
Dodoma. Chuo cha Uhasibu cha Arusha (IAA) wametangaza kuanzisha kozi mpya katika kipindi hiki ili kuendana na mahitaji ya soko.
Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Februari 20, 2026, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema malengo ya sasa ni kuwafuata vijana waliko na kwenda kuwafundisha kile kitakachowafaa hata katika mazingira yao na kuwafanya wasikimbilie mijini.
Profesa Sedoyeka ametaja sababu za kuongeza kozi hizo ni kuendana na matakwa ya soko la ajira na mahitaji ya nchi kwa wakati huu.
Miongoni mwa kozi zinazotarajia ni utalii, ambao amesema unapewa kipaumbele na soko lake ni kubwa kama vijana wataongeza ubunifu kwa kiwango kinachotakiwa.
“Baadhi ya mitaala tunakwenda kufundisha kulingana na mazingira ya eneo husika, mfano huu wa elimu ya kidijitali tunajua ndiko dunia inakoelekea sasa; lazima nasi twende huko na tutafundisha ndani na nje ya mipaka ya nchi,” amesema Profesa Sedoyeka.
Mkuu huyo amesema baadhi ya maeneo watajikita zaidi kufundisha uhasibu na kodi katika mikoa ambayo imechangamka kibiashara, ikiwemo Geita.
Katika maelezo yake, anasema hadi sasa IAA ina jumla ya wanafunzi 20,993 wanaosoma chuoni na katika matawi yaliyopo baadhi ya mikoa.
“Tunaongeza nguvu ya wahadhiri kwani tumewapeleka masomo wahadhiri wetu 20 wanaosoma ndani na nje ya nchi kwa ngazi mbalimbali za ujuzi; hawa, wakirudi, watakuwa msaada mkubwa,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema wametengewa Sh8.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mafunzo cha mambo ya Teknolojia (ICT) ili kuwa na maboresho katika matumizi ya tehama kwa vijana wabunifu.
Kabla ya kutengwa kwa fedha hizo, Sh4 bilioni zilishatolewa kwa ajili ya kujenga madarasa katika kampasi za chuo mikoani, baada ya kukamilisha ujenzi na ukarabati wa madarasa ya makao makuu ya chuo ambayo yaligharimu Sh900 milioni kwa bajeti iliyokwisha.