
Unguja. Wakati baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakieleza wasiwasi wao kuhusu sababu za Serikali kuendelea kukopa na kuongeza deni la Taifa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayokwamishwa na utegemezi wa misaada ya wahisani.
Dk Malik ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 19, 2026, alipokuwa akijibu na kuhitimisha hoja mbalimbali za wajumbe kuhusu Mpango wa Taifa na mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2026/27, katika mkutano wa 11 wa Baraza la Wawakilishi uliofanyika Chukwani, Zanzibar.
Akifafanua kuhusu suala la mikopo, amesema ni kweli Serikali inakopa, wakati mwingine kwa mtazamo wa kibiashara, ili kuhakikisha miradi yenye tija inatekelezwa kwa wakati.
Amesema katika vipindi vya nyuma, miradi mingi ya kimkakati ilitegemea wafadhili ambao mara kadhaa walikataa kuifadhili kwa sababu mipango ya Serikali haikuendana na taratibu zao.
“Tumebaini kwamba ili tujenge ni lazima tukope, kisha turejeshe baadaye. Taasisi za fedha zimeona mantiki ya mpango wetu na zinatuamini,” amesema.
Ameongeza kuwa pamoja na kukopa, Serikali inaendelea kukuza mapato ya ndani na uchumi unazidi kuimarika, hivyo utaratibu huo una manufaa na utaisaidia nchi kufikia malengo yake kwa haraka zaidi kuliko kuendelea kutegemea misaada ya wahisani.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kwa sasa Serikali inajenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 1,200 kwa fedha zake, pamoja na bandari, viwanja vya ndege na viwanja vya michezo vya kimataifa bila kutegemea wafadhili. Amesisitiza katika kipindi cha nyuma, utegemezi wa misaada haukuwezesha hata ujenzi wa kilomita 20 za barabara ya lami.
Hata hivyo, baadhi ya wawakilishi wametaka Serikali kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kufanya tathmini ya kina ya miradi ya maendeleo badala ya kuendelea kuwasilisha vyanzo vilevile vya mapato kila mwaka huku deni la Taifa likiongezeka, ingawa linaelezwa kuwa bado ni himilivu.
Wameishauri pia serikali za mitaa kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa kodi, wakisema ni vyema kupanua wigo wa walipakodi badala ya kuendelea kuwabebesha mzigo wananchi wa kawaida.
Mwakilishi wa Chambani, Mahmoud Shineni Ali (ACT-Wazalendo), amesema bado hakuna ubunifu wa kutosha katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato.
Amedai Tume ya Mipango haijafanya tafiti za kutosha kubaini vyanzo vipya, na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) inapaswa kutoa elimu zaidi kwa walipakodi badala ya kuwabana wafanyabiashara.
Ameeleza pia kuwa katika mamlaka za serikali za mitaa, makadirio ya mapato na makusanyo halisi bado yanatofautiana kwa kiasi kikubwa. Alipendekeza kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji, hususan kwenye mabango ya matangazo, ili kuongeza mapato bila kuwasumbua wananchi.
Katika sekta ya utalii, baadhi ya wajumbe wamesema bado kuna utalii wa kimazoea na kuitaka Serikali kuandaa mkakati mahsusi wa kuongeza idadi ya watalii.
Ripoti ya Serikali inaonyesha lengo la kuongeza watalii kutoka 400,000 hadi 500,000, lakini walisema idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo visiwani humo.
Aidha, wamesema hakuna ukumbi wa mikutano wa kimataifa Zanzibar, jambo walilosema linahitaji ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kuanzisha miundombinu hiyo.
Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman amesema vipaumbele na malengo yamekuwa yakijirudia kila mwaka bila tathmini ya kina ya utekelezaji wake. Ameonya kuwa utegemezi wa bajeti kwa wahisani bado ni mkubwa.
Ametoa mfano wa bajeti ya miradi ya maendeleo ya Sh5 trilioni, ambapo takribani Sh3.5 trilioni zinatoka kwa wahisani sawa na asilimia 26, huku Sh3 trilioni sawa na asilimia 74 zikitoka ndani ya Serikali.
Amesisitiza kuwa nchi haiwezi kutekeleza kikamilifu mipango yake kwa kutegemea wahisani.
Kadhalika, ameitaka Serikali kuchunguza iwapo misamaha ya kodi inaleta tija inayotarajiwa, akibainisha kuwa misamaha imeongezeka kutoka 240 hadi maombi mapya 40 katika kipindi cha sasa.
“Lazima tujiulize fedha kiasi gani zinapotea kupitia misamaha hiyo na manufaa yake ni yapi,” amesema.
Kwa upande wake, Fatma Mandoba (Viti Maalumu) amependekeza kuongezwa kwa kodi kwenye vilevi, pendekezo ambalo Dk Malik alisema litaangaliwa kwa kina kabla ya uamuzi kufanyika.
Akihitimisha, Waziri Malik amesema Serikali imepokea michango yote iliyotolewa na wajumbe na itaifanyia kazi ili bajeti itakayowasilishwa Juni mwaka huu iwe imara zaidi na inayojibu changamoto zilizobainishwa.