotokea katika mradi wa uwezeshaji wa wafanyakazi majumbani uliokuwa ukitelekezwa na Jumuiya ya Watu wa Kujitolea Ulimwenguni (CVM) kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Hoteli, Majumbani, Baa, Huduma za Jamii na Ushauri (Chodawu) ,uliokuwa unawapa mafunzo wafanyakazi hao ya mwezi mmoja mpaka mitatu na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Italia(AICS)

Katika utekelezaji wa mradi huo uliokuwa wa miaka mitatu ambao ulifungwa juzi, CVM na Veta waliandaa mtalaa maalumu kwa ajili ya  kuwafundishia wafanyakazi hao ambao umeleta mabadiliko makubwa katika utendaji kazi zao.

Mtalaa huo unaanzishwa ili kuwawezesha wafanyakazi wa majumbani kuwa na elimu ya namna ya kulea watoto, wazee, kuandaa vyakula na kutandika vitanda.

Akitoa maoni yake ya kuanzishwa kwa ngazi hiyo ya elimu, Florentina Senya ambaye ni mtaalamu kutoka Malezi Tiki Tanzania amesema itaongeza hadhi ya kazi husika.

Amesema hiyo ni kwa sababu kwa miongo mingi iliyopita kazi za ndani zimekuwa zikifanywa kimya kimya bila mikataba thabiti, mafunzo rasmi na hazikuwa na ulinzi wa haki za msingi.

“Nadhani katika hili wangeweka msisitizo katika maadili na malezi kama wanavyoweka katika fani nyingine, uandaliwe mtalaa wa malezi na maadili msisitizo uwekwe hapo, mara baadhi ya familia huwa na changamoto hasa katika mgawanyo wa majukumu,” amesema.

Amesema kukosekana kwa mgawanyo wa majukumu umefanya baadhi ya wafanyakazi kujikuta katika mrundikano wa kazi kwa kisingizio cha kulipwa, hivyo imekuwa ikiwafanya kuchelewa kulala na wa kwanza kuamka.

Amesema ili kupata mtalaa bora zaidi mama wa nyumbani washirikishwe kutoa maoni yao ya nini kinafaa kufundishwa, kwa kuwa wao ndiyo wanajua upungufu uliopo katika utumishi wa wasichana hao badala ya watu wa ngazi za juu kukaa na kuamua kitu gani kifundishwe.

Ametoa angalizo pia katika namna itakayotumika kuchagua wanafunzi wa fani hiyo akionya kuwa ni vyema kutowalazimisha au kutumia njia za vichochoroni, bali wapate watu wanaopenda, waandaliwe katika namna itakayokuwa njema.

Pia, amesema baadhi ya watoto na wavulana katika hatua zao za ukuaji wamepitia ukatili wa aina mbalimbali na wengi wamekuwa na hali ya kulipa kisasi, hivyo ni vyema wajaribu kubaini kama wamepitia matendo ya ukatili na wakijua wapewe ushauri na msaada wa kisaikolojia.

“Waondolewe machungu ya ukatili waliopitia na wafundishwe namna ya kufuatilia watoto kujua kama amepitia ukatili, kufanya hivi pia kutasaidia wao kutumika kama washauri ikiwa watoto watapata changamoto,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji Wadada Consultancy, Amani Ramadhan amesema kuanzishwa kwa kozi hiyo itasaidia kupata watu sahihi kulingana na huduma ya wafanyakazi wa nyumbani.

Amesema kwa muda mrefu kumekuwa na wimbi la upatikanaji wa wafanyakazi wa majumbani wasiokuwa na weledi huku baadhi ya madalali wakiwapeleka wafanyakazi katika nyumba za watu bila kuwafahamu kwa undani au hawana historia wanayoijua.

“Pia, wanakuwa hawajafundishwa wanampeleka kwa familia ya mtu bila kujua anakwenda kufanya nini, itasaidia watu kupata watu sahihi,” amesema.

Amesema moja ya jambo ambalo angetamani lifanyike ni kufundishwa namna ya kuwa na malengo wanapofanya kazi na kujitambua kuwa wanafanya kazi kwa sababu gani na malengo gani.

“Kwa sasa wengi wanafanya kazi kwa kuona hawana kitu kingine cha kufanya, wanaona wamefeli na hawana malengo kwa kupata kitu fulani. Kama watapewa elimu nzuri kuwa kazi hiyo unaweza kufanya hata ukiwa na kiwango gani cha elimu ili kujipatia kipato inaweza kuwasaidia.

“Wengi hudhani watafanya kazi hizo kwa sababu hawana kitu na kuchukulia poa,” amesema.

Wakati wao wakisema hayo, mmoja wa mawakala wa wafanyakazi wa majumbani ambaye hakutaka kuandikwa gazetini amesema itakuwa rahisi kwa watu kupata watu wanaojulikana, waliosoma ambao pia wanaweza kuwasaidia katika majukumu muhimu ya kiuchumi.

“Lakini, sidhani kama wote wataweza kumudu kuwalipa watu watakaokuwa wamesoma kwa ngazi hiyo, maana yake watatakiwa kulipwa kwa kiwango chao cha elimu, kwa hali ya sasa pekee mtu ukimuambia alipe Sh100,000 kwa wafanyakazi wa majumbani ni mtihani vipi hao waliosoma,” amesema mama huyo.

“Lakini ni jambo zuri, kwani kazi hii sasa itaheshimiwa itakuwa inafanywa na watu waliokaa darasani, wanajua wanachokifanya na walifaulu masomo yao, itaondoa dharau ndogo ndogo kutoka kwa watu kwa kuwaona wasaidizi ni watu walioshindwa maisha,” amesema.

Mmoja wa wazazi, Lucy Matiku amesema kutoa mafunzo hayo itasaidia kuboresha malezi ya watoto licha ya kuwa itakuwa gharama.

“Wafanyakazi wengi niliowahi kuishi nao walikuwa wametoka vijijini, hawajui kutumia baadhi ya vitu vya umeme, kulea mtoto na wakati mwingine unakuta mtoto amevalishwa pampasi kwa siku nzima yeye anaona ni sawa na wakati mwingine ukimuelekeza anaweza kuwa na mapokeo tofauti.

“Wengine pia tunaletewa wadogo sana, hawajui kulea watoto hana elimu ya lishe na hajui mtoto ale nini kwa wakati gani, anaweza kumlisha mtoto ugali mchana na jioni wali kama ambavyo mnakula watu wazima, ni changamoto lakini itasaidia,” amesema Matiku.

Faida za mafunzo

Mafunzo hayo yana manufaa ya moja kwa moja kwa mfanyakazi na Taifa ikiwamo kuinua hadhi ya kazi za ndani, kuongeza ujuzi wa kazi za nyumbani kwa viwango vya kitaalamu, kujifunza haki za mfanyakazi na usalama wa kazi.

Faida nyingine ni kujiandaa kufanya kazi ndani au nje ya nchi kwa kujiamini, kuongeza nafasi ya kupata ajira bora na mshahara wa haki.

Usafi wa nyumbani

Usafi wa kisasa hauishii kung’arisha sakafu, ni sayansi ya taratibu, vifaa na kemikali sahihi.

Mafunzo ya huduma ya usafi wa nyumba yanahimiza upangaji kazi kwa ratiba, utambuzi wa aina za nyuso (kioo, mbao, marumaru) na matumizi salama ya kemikali ili kuepusha madhara kwa afya na mali.

Aidha, kufua na kupiga pasi si shughuli za kubahatisha, ni ustadi unaohusisha kuchambua vitambaa kwa alama za lebo, kudhibiti joto la pasi na kuhifadhi mavazi kwa mpangilio unaoepusha unyevu na harufu.

Kwa familia nyingi, ubora wa usafi umeanza kuonekana kama kipimo cha hadhi na ustawi, hapo ndipo taaluma hii inapata heshima inayostahili.

Huduma za chakula nyumbani imebadilika, msaidizi wa jikoni au mpishi wa familia anatakiwa kujua si tu mapishi ya vyakula vya kawaida, bali pia misingi ya vyakula vya kimataifa kuanzia pilau, biriani, pasta na saladi za kisasa.

Usafi wa jikoni ni nguzo kuu, hapa, mafunzo huzingatia uhifadhi sahihi wa chakula kwa kuzingatia joto linalofaa, kutenganisha vyakula vibichi na vilivyoanikwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *