Dar es Salaam. Chini ya jua kali katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, makundi ya wananchi yakiwa yameshika nyaraka mbalimbali wakisubiri kwa hamu kusikilizwa, si kwa kesi za jinai, bali kwa maumivu ya migogoro ya ardhi.

Ndani ya siku chache tangu kuanza kwa Kliniki ya Sheria, migogoro ya ardhi imeibuka kuwa kilio kikubwa, ikifichua namna umiliki usio rasmi, mipaka tata na madai ya fidia vinavyoendelea kuwatesa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za kliniki hiyo, ndani ya siku tatu tangu kuanza kwa Kliniki ya Sheria Februari 16, 2026, tayari mashauri 90 yamesikilizwa ambapo baadhi yake yametafutiwa ufumbuzi.

Katika kliniki hiyo ambayo inatarajiwa kufikia tamati Februari 22, 2026, wapo wananchi waliodai kuporwa mashamba ya urithi, wengine wakilalamikia fidia huku baadhi wakieleza hofu ya kupoteza makazi yao kutokana na hati tata. Hii ikiwa ni ishara kuwa ardhi, rasilimali muhimu zaidi ya maisha, imegeuka chanzo cha migogoro isiyoisha.

Akizungumza na Mwananchi Februari 20, 2026 kuhusu migogoro hiyo katika kliniki hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Silinde Gumada, amesema migogoro mingi inayoripotiwa inachangiwa na sababu za kijamii, kiuchumi na kisheria.

Kwa mujibu wa Gumada, ukuaji wa idadi ya watu umeongeza presha ya mahitaji ya ardhi kwa ajili ya makazi na biashara. Hali hiyo imesababisha ushindani mkubwa na kuibua migogoro ndani ya familia na kati ya majirani.

“Baadhi ya wananchi waliofika kudai haki zao walieleza kuwa mashamba ya urithi yamegombaniwa baada ya kugawanywa bila kufuata taratibu rasmi. Hata yaliyofuata taratibu yamekuwa na utata kwenye ulipaji wa fidia,” amesema Gumada.

Kliniki hiyo imebaini kuwa watu wengi bado wanamiliki ardhi kwa mfumo wa kimila bila kuwa na hati miliki. Hivyo, kukosekana kwa nyaraka halali kunasababisha watu zaidi ya mmoja kudai eneo moja, hasa katika maeneo yanayokua kwa kasi mijini.

Baadhi ya waliojitokeza wamedai ardhi zao zilichukuliwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia Wizara ya Ardhi, hivyo wananchi wamekuwa wakiomba tathmini huru ya fidia na uwazi zaidi katika mchakato wa utoaji wa ardhi kwa wawekezaji.

Wakazi wa Dar es Salaam waliofika kwenye kliniki ya sheria inayofanyika Mnazimmoja, jijini Dar es Salaam wakiwa wanasubiri huduma

Mbali na hilo, Gumada amesema wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria za ardhi kama Land Act na Village Land Act, hali inayowafanya kushindwa kufuata taratibu sahihi za kisheria.

Gumada amewahimiza wananchi kutumia fursa ya kliniki hiyo kupata elimu ya sheria na ushauri wa kitaalamu ili kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

Mkazi wa Vijibweni, Wilaya ya Kigamboni, Benjamini Mayala amefika katika kliniki hiyo kwa ajili ya kupata msaada wa kulipwa fidia ya eneo lao tangu mwaka 2019, baada ya Serikali kuliingiza katika mpango wa uwekezaji na kumkabidhi mwekezaji ekari 150 na Halmashauri ya Kigamboni ekari 152.

“Baada ya uamuzi wa Serikali kuruhusu uwekezaji katika eneo hilo, kulifanyika mgawanyo wa ardhi ambapo sehemu ilikabidhiwa rasmi kwa mwekezaji, huku jukumu la ulipaji wa fidia kwa wananchi likibaki chini ya usimamizi wa mamlaka husika za Serikali,” amesema Mayala.

Amesema uamuzi huo ulitolewa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, baada ya kuona mwekezaji kutoweza kuwalipa wamiliki wa eneo hilo. Hivyo, eneo lililobaki lilipelekwa halmashauri kwa ajili ya kuuza na walitakiwa kulipwa fidia baada ya kuachia eneo hilo.

Mayala amesema tangu mwekezaji aingie mwaka 2019, bado hakuna fidia iliyolipwa kwa baadhi ya wanufaika, licha ya eneo hilo kusajiliwa kwa jina la mwekezaji.

“Eneo letu linasoma title ya mwekezaji, lakini sisi hatujalipwa fidia. Hatuwezi kuendeleza eneo hilo kwa jambo lolote. Tulichoamua ni kumzuia mwekezaji kutoendeleza eneo hilo hadi tutakapolipwa fidia, na ameungana na sisi katika jambo hilo,” amesema Mayala.

Mgogoro wa umiliki, nyaraka

Chanzo kingine cha kuchelewa kwa fidia, kwa mujibu wa Mayala, ni kuwepo kwa familia nyingine zilizowasilisha madai ya umiliki zikidai eneo hilo ni lao tangu mwaka 1959.

Amesema kutokana na sintofahamu hiyo, kesi ilifikishwa mahakamani na kila mmoja alitakiwa kupeleka nyaraka zake. Watu hao walipeleka nyaraka zilizochapishwa huku Mayala akipeleka nyaraka zilizoandikwa kwa mkono.

“Mahakama baada ya kuona mkanganyiko huo waliamua kutupilia mbali mashauri yaliyowasilishwa na familia hiyo kwani walidai wanamiliki kiwanja tangu 1959, lakini wakapeleka nyaraka za mwaka 1989 zikiwa zimechapishwa, huku mimi nikipeleka nyaraka za mwaka 1994 zikiwa zimeandikwa kwa mkono na ushahidi wake,” amesema Mayala.

Amesema baada ya mahakama kuamua kesi hiyo, walirudi halmashauri kuendelea na mchakato wa fidia. Wakiwa katika shughuli hiyo, familia hiyo ikarudi tena na kusababisha kusimamishwa kwa mchakato, jambo ambalo hawana majibu nalo hadi sasa.

Hata hivyo, amesema wao wakiwa wanasubiri fidia yao, eneo hilo limekuwa likiuzwa na dalali na kupewa hati za umiliki wateja walionunua.

“Sijui kuna kitu gani kinaendelea. Hadi sasa tunachoomba sisi ni kukutanishwa na uongozi wa juu ili utoe kauli tena, ili tuweze kupata haki yetu. Maana yupo mzee mmoja hadi amefariki bado hajapata fidia yake, hii si sawa,” amesema.

Kutokana na jambo hilo kufahamika kwa viongozi wote wa halmashauri hiyo, ameamua kufika Kliniki ya Sheria ili kupata msaada wa kulipwa fidia zao kulingana na thamani ya sasa au kupewa eneo lao ambalo halijajengwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *