Dar es Salaam. Kampuni ya Continental Reliable Clearing (T) Limited (CRC) imekwama katika harakati zake za kukwepa kulipa mkopo wa Dola za Marekani 10,139,664.95 (zaidi ya Sh26.36 bilioni) iliouchukua kutoka benki za Equity, baada ya Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imetupilia mbali kesi yake ya kupinga kurejesha mkopo huo.

Kampuni hiyo ya CRC ilifungua kesi hiyo dhidi ya benki za Equity Tanzania (EBT) na Equity Kenya (EBK) ikipinga madai ya benki hizo ya malipo mkopo wa Dola za Marekani 10.13 milioni (zaidi ya Sh26.36 bilioni) ambao zilikuwa zimeipatia kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013.

CRC ilichukua hatua hiyo baada ya benki ya Equity Kenya kupitia wakala wake, Equity Tanzania kuiandikia barua ikiipa siku 21 kurejesha mkopo huo.

Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023, ilikuwa ikidai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.

Hivyo, ilikuwa ikiiomba mahakama itoe tamko kwamba wadaiwa wamekiuka makubaliano ya mikopo na wajibu wa kibenki kwa mlalamikaji.

Kwamba, mlalamikaji (CRC) amelipa na kumaliza mikopo yote na kwamba kiasi cha Dola za Marekani 10,139,664.95 kinachodaiwa na wadaiwa kama deni lililosalia si halali na hakipo.

Kwamba hati za mikopo za Mei 29, 2018,  Novemba 3, 2021 na Januari 19, 2022 ni batili na  kwamba hati za mikopo za Februari Mosi, 2019 na Septemba 17, 2020 zilitimizwa kwa sehemu na mdaiwa wa kwanza na hazikutimizwa kabisa na mdaiwa wa pili.

Kwamba rehani zote zilizotekelezwa kwa manufaa ya wadaiwa ni batili mahakama itoe amri ya kufuta rehani, hati ya dhamana ya kampuni, dhamana binafsi na dhamana nyingine zote zilizotolewa na mlalamikaji au wadhamini wake ili kuhakikisha ulipaji wa madeni kwa washtakiwa.

Vilevile, iliomba mahakama itoe tamko na amri kwamba barua za madai na notisi za ukiukwaji wa rehani zilizotolewa na washtakiwa ni batili.

Maombi mengine yalikuwa ni tamko kwamba mdaiwa wa pili, Equity Kenya, haina leseni ya kufanya biashara ya kibenki au biashara yoyote nchini Tanzania na inafanya biashara kinyume cha sheria na kanuni zinazosimamia shughuli za kibenki nchini;

Mwisho iliomba tamko kwamba Equity Kenya hajatoa mkopo wowote kwa mlalamikaji; fidia ya jumla itakayopimwa na mahakama; gharama za shauri; na nafuu nyingine yoyote itakayoonekana inafaa kutolewa na mahakama.

Hata hivyo, Mahakama katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji, Dk Mwajuma Kadilu, Februari 13, 2026 imeitupilia mbali kesi hiyo ikisema kuwa mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake.

Badala yake imesema kuwa imethibitika kuwa mlalamikaji alipokea na kutumia mikopo kutoka kwa wadaiwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2018 na 2022, na hakuwahi kuurejesha, hivyo akamuru fedha hizo zirejeshwe.

“Kutokana na uchambuzi na rejea za kisheria zilizotajwa hapo juu, Mahakama hii inaona kuwa mlalamikaji hastahili kupata nafuu yoyote aliyoomba katika hati yake ya madai,” amesema Jaji Kadilu baada ya kuchambua na kujadili ushahidi wa pande zote na kuhitimisha:

“Kwa hiyo, shauri hili linatupiliwa mbali kwa kukosa mashiko, na kwa gharama.”

Madai ya CRC

Kwa mujibu wa mlalamikaji, katika hati zake za madai na wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Equity Kenya imetajwa katika hati za mikopo za Mei 29, 2018, Novemba 3, 2021 na  Januari 19, 2022 kama mkopeshaji mwenza na Equity Tanzania.

Hata hivyo, hakuwahi (mdai CRC) kupokea mkopo wowote kutoka kwake Equity Kenya.

Kwa mujibu wake hati ya mkopo ya Mei 29, 2018 ilitoa ukomo wa Barua ya Mkopo (Letter of Credit – LC) wa Dola za Marekani 3 milioni ambao haukutekelezwa.

Hati ya mkopo ya Novemba 3, 2021 ilitoa mikopo mitatu: mkopo wa Dola za Marekani 6,712,268 kutoka kwa Equity Kenya; mkopo wa Dola za Marekani 4,470,265.41; na mkopo wa Dola za Marekani 1 milioni kutoka kwa Equity Tanzania.

Hata hivyo, mikopo hiyo haikutolewa kwake mlalamikaji na Equity Kenya, ilhali mlalamikaji alilipa kikamilifu mikopo aliyopata kutoka kwa Equity Tanzania.

Kuhusu mikopo kutoka Equity Tanzania, CRC ilidai kuwa ilikuwa akirejesha mikopo hiyo na kwamba Equity Tanzania mara kwa mara ilithibitisha kuwa akaunti yake ya mkopo ilikuwa katika hali nzuri.

Hata hivyo, ilidai kuwa Equity Tanzania ilikuwa ikisimamia vibaya mikopo yake.

Ilifafanua kuwa Equity Tanzania ilikuwa ikidai madai yasiyo ya haki, ikitoa takwimu zisizo sahihi za deni lililosalia, ikijihusisha na utoaji mikopo kwa masharti kandamizi, kubadilisha viwango vya riba bila makubaliano, na kusajili mikopo hiyo Tanzania na Kenya bila taarifa yake.

Pia, ilidai kuwa hati za mikopo za Februari Mosi, 2019 na Septemba 17, 2020 hazikutekelezwa na Equity Kenya na zilitimizwa kwa sehemu tu na Equity Tanzania.

CRC ilidai kuwa Equity Kenya, kwa msaada wa Equity Tanzania, iliingia makubaliano ya mikopo nchini Tanzania bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na pia ilishindwa kuzingatia matakwa ya usajili wa mikopo ya nje.

Utetezi wa wadaiwa

Wadaiwa katika hati ya utetezi wa pamoja walikanusha madai ya mlalamikaji wakidai kuwa hastahili nafuu zozote alizoziomba na walidai kuwa mlalamikaji CRC ilikiuka masharti ya mikopo kwa kushindwa kulipa kama ilivyokubaliwa.

Kwa mujibu wa wadai, huduma za kibenki na mikopo yote aliyopata mlalamikaji zilitolewa na wadaiwa wote wawili kulingana na masharti ya kila hati ya mkopo na dhamana zilizotekelezwa.

Mei 2018 walitoa mikopo ya ziada kwa ajili ya ununuzi wa malori na trela, na mlalamikaji alibadilisha dhamana zilizokuwepo na kutoa dhamana zaidi kwa manufaa ya washtakiwa wote.

Baadaye, Februari 2019, walitoa mikopo mingine yenye jumla ya Dola za Marekani 18,700,000, iliyolindwa kwa marekebisho zaidi ya dhamana na dhamana mpya kwa manufaa ya washtakiwa wote.

Novemba 2021, mikopo ya muda na LC iliunganishwa kuwa mkopo mmoja ikahuishwa kuendelea kufadhili gharama za uendeshaji wa biashara ya usafirishaji wa mafuta.

Mbali na dhamana zilizokuwepo, mlalamikaji aliweka rehani za kisheria juu ya mali zisizohamishika zenye Hati za Umiliki Na. DSMT 1010470 na Na. 3472.

Katika marekebisho hayo, deni lililosalia lilikuwa Dola za Marekani 6,418,376.21, kulipwa ndani ya miezi 45 kuanzia Januari 2022 kwa malipo ya kila mwezi ya Dola za Marekani 166,000 hadi kumaliza.

Mkopo wa Dola za Marekani 4,470,000.41 na wa Dola za Marekani 1,000,000 ulitolewa na Equity Tanzania, ilhali mkopo  wa Dola za Marekani 6,712,268 ulitolewa Equity Tanzania, kwa ombi la mlalamikaji na ilitumika na haikulipwa hadi kufunguliwa kwa shauri hili.

Kufikia 25 Februari 2023, deni lililosalia lilikuwa Dola za Marekani 10,125,798.67.

Baada ya kudai marejesho ya mikopo yenye jumla ya Dola za Marekani 10,139,664.95, mlalamikaji alifungua shauri hili kuzuia hatua za urejeshaji.

Waliambatisha nyaraka mbalimbali za dhamana zilizosajiliwa kwa manufaa ya mdaiwa wa kwanza, Equity Tanzania kuhakikisha marejesho ya mikopo.

Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza ushahidi  na hoja pamoja na vielelezo vya pande Jaji Kadilu  imesema kuwa  imethibitika kuwa mlalamikaji alipokea na kutumia mikopo kutoka kwa wadaiwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2018 na 2022.

Jaji Kadilu amesema kuwa mlalamikaji aliomba mikopo hiyo kwa hiari yake mwenyewe, na hajaonesha kuwa utoaji wake uliathiriwa na shuruti, upotoshaji au ushawishi usio halali ambao ungeondoa ridhaa yake huru.

“Hawezi sasa kukataa kuwa aliitumia mikopo hiyo,” amesema Jaji Kadilu katika hukumu hiyo na kusisitiza:

“Zaidi ya hapo, pale ambapo ushahidi unaonesha kuwa fedha zililipwa kutoka kwa wadaiwa kwenda kwa mlalamikaji, bila ushahidi kuwa fedha hizo zilibaki bila kutolewa katika akaunti zake au zilirejeshwa kwa wakopeshaji, yaani wadaiwa, basi hawezi kukanusha matumizi yake.”

Amesema kuwa mdai ameshindwa kuthibitisha madai yake hivyo Mahakama imeshindwa kuamini madai yake ya kwamba hakuwahi kupokea mikopo kutoka kwa mdaiwa wa pili na kwamba alilipa kikamilifu mikopo aliyopokea kutoka kwa mdaiwa wa kwanza.

Pia Jaji Kadilu amesema kuwa mdaiwa wa pili Equity Kenya alizingatia matakwa ya kisheria kuhusu utoaji wa mikopo ya nje nchini Tanzania.

Amesema kuwa wadhamini wa mikopo katika kesi hiyo wanawajibika sawa na mlalamikaji na kwmba Mahakama hii haiwezi kumsaidia mlalamikaji kuwazuia wadaiwa kurejesha mikopo waliompa.

Katika usikilizaji, mlalamikaji aliwakilishwa na Wakili Frank Mwalongo na Wakili Shaba Mtung’e; Equity Tanzania aliwakilishwa na Wakili Emanuel Saghan; na Equity Kenya aliwakilishwa na Wakili Mpaya Kamara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *