Rombo. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza utekelezaji wa haraka wa mradi wa maji katika Ziwa Chala, unaojengwa katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, ukitarajiwa kutatua kero ya maji wilayani humo.

Kukamilika kwa mradi huo wa maji kutawanufaisha wananchi 34,104 waliopo katika vijiji 14 vya ukanda wa chini wa wilaya hiyo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Februari 19, 2026 katika eneo la Masekini, kata ya Marangu Kitowo, Dk Mwigulu amesema atahakikisha anafuatilia mradi huo hatua kwa hatua ili wananchi waondokane na tatizo hilo la maji.

“Mawaziri mnaosimamia miradi hii, mtakuwa na kazi kubwa kwelikweli kwa sababu nitafuatilia kila dakika, jambo hili sio la Serikali tu, ni la nyumbani na nitakuja niende mpaka Ziwa Chala pale. Nitafuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wake, sasa hapa hili jambo nina masilahi nalo,” amesema Dk Mwigulu.

Taarifa ya mradi

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Rombouwasa), Tumaini Marandu amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Sh8.6 bilioni hadi kukamilika kwake.

“Utekelezaji wa mradi wa maji wa Ziwa Chala ambao unaanza mwaka huu wa fedha 2026/27 utaongeza uwezo wa uzalishaji wa mita za ujazo 8,740 kwa siku,” amesema Marandu.

Aidha mradi huo utakapokamilika utaongeza uzalishaji wa maji kufikia lita za ujazo 34,440 kati ya mahitaji ya lita za ujazo 34,775 sawa na upungufu wa maji lita za ujazo 335.

“Mradi huu wa Ziwa Chala utakapokamilika utaongeza uwezo wa uzalishaji kufikia lita za ujazo 34,440 kati ya mahitaji 34,775, kwa hiyo tutakuwa na upungufu wa lita za ujazo 335,” amesema Marandu.

Ameongeza: “Mradi huu wa Ziwa Chala unatarajia kugharimu Sh8.6 bilioni na utanufaisha wananchi wapatao 34,104 waliopo katika vijiji 14 vya ukanda wa chini wa wilaya hii.”

Aidha, amesema Serikali imeshatanga zabuni kwa mradi huo na tayari mchakato wa upembuzi yakinifu unaendelea.

Naye, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara hiyo itahakikisha taratibu zote zinafanyika kwa haraka ili kuanza kwa mradi huo.

“Kwa kuwa tupo katika hatua ya upembuzi yakinifu katika mradi huu, nimeelekeza mchakato huu ufanyike kwa haraka na wizara tutatoa fedha kwa haraka ili uanze kutekelezwa,” amesema Waziri Aweso.

Anna Assenga, mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, amesema kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya huduma ya maji.

“Hapa kwetu Marangu Kitowo, tangu mwaka 2025 hatujapata maji, tunateseka, wanasema kuna mgao wa maji lakini ikifika siku ya inayoonyesha yatatoka huku kwetu hatupati kitu  ,” amesema mwananchi huyo.

Amedeus John, mkazi wa Marangu Kitowo, amesema tatizo la maji katika eneo lao ni la muda mrefu na halijawahi kupatiwa ufumbuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *