Moshi. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekiagiza Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) kuuza moja ya mali zake kulipa madeni ya zaidi ya Sh400 milioni yanayodaiwa na chama cha msingi Mwika kinyamvuo, kilichopo kata ya Mwika Kaskazini, Wilaya ya Moshi.

Madeni hayo yanatokana na mauzo ya kahawa yenye uzito wa kilo 40,283 ambayo yaliuzwa kupitia KNCU, lakini chama hicho bado hakijapokea malipo yao tangu mwaka 2023.

Hata hivyo, mwaka 2023 vigogo watatu wa (KNCU), walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa utata wa mauzo ya kahawa iliyozalishwa kwa kilimo hai na chama cha Msingi cha Mwika Kinyamvuo.

Awali akitoa malalamiko hayo mbele ya Waziri Mkuu huyo, mmoja wa viongozi wa chama hicho, Glory Sam, amesema tangu mwaka 2023 wamezunguka kutafuta haki yao bila mafanikio.

“Tulikuwa vyama vya msingi 11, tulipitisha kahawa yetu katika Chama Kikuu cha Ushirika (KNCU) mwaka 2021/2022 tulipopeleka kahawa ndio ikawa basi tena hata mabaki na nyongeza, tumezungushwa tangu mwaka huo na mimi nimefika Dodoma kwa Mrajisi Mkuu, Dk Ndiege na Waziri Hussein Bashe kipindi hicho mwaka 2023,”amesema

Amesema, licha ya Mrajisi kuunda tume ya uchunguzi kuhusiana na madai yao bado hawajalipwa fedha zao hali ambayo amesema imekuwa ni changamoto ya muda mrefu na kwamba mpaka sasa wamelipwa Sh95 milioni pekee.

“Tume iliyoundwa wakaikagua KNCU na kuichunguza, tume ile ilirudi na ikaona wakulima wanahaki ya kulipwa maana hakuna mahali walipofanya makossa, ikaenda hivyo mpaka leo tumepiga sana kelele hapo katikati, chama chetu kikawa kimelipwa Sh95 milioni mpaka leo hakuna jambo jingine ambalo tumelipwa tupo hapa tunalia miaka mitano watu wamekufa tumebaki wajane, hatuna kinacholipwa,”amesema Mwanachama huyo

Akijibu malalamiko, Mwenyekiti wa KNCU, Julius Mollel amesema tayari wamekaa pamoja na chama hicho na wakakubalina kwamba watalipa fedha hizo kwa awamu, mwaka wa fedha 2026/27.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu tayari tumeshakubaliana mwaka wa fedha unaoanza tugalipa hizo fedha na jana walisaini hizo fedha na tutalipa kwa awamu na nishawahakikishi fedha zitalipwa na mimi nimeteuliwa hapa nina miaka miwili tangu tatizo litokee na nimeanza kushughulikia na nimshalipa Sh95 milioni,” amesema Mwenyekiti huyo

Amesema, “Timu ilifika ikafanya uhakiki na inajua hayo madeni hivyo tutalipa kwa awamu kadri fedha zitakapopatikana na tumekubaliana jana.”

Mmoja wa viongozi wa chama cha msingi Mwika kinyamvuo, Glory Sam.

Akitoa maelekezo kwa uongozi wa KNCU, Dk Mwigulu ametaka fedha zipatikane kwa haraka na kulipa madeni ya chama hicho cha msingi.

“Tangu mwaka 2023 mnataka kulipa kwa awamu , muuze hata mali hawa wananchi walipwe, nyie mnakaa mnadunda na mnamiliki fedha za wananchi, mna mashamba nyumba tafuteni kimojawapo hii Sh400 milioni ipatikane wananchi walipwe fedha zao,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema, “Hatuwezi kukaa na jambo moja mwaka wa kwanza, wa pili watatu na wanne watu wanaumia, kama chama hamuwezi kulipa wananchi mnakaa nacho cha nini. Kila siku siku watu wanalia, deni lao limeshamaliza miaka mitano. Nambieni mnauza lini mnalipa lini hawa wananchi walipwe kwa mara moja.”

“Nataka Jumatano mkae mtoke na majibu, Mkuu wa Mkoa ukae nao, wakija na majibu ya ovyo wote nitawaweka ndani mpaka muwalipe ndio nitawatoa,.msiniletee mimi mambo ya kipuuzi puuzi, ya kipumbavu pumbavu hapa,” amesema Dk Mwigulu

Hata hivyo chama hicho kimesema kitakaa Jumatano ijayo na kuja na majibu ya mwafaka wa fedha za wanachama hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *