WAZIRI Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ameipa Wizara ya Maji kipindi cha wiki mbili kuhakikisha inakamilisha mchakato wa upatikanaji wa mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Ziwa Chala.
Ametoa agizo hilo leo Februari 19 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Marangu-Kitowo, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kupokea taarifa za ujenzi wa Mradi wa Maji kutoka chanzo cha ziwa Chala, Ujenzi wa mradi wa barabara Holili(Rotima)-Tarakea(Nayemi), pamoja kuweka jiwe la msingi la Shule ya Sekondari Stephen Moshi Technical.

Dk Mwigulu amesema kuwa ujenzi wa mradi huo unapaswa kuanza kutekelezwa kwani unategemewa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Wilaya nzima ya Rombo.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuwa Wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa mradi huo na watahakikisha katika kipindi cha siku 14 wanampata mkandarasi wa mradi huo.

Mradi wa maji Ziwa Chala unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bilioni 8.66 na utanufaisha wananchi 34,104 katika vijiji 14 vya wilaya ya Rombo.
Kadhalika Dk Mwigulu amemuagiza Waziri wa Fedha kuhakikisha anatafuta fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya awali kwa mkandarasi ili aanze ujenzi wa mradi wa barabara Holili(Rotima)-Tarakea(Nayemi) kilomita 52.8.

Mradi huo ambao utagharimu kiasi cha sh bilioni 28 unapita mpakani mwa Tanzania na Kenya na unategemewa kusaidia kukuza shughuli za kijamii, kiuchumi pamoja na utalii.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Stephen Moshi Technical ambayo itagharimu sh bilioni 1.6 Dk Mwigulu amesema kuwa shule hiyo ni kielelezo cha uwepo wa kiongozi mwenye maono na mipango.

“Ndani ya muda mchache sana zimejengwa shule zaidi ya 103 za aina hii nchi nzima,” amesema Dk Mwigulu.