Dar es Salaam. Kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) kimeanza baada ya akidi ya wajumbe kukamilika, tayari kwa kutekeleza majukumu yake ya kupitia ajenda za kuitisha mkutano mkuu wa dharura kwa ajili ya kuchagua viongozi wapya wa juu wa chama hicho.

Kikao hicho kinafanyika katika Ukumbi wa Shaban Mloo, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni, kikiongozwa na katibu wa muda, Mussa Mbarouk, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Tanga.

Kulingana na Katiba ya chama hicho, kuna wajumbe hai 43 wanaotambulika. Ili kikao hicho kiwe halali na uamuzi wake utambuliwe bila shaka, ni lazima kihudhuriwe na angalau wajumbe 25. Hadi kikao kianze, jumla ya wajumbe 27 walikuwa wamejiandikisha kuhudhuria.

Kwa msingi huo, uamuzi utakaotolewa katika kikao hicho, ambacho tayari kimepata baraka kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, utatambuliwa na ofisi hiyo kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa kuchagua viongozi wapya kesho. Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho chama hicho kimekumbwa na mgogoro wa uongozi kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, uliotolewa kupitia barua yake ya Februari 13, 2026, wa kutengua uongozi wa Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na wenzake watano.

Sababu ya kutengua uchaguzi huo uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, ni kwamba washindi waliotangazwa hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama hicho, hivyo mchakato huo ulipaswa kurudiwa.

Uamuzi huo umesababisha wanachama kugawanyika katika makundi mawili; kundi linaloongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba, linalodai litaenda mahakamani kupinga uamuzi wa Msajili kwa madai kuwa halikupatiwa haki ya kusikilizwa dhidi ya malalamiko yaliyowasilishwa.

Kwa upande mwingine, kundi linaloendelea na kikao hicho cha Baraza Kuu linaunga mkono uamuzi wa Msajili na linatekeleza maagizo yake kwa lengo la kuhakikisha chama kinapata viongozi wapya na kuvuka kipindi cha mpito kinachokikabili.

Wakati kikao hicho kikiendelea, ulinzi wa Jeshi la Polisi umeimarishwa katika makao makuu ya chama hicho, huku wajumbe wa mkutano mkuu kutoka mikoa mbalimbali wakiwasili tayari kwa uchaguzi wa viongozi wapya kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *